![]() |
Mchungaji Christopher Mtikila |
Mwenyekiti wa Tume ya
Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba amewasilisha Rasimu ya Pili ya
Mabadiliko ya Katiba katika Bunge la Katiba Machi 18, mwaka huu.
Katika hotuba yake, Jaji Warioba alitumia saa matatu, kueleza wazi kuwa
kutokana na maoni ya wananchi na taarifa za uchunguzi na utafiti,
muundo wa Serikali tatu ndiyo mwafaka kwa sasa.
Jaji Warioba katika hutuba yake, alianisha
malalamiko ya pande zote za Muungano, ambayo kwa zaidi ya miaka 30
yameshindwa kupatiwa ufumbuzi katika Muundo wa Serikali mbili.
Akasema kutopatiwa ufumbuzi kwa malalamiko hayo,
sasa kumefanya yafikie hatua ya upande wa Zanzibar kuvunja Katiba ya
Muungano kwa kuunda Katiba yake yenyewe. Ilielezwa kwamba Zanzibar
ilifanya mabadiliko katika Katiba yake ya mwaka 1984 ambayo sasa
inajiita nchi yenye Rais mwenye mamlaka kamili ya kuigawa ardhi ya
visiwa hivyo katika maeneo ya utawala.
Jaji Warioba akasema kutokana na mabadiliko hayo
ya Katiba sasa Muungano, umetoka kuwa wa nchi moja Serikali mbili,
kwenda muungano wa nchi mbili na Serikali mbili. Hivyo ili kuimarisha
Muungano kwa mazingira ya sasa tume yake ikapendekeza mfumo wa Serikali
tatu, ambazo ni Serikali ya Tanganyika, Serikali ya Zanzibar na
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mchungaji Christopher Mtikila ni mmoja ya
wanasiasa ambao kwa miaka zaidi ya 20 sasa, wamekuwa wakililia kurejea
Serikali ya Tanganyika. Katika mahojiano na gazeti hili Mtikila akaeleza
kwamba “Serikali ya Tanganyika sasa haiepukiki.”
Swali. Wewe ni Mjumbe wa Bunge la Katiba
nini maoni yako baada ya Jaji Joseph Warioba kuwasilisha Rasimu ya
Pili ya Katiba Mpya kwenye Bunge la Katiba?
Jibu: Jaji Warioba na tume yake
wamefanya kazi nzuri na wameunga mkono harakati zangu za kuidai
Tanganyika iliyo huru ambayo ilikuwa inafichwa na watu wachache.
Swali. Katika taarifa ya Jaji Warioba
amebainisha changamoto nyingi ndani ya Serikali mbili je unadhani mfumo
wa Serikali tatu sasa ni mwafaka?
Jibu: Muungano ni uhusiano ya
hiari na lazima usukumwe na masilahi ya kila upande, hivyo kwa sasa
kuendelea na Muungano unaopingwa kila upande ni sawa na utumwa.
Swali: Baadhi ya Watanzania wamekuwa
wakipinga Mfumo wa Serikali tatu ambao, umependekezwa na Tume ya
Mabadiliko ya Katiba. Je, wewe maoni yako ni nini?
Jibu: wanaopinga mfumo huu wana
matatizo, kwani hakuna taifa la Tanzania ambalo lilikwenda kudai uhuru
Umoja wa Mataifa bali waliodai uhuru ni Watanganyika hivyo huwezi kuiua
Tanganyika.
Swali: Baadhi ya wanasiasa wamekuwa
wakipinga taarifa ya Tume ya Jaji Warioba kuwa watu waliohojiwa na kutoa
maoni ya kutaka muundo wa Serikali tatu hawazidi 17,000 ambao
hawafikii hata asilimia tano ya Watanzania wote, nini maoni yako?
Jibu: Mimi ninaamini Maombi ya Serikali tatu ni
ya Watanzania wengi hao CCM ambao wanadai, maoni ya Tume ya Warioba
ambaye ni CCM mwenzao hawafiki hata milioni 2.5 hata ikipigwa kura ya
katiba hatawashinda.
Swali: Kutokana na utata juu ya uhalali wa
maoni ya wachache kudai Tanganyika kuna hoja ya sasa kuitishwa kura ya
maoni ya Watanzania wote juu ya muundo wa Muungano nini maoni yako?
JIbu: Hakuna sababu ya kura za
maoni kwani suala la kudai utaifa halina wingi au uchache ni muhimu sasa
kukubaliana na Muundo wa Serikali tatu, kwani baadaye unaweza kudaiwa
kwa njia ya vurugu.
Swali: kwa mujibu wa maelezo ya Jaji
Warioba tayari Wazanzibari wamevunja Katiba ya Muungano kwa kuifanya
Zanzibar nchi. Je, nini maoni yako?
Jibu: Wazanzibari wanajua haki
zao ndiyo sababu wamejivua hilo kongo la Muungano na ninaamini hata
Watanganyika ambao walikuwa usingizini, sasa wataamka na kudai
Tanganyika yao.
Swali: Kwa hali ilivyo sasa bado ni
vigumu kutabiri kama mfumo wa Serikali tatu utapita. Je, ukiendelea
kukwama unadhani kuna njia nyingine za kudai?
Jibu: Binafsi nimeshasema
tukishindwa kupata sasa Serikali ya Tanganyika mimi nitakwenda
mahakamani tena Mahakama za kimataifa. Najua huku ndiko Watanganyika
watapata haki na tayari nina mawakili wanasubiri tukwame.
Swali: Baada ya Rais Kikwete kukuteua kuwa
Mjumbe wa Bunge la Katiba, ulitishia kutohudhuria Bunge hili imekuwaje
sasa unashiriki?
Jibu: Washauri wangu ambao ni
wanasheria ndiyo wamenitaka kushiriki ili tukishindwa kuipata Tanganyika
katika Bunge hili ndiyo tuendelee na kesi.
Swali: Nini maoni yako ya jumla kuhusiana na mchakato wa Katiba ambao unaendelea sasa katika Bunge hili?
Jibu: Nina imani watu waliokuwa hawajui matatizo na kero za Muungano wamejua na sasa Tanganyika itapata uhuru wake tena.
Chanzo: Mwananchi
Chanzo: Mwananchi
Comments