MIAKA 30 YA UASKOFU YA KARDINALI PENGO


Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo akipokea zawadi kutoka kwa waumini wa sehemu mbalimbali wakati wa misa maalumu ya miaka 30 ya uaskofu iliyofanyika Kituo cha Msimbazi jijini Dar es Salaam jana. Picha na Silvan Kiwale.

Dar es Salaam. Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo ameadhimisha miaka 30 ya uaskofu, 43 ya upadri na miaka 16 ya ukardinali.

Kardinali Pengo alitoa shukrani wakati wa misa maalumu ya maadhimisho iliyofanyika kwenye Kanisa la Msimbazi Dar es Salaam, alisema ushirikiano alioupata sambamba na amani iliyopo, yote ni matunda ya Mwenyezi Mungu.

“Niliitwa nami nikaitikia, kwani nilipokuwa Jimbo la Nachingwea Lindi, nilipoambiwa nakwenda Dar es Salaam nilijiuliza sana, sauti ya mtu wa Nachingwea itawezaje kutoka kwa watu wa Dar es Salaam, leo (jana) naadhimisha miaka 30 kwa kuwa ushirikiano mlionipa ndiyo umenifikisha hapa,” alisema.

Aliongeza: “Kipindi nakuja Dar es Salaam, kulikuwa na parokia 20, lakini leo kuna parokia 79, ndoto yangu kabla Mungu hajanichukua nataka niache parokia 100 na hiyo itawezekana kwa ushirikiano wenu.”

Katika misa hiyo, Balozi wa Papa nchini, Askofu Mkuu Francisco Montecillo Padilla, maaskofu, mapadri, watawa, mashemasi, mafrateli na waumini mbalimbali walijitokeza kuungana na Kardinali Pengo ambaye licha ya kuadhimisha miaka 30 ya uaskofu pia anaadhimisha miaka 43 ya upadri na 16 ya ukardinali.

Hata hivyo, hali ya afya ya Kardinali Pengo ilielezwa kutokuwa nzuri na kutotakiwa kusafiri kwa umbali mrefu kwa kutumia barabara.

Hali kadhalika jana hakuweza kuingia na kutoka madhabahuni kwa maandano na mapadri na maaskofu kwa pamoja. Aliingia na kutoka kwa kutumia mlango wa mbele.

Awali katika mahubiri, Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo la Morogoro, Telesphory Mkude alisema Juni 3 mwaka huu, kutakuwa na mkutano jimboni humo na wamemwomba Kardinali Pengo kuhudhuria.

“Wameniomba nije kukuomba uhudhurie katika mkutano utakaofanyika Juni 3, mwaka huu. Najua afya yako hairuhusu kutembea umbali mrefu kwa kutumia barabara ngumu, tutaangalia uwezekano wa kutumia ndege ili uweze kuwapo,” alisema Askofu Mkude.

Naye Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Tarcisius Ngalalekumtwa alimshukuru Kardinali Pengo kwa jitihada zake za kudumisha amani na usawa nje na ndani ya jimbo hilo.

Askofu Ngalalekumtwa, ambaye pia ni Askofu wa Jimbo Katoliki la Iringa, aliwataka waumini wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam kutoa ushirikiano kwa Kardinali Pengo kama ambavyo wamekuwa wakifanya mara zote.

Pengo ni Kardinali wa pili kutoka Tanzania, aliyeteuliwa baada ya kifo cha Kardinali Laurean Rugambwa mwaka 1997.

                                                                    Chanzo Mwananchi.

Comments