MAOMBI YA TOBA


Kutana na Mtu wa Mungu  Nabii Samson  pale katika hema ya Kinabii kwaajili ya kufunguliwa kukombolewa kuwekwa huru kurejeshwa, kwa msaada zaidi piga simu ni Bure 0756 809 209 Mtu wa Mungu,
MAOMBI YA TOBA

Na Mtu wa Mungu Nabii Samson,
Utangulizi:
Tunahitaji msaada wa Mungu kwa kila jambo tunalolifanya katika maisha yetu na  Msaada unapatikana kulingana na Mahusiana yaliyopo baina ya muombaji  na mtoaji, kwa kawaida unalolitaka kwa kwa mtu ili ulipate mahusiano yanatakiwa yawe mazuri,

Maana ya Maombi:
Maana ya maombi ni kusema na Mungu au kuhitaji msaada toka kwa Mungu. Isaya 43:26, Unikumbushe, na tuhojiane; eleza mambo yako, upate kupewa haki yako. Sehemu pekee ya kueleza mambo yako ni kwa Mungu,
Unikumbushe – Mungu anaposema tumkumbushe hana maana kuwa amesahau. Hapana. Ila anataka kuona moyoni umeweka nini. aliwaambia wana wa Israel kuwa “Niliwazungusha makusudi ili nione mioyoni mwenu mna nini.” Ndiyo maana tunatakiwa kuliweka Neno la Bwana mioyoni mwetu. Zab 119:10,

Yeremia 1:12

Tuhojiane – Ni jambo la kumshukuru Mungu anayetupatia nafasi ya kueleza mambo yetu, kero zetu na shida zetu kwake kwa kuhojiana  naye ili tupate kupewa haki zetu.
Haki zetu:
Katika Biblia ziko haki zetu nyingi sana ambazo Mungu wetu ametuahidi. Lakini wengi wetu  hatuzijuwi. Inatubidi kusoma Biblia kwa bidii ili Neno lake Kristo likae kwa wingi ndani    
 Biblia ina mistari 31,173. Hebu jipime uone, wewe unaijua mingapi? Dan 9:1 – Daniel katika wakati wake alisoma kitabu alichokuwa ameandika nabii Yeremia akakuta muda ambao walitakiwa watoke utumwani umepita na bado wako utumwani. Walikuwa huko kwa kutokujua. Kwa hiyo kusoma Neno la Mungu kuna faida nyingi, muhimu ikiwa ni kufahamu ukweli wa mambo.


Sababu za Kuomba:
Ziko sababu mbali mbali za kusema na Mungu. Na kama tulivyoona hapo juu kuomba ni kusema na Mungu. Hii ina maana unapotaka kusema na Mungu ni vizuri ujuwe unataka kusema naye kuhusu nini.
Tuchukue mfano: Unapoenda ofisi ya mtu ye yote, huwezi kuingia ofisini hapo wakati hujuwi unakwenda kwa sababu gani. Ndiyo maana ukiingia unaambia ‘karibu, tukusaidie nini?’.
Ni kawaida kwamba jibu la swali hilo huwa lipo. Lakini watu wengi humwendea Mungu wakati hawajuwi sababu ya kumwendea. Pia, kwa kuwa Mungu ni baba yetu hatutakiwi kumwendea wakati wa shida tu, yaani shida ikiisha, basi. Hapana.
 kwenye ofisi za watu huenda wakati tunashida tu, lakini kwa Mungu wetu tunatakiwa kwenda wakati wote. Hii huonyesha ushirika,Mahusiano yaliyopo kati yetu na Yeye.
Sababu za kusema na Mungu, yaani sababu za maombi ni nyingi sana. Yako mambo mengi sana ambayo tunatakiwa kuyabeba wakati wa maombi. Ni vigumu kuyataja yote lakini tutaangalia baadhi, ambayo yatafanyika kama kielelezo. Lakini kwanza tuangalie maandiko,:
Kolosai 4:2-4 inasema hivi, Dumuni katika kuomba huku na shukurani, mkituombea na sisi pia, kwamba Mungu atufugulie mlango kwa lile neno lake, tunene siri ya Kristo, ambayo kwa ajili yake nimefungwa, ili niidhihirishe, kama inipasavyo kunena.

Hayo mambo mazito hapo juu ni maagizo ambayo Paulo aliwaandikia Wakolosai. Napenda tujifunze kutokana na hayo maombi. Mara nyingi watu wa Mungu husema tuko kwenye maombi, hata wakati mwingine tunakosea maana si jambo la kutangaza. Maandiko hayo yanatupatia mwelekeo wa sababu za kutupeleka mbele za Mungu kwa maombi. Pamoja na sababu hizo chache, hapo, pia tunaambiwa kuwa tunatakiwa kudumu katika kuomba, kudumu, ni kutokata tamaa, kutokuchoka, kutokupunguza, kutoacha,

Katika maneno hayo MtumePaulo aliwaomba Wakolosai wawaombee pia. Unajua tunafanya makosa makubwa kama hatutaombea viongozi wetu.
Tutawaombea nini?
Mungu awafungulie milango, Mungu awape usemi, Mungu awawezeshe katika kunena na kutenda pia. Je, hayo ndiyo tutaombea kila siku? Hapana. Ni pamoja na hayo. Tutaona kwa kirefu baadhi ya mambo mengine ambayo tunapaswa kuyaombea, maana kama ni hayo tu basi nadhani ni muda mfupi tu nasi tutakuwa tumemaliza.
Tuangalie tena 1Yohana 5:14-15 Na huu ndio ujasiri tulionao kwake, ya kuwa, tukiomba kitu sawa sawa na mapenzi yake, atusikia. Na kama tukijua kwamba atusikia, tuombacho chote, twajua kwamba tunazo zile haja tulizomwomba.
Ujasiri wetu unaotupeleka kwenye maombi ndio huo. Mtu jasiri haogopi, hana mashaka hata kidogo. Kwa hiyo tunapaswa kuwa majasiri kwa Mungu wetu.
Mahali pengine Biblia inasema mwenye haki ni jasiri kama simba. Uajua simba ni mnyama wa ajabu sana. Si mwoga. Hafanani na fisi. Ukiwa karibu na fisi ukamshtua kile anafanya ni kukuharishia: ishara ya uoga. Lakini ukimshtua simba, yeye hakimbii. Ni kama ndiyo unamwita kuwa aje mkutane mpambane,  yesu Anaitwa Simba wa Yuda,
Maandiko yanasema pia tuombe sawa sawa na mapenzi ya Mungu. Ni vizuri tufahamu  mapenzi ya  Mungu. Tutayapata wapi? Mapenzi ya Mungu tutayajuaje? Mapenzi ya Mungu yako kwenye Neno lake. Ebu tuangalie maandiko machache yanayohusu mapenzi ya Mungu. Na haya tunaweza kuyatumia kama muongozo wa maombi yetu wakati tunapoomba.
1Tim 2:1-4, Basi, kabla ya mambo yote, nataka dua, na sala, na maombezi, na shukurani zifanyike kwa ajili ya watu wote; kwa ajili ya wafalme na wote wenye mamlaka, tuishi maisha ya utulivu na amani, katika utauwa wote na ustahivu. Hili ni zuri, nalo lakubalika mbele za Mungu mwokozi wetu, ambaye hutaka watu wote waokolewe, na kupata kujua yaliyo kweli.

Hapo tunaona wajibu wetu. Tunatakiwa kuwaombea watawala wetu, wafalme wetu, ili tuishi kwa amani. Vinginevyo amani hutoweka. Amani inatakiwa kuendelea kuwepo kwa ajili ya maombi ya watakatifu. Pia anasema tuombee watu wote. Mpendwa ukweli Mungu anapenda watu wote, na anapenda wote waokolewe.

 Tunachotakiwa kuendelea kufanya ni kuwaombea. Anzia na wale unaowafahamu, ambao bado hawajaokoka. Waombee, ukijua kuwa na wewe kuna mtu alikuombea ukapata wokovu. Kumbuka pengine ulivyokuwa mbishi, hukutaka hata kusikia habari za wokovu. Pengine uliwafukuza waliokushuhudia habari za wokovu. Je, waweza kujua kwa nini uliokoka? Jibu: uliombewa na mtu.
Sasa zifuatazo ni baadhi ya
Sababu za maombi,
1. Isaya 62:7, Wala msimwache akae kiimya, mpaka atakapofanya imara Yerusalem, na kuufanya kuwa sifa duniani.
Maandiko yanasema tusimwache akae kimya. Ina maana tuendelee kuomba. Hivyo hayo ni mapenzi ya Mungu kwetu.
2. Zaburi 122:6, Utakieni Yerusalem(ISRAEL) amani, na wafanikiwe wakupendao.
Mpendwa, Baraka zingine ni za kuchukua tu, wala hazina gharama sana. Kutamka tu kwamba tunaitakia amani, tunaiombea amani Yerusalem, hizo ni Baraka za mafanikio; andiko linasema wafanikiwe wakupendao.
Kuna watu hawataki kusikia Israel.
 Wengine husema wataifuta katika ramani ya dunia hii! Huwa nacheka kwa kuwa kwa kusema hivyo huwa wanasema:

 Watamfuta Mungu kutoka katika uso wa dunia.  Ukweli huwa hawajuwi wanasema nini. Mungu alimwambia Ibrahimu kuwa yeye atakaye kulaani nitamlaani, yeye atakayekubariki nitambariki. Ebu tujipatanishe na wateule wa Mungu kama tunataka kupona. Pia Mungu alisema ‘mpaka mtakapogundua dunia hii inakaa kwenye nini’,

hapo ndipo atakapoiacha Israel wasiwe watu wake.  Yeremia 31:35-37, Bwana anasema hivi, awapaye watu jua, ili kuwa nuru wakati wa mchana, na amri za mwezi na nyota, ili kuwa nuru wakati wa usiku, aichafuaye bahari, hata mawimbi yake yakavuma, Bwana wa majeshi, ndilo jina lake. Amri hizi zikiondoka, zisiwe mbele zangu, asema Bwana, ndipo wazao wa Israel nao wataacha kuwa Taifa mbele zangu milele. Bwana asema hivi, kama mbingu zikiweza kupimwa, na misingi ya dunia ikiweza kugunduliwa huko chini, ndipo wazao wa Israel pia nitawatupilia mbali, kwa ajili ya hayo yote waliyoyatenda, asema Bwana.

Mpendwa, mtu asikudanganye, ukasema vibaya juu ya Israel. Hii pia ni sawa na kusema vibaya juu ya mcha Mungu ye yote. Wala usithubutu kufungua kinywa kumnena mabaya. Nikukumbushe kidogo habari ya wale waliofungua vinywa kumnena vibaya Musa, walikuwa Miriamu na Haruni. Nakuambia Mungu aliingilia kati mwenyewe, akawaadhibu mara moja. Miriam akapigwa na ukoma. Kwa hiyo tujiepushe kulisema vibaya Taifa hilo la Mungu. Ni lake. Sikia Mungu anavyosema: ‘kama mtu atajua dunia imekaa juu ya nini ndipo Taifa hilo liaacha kuwa Taifa lake.’
3. Luka 6:28, Wabarikini wale ambao wawalaani ninyi, waombeeni wale ambao wawaonea ninyi.

Mpendwa, safari ya mbinguni imeelekezwa vizuri namna ya kuisafiri. Hiyo ni njia moja wapo ya kuelekea huko: Kuwaombea wale wanaowaonea, kuwabariki wale wanaowalaani! Fanya hivyo na Mungu atakubariki.
4. Luka 22:40, Alipofika mahali pale aliwaambia, ombeni kwamba msiingie majaribuni.
Bwana akawaambia kuwa waombe ili wasiingie majaribuni. Hakusema ‘ombeni kwamba msijaribiwe’. Aliwaambia waombe kuwa ‘wasiingie’. Maana yake nini? Unaweza kufika nyumbani kwa mtu, kwa nje, wala usiingie ndani. Waweza kufika Ubungo, ambapo tunajua ni Dar es salaam. Lakini ukifika Ubungo, bado utakuwa hukuingia mjini. Ebu tuombe kuwa tusiingie katika majaribu, mpaka yakatumeza na kutushinda.

5. 2Kor 13:7, Nasi twamwomba Mungu, msifanye lolote lililobaya, si kwamba sisi tuonekane tumekubaliwa, lakini ninyi mfanye lililojema, tujapokuwa sisi tu kama waliokataliwa.
Omba kuwa usifanye lolote lililobaya, yaani usifanye dhambi. Pia ombea watu uwajuao na usiowajua wasifanye dhambi. Hiyo itawasaidia wengine kujilinda na itafanya watu wengine wawe na breki katika kutenda maovu.
Omba watu wafanye yaliyo mema, ni pamoja na wewe mwenyewe, omba kuwa ufanye mema.
6. Filipi 1:9, Na hii ndio dua yangu, kwamba pendo lenu lizidi kuwa jingi sana, katika hekima na ufahamu wote.
Omba kuwa upendo wako uzidi kwa watu, omba kuwa upendo wa watu kwa wenzao uzidi kuwa mwingi sana. Unajua mpendwa Neno linasema siku za mwisho upendo wa wengi utapoa:
utapoa wao kwa wao, utapoa kwa Mungu. Sasa omba kuwa watu wapendane. Omba kuwa watu wampende Mungu wao aliye waumba. Wasimpende adui ambaye hakuwaumba.
7. 1Thes 5:23, Mungu wa amani mwenyewe awatakase kabisa; nanyi nafsi zenu na roho zenu na miili yenu mhifadhiwe mwe kamili, bila lawama, wakati wa kuja kwake Bwana wetu Yesu Kristo.
Ndugu mpendwa, haya ni maombi ya muhimu sana. Kama Biblia isemavyo kuwa Yesu atakuja kama mwivi. Ni wazi kabisa tunafahamu kuwa mwizi hatoi taarifa ya kuwa anakuja kuiba, labda jambazi. Jambazi anaweza kutoa taarifa maana huwa anakuja akiwa tayari kwa lolote lile. Bwana alisema atakuja kama mwivi. Kwa hiyo tunatakiwa kuomba kuwa wakati wa kuja kwake, tusiwe na kasoro katika miili yetu, nafsi  zetu na roho zetu.
8. Luka 11:13, Basi, ikiwa ninyi mlio waovu mnajua kuwapa watoto wenu vipawa vilivyo vyema, je! Baba aliye mbinguni hatazidi sana kuwapa Roho mtakatifu hao wamwombao?
Wapo watu wengi ambao hukaa muda mrefu kabla hawajajazwa na Roho Mtakatifu, mpaka wengine wanakata tama na kudhani Roho mtakatifu ni wa watu maalumu. Hapa. Wala usikate tamaa, endelea kuomba huku ukiamini kuwa Mugu atakupatia Roho mtakatifu. Pia inawezekana unanena kwa lugha, ambayo wengi wamedhani kila anayenena kwa lugha ana Roho wa Mungu. Mpendwa, ebu kagua kama kweli ni Roho wa Mungu. Maana hata waganga wa kienyeji wananena kwa lugha.

Tofauti iliyopo ni kwamba hawana matunda ya Roho mtakatifu. Usiridhike na lugha tu isiyo na matunda, maana imeandikwa:Mtawatambua kwa matunda yao. Math 7:16
9. 1Kor 14:13, Kwa sababu hiyo yeye anenaye kwa lugha na aombe apewe kufasiri.
Ziko haki zetu nyingi katika Biblia ambazo hatujazifahamu. Na kama hatuzifahamu, basi, hatuwezi kuziomba. Lakini hapa tunaambiwa kuwa mtu anayenena kwa lugha aombe pia apewe kufasiri. Fanya hivyo na Mungu atakujalia kufasiri.
10. Zab 37:4, Nawe utajifurahisha kwa BWANA, Naye atakupa haja za moyo wako.
Wakati mwingine huwa tunayo yale tunayoyawaza mioyoni mwetu, bila mtu mwingine kujua. Tunapaswa kumuomba Bwana atupatie haja ya mioyo yetu. Ni kweli kuwa Mungu anajua yote. Lakini anapenda kusikia tukimwambia. Yesu akamuuliza Baltmayo kipofu kwamba“wataka nikufanyie nini?” Akasema nipewe kuona, akapewa kuona. Marko 10:51
11. Zab 71:9, Usinitupe wakati wa uzee, Nguvu zangu zipungukapo 

usiniache.
Mpendwa, hili ni ombi muhimu sana katika maisha yetu. Unajua wako watu wanaishi kama Wafalme wa zamani. Wafalme wa zamani waliishije? Walikuwa wanasalimiwa ati ‘Uishi milele ee mfalme’. Hawakuwa wanajiandaa kuwa kwa vyovyote wataondoka katika utawala. Hawakujua kabisa kuwa siku moja nguvu zao zitakwisha.

Natumaini unakumbuka jinsi Herode alipopata taarifa kuwa mfalme mwingine amezaliwa, yeye alipanga namna ya kumwangamiza. Mfalme aliyezaliwa akiwa kitoto kichanga ingemchukua miaka mingi kufikia umri wa kutawala kama mfalme. Na inawezekana kabisa hadi afikie umri huo wa kutawala, yeye Herode tayari angekuwa ameshakufa. Lakini kwa sababu ya kufikiri ataishi milele kweli, kama ambavyo alikuwa akisalimiwa, yeye akaona cha kufanya ni kumuangamiza mfalme-mtoto huyo kwa kuwa yeye Herode ataendelea kutawala milele. Ni ajabu kabisa!
Hebu tuone maombi hayo ya Daudi katika Zaburi 17:9 yalivyokuja kufanya kazi. Tunapata habari hiyo katika 2Sam 21: 15-17, Basi kulikuwa na vita tena kati ya Wafilisti na Israel; Daudi akashuka mpaka Gobu, na watumishi wake pamoja naye, akapigana na Wafilisti, naye Daudi akaishiwa na nguvu. Naye Ishi-benobu, aliyekuwa mmojawapo wa Warefai, ambaye uzito wa mkuki wake ulikuwa shekeli mia tatu za shaba kwa uzani, naye amejifungia upanga mpya, alijaribu kumwua Daudi. Lakini Abishai, mwana wa Seruya, akamsaidia, akampiga Mfilisti akamwua. Ndipo watu wa Daudi wakamwapia, wakasema, Wewe hutatoka tena pamoja nasi kwenda vitani, usije ukaizima taa ya Israel.

Maombi aliyoyaomba Daudi mtumishi wa Mungu kuwa atakapokuwa mzee, yaani nguvu zake zitakapokwisha asiachwe, siku ilifika kweli nguvu zake zikaisha. Akakaa chini. Ndugu yangu, mwanaume Daudi alishindwa hata kukimbia, achilia mbali kupingana. Huyu ni Daudi aliyeua dubu, aliyeua simba, Daudi aliyeua Goliathi!
Ndugu yangu siku zinakuja, wengine tayari zimewafikia, hawawezi tena kuomba kama walivyofanya zamani. Hawawezi tena kuhubiri kama walivyofanya zamani. Nguvu zao zimekwisha. Hata wanapokabiliana na Ishi-benobu wao, hawawezi tena.
Japo Ish-benobu alikuwa ana upanga mpya, maana yake mbinu mpya tofauti na ile aliyoizoea enzi zake, lakini kifo kilikuwa kinamkabili. Daudi aliwahi kuomba zamani na sasa faili lake likafunguliwa, likakutwa kuna ombi hilo ambalo halikuwa limejibiwa hadi wakati huo.
Na ndipo ilibidi jibu litumwe. Ndugu yangu, nikipiga picha jinsi Daudi alivyokuwa amekaa chini, anamwangalia Ishi-benobu mbele yake, bila shaka alikuwa anamwambia ‘siku zako zimekwisha…..Wewe ni halali yangu’. Kumbuka vijana wote walikuwa wamekimbia hivyo Daudi alikuwa amebaki peke yake.
Yawezekana hapo ulipo uko peke yako, huna mtu wa kulia kwako wala kushoto kwako. Ni vita mbaya sana hiyo. Huna hata mtu wa kumwambia jambo, kuwa nikifa watazame kitu muhimu nimekiweka mahali. Kumbuka wakati huo Daudi alikuwa na ramani ya Hekalu, wala asingeweza kumpatia Ishi-benobu maana haikuwa inamhusu.

Pengine sasa Ishi-benobu yuko mbele yako, unachokiona ni upanga mpya! Sikia Neno toka kwa Bwana Mungu wako, hatayaabisha mafuta aliyokupaka, kamwe. Pamoja na maombi yako kuwa asikuache, lakini nasema Mungu alikupaka mafuta,
Amini tu Mungu  hatakuaibisha. Hataaibisha mafuta aliyokupaka. Abishai hayuko mbali. Kaza macho yako juu, kuna jambo litatokea. Kabla Ishi-benobu hajakufikia, Abishai atakutokea. Bwana ameshasema na Abishai. Namuona katika ulimwengu wa roho anakuja mbio. Ole wa Ishi-benobu, mauti imemkaribia sana. Usiogope. Abishai huyo, anakuja. Hutaaibika. Vita ni vya Bwana! 2Nyakati 20:15

Comments