Kanisa la Anglikan lasaidia matibabu



Mwanamke aliyefanyiwa ukatili wa kijinsia kwa kukatwa mkono na sehemu za siri na anayedaiwa kuwa mume wake, amepata msaada wa kuendeleza matibabu yake kutoka Kanisa la Anglikana Jimbo la Mara kupitia kitengo cha maendeleo ya jamii.
Akizungumzia msaada huo, Meneja Mradi wa Maendeleo ya Jamii wa kanisa hilo, Theophir Kayombo alisema kanisa limeamua kumsaidia mama huyo baada ya kumsikia akitoa ushuhuda katika Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani ambayo kimkoa yalifanyika wilayani Bunda.
Alisema kanisa liliguswa na ukatili aliofanyiwa mama huyo kwa kufuatwa nyumbani kwake usiku akiwa na watoto wake na kuanza kukatwa sehemu mbalimbali za mwili wake.
Kayombo alisema mama huyo alikuwa katika matibabu ambayo hata hivyo amepewa rufaa ya kwenda Hospitali ya (KCMC) Moshi kwa matibabu zaidi na kwamba kanisa hilo la Anglikan kupitia ktengo chake cha huduma na maendeleo kwa jamii litahakikisha linamgharimia mama huyo hadi pale atakapopona tatizo hilo linalomsumbua.
Aidha aliiasa jamii kuhakikisha wanawakinga wanawake na watoto wao na wananchi kwa jumla na vitendo vya ukatili wa kijinsia ambavyo kwa kiasi kikubwa vimekuwa vikisababisha vifo kwa wahusika, huku wengine wakibakia kupata ulemavu wa kudumu na hatimaye kurudisha maendeleo ya jamii na Taifa kwa kushindwa kushiriki shughuli za maendeleo na wengi kuwa maskini.

Comments