NJIA ZA MWANADAMU ZI MBELE ZA MACHO YA BWANA


Ndugu zangu shalom.
Namshukuru Mungu kwa uzima wa siku ya leo.
Labda kabla sijaenda mbali naomba nitoe ufafanuzi kuhusu neno shalom. Watu wanatamani kujua nini maana ya neno hili maana nimekuwa nikilitumia karibu kila siku. Kwa hiyo watu mlokuwa mkitaka kujua maana yake ngoja nitoe ufafanuzi.
Shalom ni neno la kiebrania lenye maana ya 'amani'. Na neno hili wakati mwingine  kipekee kabisa limekuwa likitumika kama salamu ya kusalimiana au kuagana (Hello au goodbye - kwa kiingereza kuonyesha msisitizo).  Linaweza kumaanisha amani kati ya Mungu na mwanadamu au kati ya mtu na mtu au mtu na kikundi cha watu. Kwa kiarabu neno hili shalom ni sawa na neno salaam, sliem. Kule nchini Syria wanaita  shlomo.


Basi ndugu zangu namshukuru Mungu wa amani aliyetupa neema ya kumtumikia jumamosi ya leo. 
Labda nimshukuru Mungu pia kwa ajili ya nchi yetu pia. Tumekuwa tukipita kwenye kipindi cha vuguvugu la mabadiliko ya kisiasa katika serikali yetu kwa wiki takribani tatu nne hivi. Hatimaye jana Rais wa nchi ameamua kufanya mabadiliko katika baraza la mawaziri hasa baada ya baadhi ya wizara kuwa zimekumbwa na kashfa ya wizi wa mali ya umma. Tunamshukuru Mungu kwamba hili nalo limepita na ni vema niendelee kutoa wito kwako ndugu yangu unayesoma makala ya leo tafadhali usiache kuliombea taifa letu. Na kipekee usiache kumuombea Rais wa nchi.
Ndugu zangu kama ilivyo kalenda yetu ya leo, tunaiangalia mithali sura ya 5. Na mstari tunaouangalia leo ni ule wa 21. Neno la Mungu linasema:
"Kwa maana njia za mwanadamu zi mbele za macho ya Bwana,Na mienendo yake yote huitafakari."
Mungu wetu aliye hai anajua sana mienendo na njia zetu. Mawazo yetu anayafahamu ipasavyo. Kabla hatujafanya kitu kwa kuwa lazima tukiwaze Mungu anakijua.Ndo maana anasema "Nami nayajua matendo yao na mawazo yao".
Siku moja Bwana Yesu aliwastukia watu walipokuwa wakiwaza uovu. "hali akijua mawazo yao, akasema, Mbona mnawaza maovu mioyoni mwenu?
Kwa hiyo Mungu anajua sana mawazo yetu na njia zetu. Hebu kwa kutambua hili tujione ya kuwa tu watupu mbele za Mungu. Hatuna kitu cha kuficha kwa hiyo tumtegemee Mungu katika maisha yetu.
Na tuchukulie hili kama changamoto ya kumtwisha Mungu mambo yetu tuyafanyayo kila siku. Neno la Mungu linasema haja zenu na zijulikane na Mungu kwa kuwa yeye hujishughulisha sana kwa mambo yenu.

Comments