MFALME



Yesu hakuja kwa namna ya "kutisha watu" ila alikuja kama "Mwana-Kondoo". Japo alikuwa Mfalme wa wafalme, hakuja juu ya farasi wa kivita na misafara ya magari ya deraya, alikuja juu ya mwana-punda. Kila alipozungumza alimtukuza Baba na wala sio yeye mwenyewe, japo alikuwepo tangu mwanzo na hakuna kilichofanyika pasipo yeye!

Alipojua "amepewa mamalaka Mbinguni na duniani, na kwamba kila kitu kiko chini yake, alitoka mezani (chakulani), akavua vazi lake, akajifunga kitambaa, na kuwanawisha wanafunzi wake miguu, kisha kuwafuta na nguo/kitambaa alichojifunga"! Ukiona mtumishi anakuja kwa kutisha-tisha, na hana kabisa hizi sifa za Mwana-kondoo, wala huoni utukufu wa Mungu ila wa wanadamu au majigambo, jua kwamba msingi wa huduma yetu ni kumtukuza Kristo na ukuu wetu unapimwa na UPENDO wala sio nguvu katika unabii na miujiza. Jinsi tunavyozidi kuwa "watumwa" na chini sana, ndivyo tunavyokuwa wakuu katika ufalme wa Mungu. Kipomo cha ukuu ni udogo/kujishusha kwa mtu.

Hata hivyo nakubali wapo watakaokuja kwa usahihi ila pia na miujiza ikiambatana nao. Kwa hili kundi dogo la watumishi, miujiza sio kitu cha kutafuta wala kuhangaika, ila kutenda mapenzi ya Mungu. Hebu kumbuka, Yesu alipotenda muujiza alitaka kuficha watu wasijue, alijitahidi kukataza watu wasisema. Sehemu nyingine alimkamata kipofu mkono akamtoa nje ya mji kwenda kumponya huko, na kisha akamwambia asirudi mjini (Marko 8:22-26). Hataki watu wajue hii kitu. Muujiza wa Mungu sio jambo la kujigamba nalo, ndio maana wanafunzi waliambiwa "msifurahi kwa kuwa mapepo yanawatii, bali furahini kwa sababu majia yenu yameandikwa Mbinguni"

Tuko katika kipindi cha hatari, inakuwa ngumu kujua ni kipi halisi na kisicho halisi. "Wengi sana walio wa kwanza watakuwa wa mwisho na walio wa mwisho watakuwa wa kwanza". Usihofu juu ya wachanga, Bwana anajua walio wake na wala hakuna "awezaye kupokonya kutoka mikononi mwake", washike tu kwa uaminifu kile KIDOGO walicho nacho hadi Bwana arudipo...watauona uso wake
na watakuwa pamoja naye katika raha ya milele.

Frank Philip

Comments