Kiongozi wa dini mpya ya Sabato Matengenezo asema Kamwe hawatasitisha imani yao ya kutopeleka watoto shule wala Hospitali


Licha ya serikali kulipiga marufuku dhehebu lililoibuka katika kijiji cha Rumashi wilaya ya Kakonko mkoani Kigoma liitwalo Sabato matengenezo, mwanzilishi wa dhehebu hilo amejitokeza na kusisitiza kuendelea na imani hiyo. 

Baada ya kupata taarifa za kuwepo kwa dhehebu hili ambalo linakataza watoto kwenda shule na wagonjwa kutibiwa hospitalini, Serikali ilimkamata kiongozi wake pamoja na waumini kadhaa lakini baadae wakaachiwa huru.

Alieanzisha hili dhebebu anaitwa Medadi Laurent ambae baada ya kukamatwa alihukumiwa kifungo cha miezi miwili jela au faini ya shilingi 30,000/.

Anasema ‘kama ni baridi unapaswa uwe baridi, kama ni moto unapaswa uwe moto, kama nilivyosema toka mwanzo mimi mpaka dakika ya kufa sina mpango wa kusomesha mtoto isipokua kile serikali itachoamua ndio ifanye’

Mmoja wa waumini wa kike wa kanisa hili alisema  kwamba ‘sisi elimu tunayoijua ni elimu ya kumfahamu mtakatifu alie juu maana ndipo kuna uzima lakini katika elimu ya dunia hakuna uzima, maana tunawashuhudia wasomi wengi wakifa hawapati uzima lakini sisi hata tusiposoma elimu ya dunia hii kama tutamtii Mungu au hata kama tutakufa tutakua na uzima wa baadae’

Muumini mwingine wa kiume  nae katika mahojiano na kituo kimojawapo cha radio alisema kwamba‘swala la elimu siafikiani nalo kwa sababu kwanza kwa mujibu wa maandiko matakatifu hatupaswi kujifunza elimu nyingine tofauti na elimu ya kumjua Mungu maana ukisoma Yohana anasema na uzima wa milele ndio huu wakujue wewe Mungu wa pekee na Yesu kristo uliemtuma.

Mkuu wa wilaya ya Kakonko Peter Toyima amesema ‘tumeandika barua kuliandikia lile dhehebu kwamba ni marufuku kuendelea na shughuli hizi kwa sababu kwanza hawajasajiliwa kwa hiyo hamna uhalali wa kuwepo na wakifanya tena mkusanyiko wa namna hiyo lazima tuwakamate na hatua zichukuliwe tena.


Dhehebu la Sabato Matengenezo lilianzishwa January 2014 baada ya kujitenga kutoka katika dhehebu la Waadventista wasabato. 


                         Credits:millardayo.

Comments