KWANINI TUNATAKIWA KWENDA KANISANI....



Kwa mtu aliyeokoka ni lazima kuhudhuria kanisani. Sio tu kwa sababu ni kitu kinachompendeza Mungu, bali pia ni kwa ajili ya kukua na kuimarika kiroho. Kuna sababu nyingi za kiMungu zinazotufanya tuhudhurie ibada kanisani, hapa kuna baadhi ya hizo

1. Ni udhihirisho wa upendo wetu kwa Mungu

Kuhudhuria ibada kanisani ni udhihirisho halisi na unaoonekana wa
upendo wetu kwa Mungu. Ni mahali tunapoweza kumtolea Mungu dhabihu za sifa, shukrani na heshima.

Zaburi 134:2 Inueni mikono yenu katika mahali patakatifu
na mumsifu BWANA .

Tunapaswa kumtolea Mungu muda na nguvu zetu katika kumwabudu na kumsifu maana yeye pekee ndiye anayestahili.

Ufunuo 4:11 Bwana wetu na Mungu wetu, wewe umestahili kupokea utukufu na heshima na uweza, kwa maana ni wewe uliyeviumba vitu vyote, na kwa mapenzi yako vitu vyote viliumbwa na vinapata kuwapo.”

2. Tunaimarika Kiroho

Tunaposikia neno la Mungu likihubiriwa na kufundishwa kanisani imani yetu inakua na roho zetu zinaimarika. Ni muhimu kwa roho zetu kuwa na akiba ya neno la Mungu la kutuwezesha kuvuka pale tunapokutana na changamoto mbali mbali. Ni muhimu kutumia kila nafasi tunayoipata kujivika silaha za Mungu ili tuweze kumshinda adui, na tunapohudhuria kanisani tunapata kulishwa neno la Mungu, kutiwa moyo na kuimarishwa roho zetu. Neno la Mungu ndilo linatuimarisha na kujenga imani yetu.

Warumi 10:17 Basi, chanzo cha imani ni kusikia, na kusikia huja kwa kuhubiri neno la Kristo.

3. Tunapata nafasi ya kuwa katika uwepo wa Mungu

Kuna ahadi ya Mungu kuwa wakutanapo wawili au watatu yeye anakuwa kati kati yao, watu wanaojihudhurisha pamoja kwa ajili ya kumtafuta. Pamoja na kwa Yesu yupo ndani yetu, anadhamini sana mkutaniko wa watu wanaokutanika kwa ajili ya kumuomba, kumsifu, kumuabudu na kumsikiliza. Mahali kama hapo Mungu anashusha uwepo wake, upako na nguvu zake.

Mathayo 18:20 Kwa maana wanapokutana watu wawili au watatu katika jina langu, hapo mimi nipo pamoja nao

Na katika uwepo hu wa Mungu, Roho Mtakatifu anashusha vipawa vyake na karama mbalimbali.

4. Inaleta umoja katika kanisa la Mungu

Tnapokutanika pamoja kwenye ibada tunapata kufahamiana na wapendwa wengine na kuleta umoja miongoni mwa watu tunaomwamini Mungu. Uhusiano mzuri na Mungu unahitaji pia kuwa na uhusiano mzuri na watu wa Mungu. Huwezi kumpenda Mungu na kumchukia ndugu yako.

1 Yohana 2:9-10 Mtu anayesema kwamba anaishi nuruni, naye anamchukia ndugu yake, bado yumo gizani. 10Anayempenda ndugu yake anaishi katika nuru na wala hana kitu cha kumfanya ajikwae

Huwezi kuwa na uhusianao na watu usiowajua wala kukutana nao hivyo kwenda kanisani kunakupa nafasi ya kukutana na kufahamiana na watu wa Mungu.

1 Yohana 1:7 Bali tukiishi nuruni, kama yeye alivyo nuru, tunakuwa na ushirika sisi kwa sisi na damu ya Mwanae Yesu, inatutakasa dhambi zote

5. Ni ishara ya utii kwa Mungu

Kwenda kanisani ni ishara ya kuonyesha utii kwa Mungu na kwa neno lake. Neno la Mungu linatuasa tusiache kukutanika pamoja.

Ebrania 10: 24-25 Na tujishughulishe kutafuta jinsi ya kuhimizana katika kuonyeshana upendo na kutenda mema. Tusiache kukutana pamoja, kama wengine wanavyofanya, bali tutiane moyo, hasa zaidi tunapoona siku ile ikikaribia.

Kukutanika huku kunatupa nafasi ya kuimarishana, kutiana mouo, kuinuana na kufarijiana na wapendwa wengine. Ukifahamu umuhimi wa kenda kanisani nawe ukawa hufanyi hivyo utakuwa unamkosea Mungu.

Yakobo 4:17 Mtu ye yote anayefahamu lililo jema kutenda, lakini asilitende, basi mtu huy
o anatenda dhambi.


MUNGU akubariki ana.
Neema za Kristo.

Comments

Unknown said…
Hallelujah , mungu akubaliki sana mtumishi wa mungu
Kwani somo nizuri sana ukiangalia kizazi cha sasa kimemezwa na utandawazi wa leo, wengi hawapendi kukusanyika kwa pamoja wanakwambia nitaangalia mahubili kwa njia ya TV nk.