NILINUSURIKA KUCHUKULIWA MSUKULE NA KAKA YANGU AMBAYE NI TAJIRI SANA

Mchungaji kiongozi wa kanisa la Ufufuo na Uzima Morogoro Godson Zacharia akiwa na Victoria tayari kutoa ushuhuda wake.
Utangulizi: Victoria Mwankenja ni muuguzi. Alishawahi kufa kipindi cha nyuma. Kimwili alikuwa anaonekana, lakini kiroho taratibu zote za mazishi zilikuwa tayari zilishafanyika.

Aliwahi kupata magonjwa ya kutatanisha, ukiwemo (hypertension) yaani BP kuwa juu. Aliambiwa aende hospitali kubwa zaidi DSM ambapo alifanyiwa vipimo vyote. Pale DSM alipelekwa pia kwa Hospitali ya Tiba Mbadala, ambapo alilipa shs. 50,000 na kuambiwa moyo wake ni mkubwa ndiyo sababu kubwa. Alikuwa akivimba mwili mzima kana kwamba ni mnene wakati uzito wake ulikuwa kilo 55 tu. Gharama zote za Tiba Mbadala alipaswa kulipa Sh. 1,700,000. Alilipa sh. 200,000 na kupewa dawa aina tatu.

Victoria Mwankenja ana Wifi yake huko DSM, ambaye alimsaidia kuijua Ufufuo na Uzima. Siku moja ya Alhamisi alifikishwa kanisani, na alipoulizwa shida yake, VICTORIA MWANKENJA alijibu “Mimi nasikia kufa kufa tu”. Aliombewa, na Wakati wa yale maombi alikuwa anaona kwamba yupo tayari kaburini, pembeni mwa kaburi la dada na ndugu zake ambao waliwahi kufa vifo vya kutatanisha. Mle kaburini alikuwa anajiona akifanya kazi ya kuita magari, na kila anapoyaita yanaaenda kwa kaka yake, ambaye ni tajiri mkubwa sana mwenye magari mengi. Kumbe kaka mtu alikuwa ndiye mchukuaji. Ushindani kati ya pande zote mbili uliendelea wakati wa Maombi haya. Wakati Upande wa Kanisa walikuwa wakimwita “KWA JINA LA YESU NJOO, NJOO” lakini upande wa pili wakawa wanamzuia. Hawa wazuiaji walikuwa wanamwambia ‘Wewe unataka kaka yako afilisike. Baki huku huku, magari mengine yatakuwa ya kwako.’

Siku iliyofuata ilikuwa ni Ijumaa, Mchungaji akamwabia kuwa leo utaota ndoto usiku. Ilipofika usiku wahiyo siku, kweli Victoria Mwankenja aliota ndoto akiwa nyumbani kwao Mbeya, akawaona wageni wametokea Kenya, Nigeria na Tanzania wamekuja kula nyama. Miongoni mwa watu wale, alikuwemo mama yake wa kambo, ambaye aliwaambia hawa wageni kuwa “taratibu za kula nyama leo zimevurugika kwani yule mtu wa kuliwa nyama zamu ya leo ametoroka”. Basi wakawa wanamlaumu huyu mama kwamba alifanya uzembe hata kuruhusu hiyo nyama ikatoroka. Aliamka mara moja akaanza kuomba, ingawa alikuwa mchanga kiroho. Wifi yake naye alipomsikia kuwa anaomba, akaungana naye kuomba. Wifi alimwambia ameona majina ya watu wanaopaswa kufa katika ukoo wake. Waliomba kwa ajili ya kufuta hayo majina.

Baadaye, kaka na ndugu zake walimpeleka Hospitali ya TMJ kucheki vipimo vyote, na majibu yakaonesha hana tatizo lolote. Ilibidi madaktari waulizane wao kwa wao “Mbona huyu mtu vipimo vyake vinatofautiana na vipimo vya Hospitali ya Morogoro vyenye kuonesha ana moyo mkubwa? Mbona huyu mtu vipimo vyake havifanani na vya mwanzo?” Waliitisha vikao vya dharura, wakakaa jopo la madaktari, wakamwandikia dawa nyingi tu. Kaka yake kwa kutumia nafasi yake kwenye Bima ya Afya alilazimisha madaktari wamwandikie dawa nyingi tu akiwaambia “Mtu huyu ni mgonjwa!!” Jumapili kanisani lilikuwepo somo la “KILA MTU ANA MLIMA WAKE ”. Victoria Mwankenja wakati wa Maombi ya siku hii aliomba kwa habari ya ndugu zake kwa kuwaita “NJOO kwa JINA LA YESU”. Saa tisa alipokea simu kwamba yupo ndugu yake aliyekuwa amepotea huko Mbeya siku chache zilizopita, na sasa amepatikana.

Yeye na wifi waliendelea na Maombi ya kurudisha mishale kwa maadui zao. Baadaye, Victoria Mwankenja alipokea Simu ya pili muda wa saa moja jioni, kutoka kwa yule kaka aliyempeleka TMJ hospital, kuwa wapo wadogo zake wawili walikuwa kwenye pikipiki wamepata ajali mmoja tayari kafa mwingine mahtuti. Baada ya saa moja hivi akapigiwa tena simu kwamba wote wamefariki dunia. Msiba wa vijana hawa uliibua mambo mengi, kwani walizikwa haraka haraka, wachawi wakawa wanalaumiana wao kwa wao, kuwa huu msiba haukuwa wa vijana hawa.

Wiki hii Victoria Mwankenja alifanya Maombi ya Mkesha wa Ijumaa (21/03/2014) na baadaye akapata taarifa ya kifo cha baba yake mdogo, ambaye alikuwa miongoni mwa timu ile ya wala nyama na kuchukua watu msukuleni katika ukoo wake. Leo hii Jumapili (23/03/2014) wakati wa kutoa huu Ushuhuda, Victoria Mwankenja ana msiba wa baba mdogo wake, lakini sifa na utukufu ni kwa Bwana Yesu aliyegeuza mashimo waliyomchimbia Victoria Mwankenja kuwa mashimo ya maadui zake, na wote wamedumbukia humo wao wenyewe. Victoria Mwankenja anawasihi watu wasifanye mizaha na Maombi ya Ufufuo na Uzima, kwani yanafanya kazi zenye kuonekana kwa macho.

Mwisho wa Ushuhuda

==Na Mwandishi Wetu==

== Information Ministry (Ufufuo Na Uzima - Morogoro)== Via Gospel kitaa

Comments