SOMO:JINSI YA KULIELEWA NENO LA MUNGU

Na askofu Zacharia Kakobe
T unaendelea tena leo, kujifunza Kitabu cha YOHANA katika Biblia zetu.  Leo tunatafakari YOHANA 7:17-52.  Ingawa kichwa cha somo letu la leo ni, “JINSI YA KULIELEWA NENO LA MUNGU“, kuna mengi zaidi ya kujifunza katika mistari hii.  Tutayagawa mafundisho yote tunayoyapata katika mistari hii, katika vipengele kumi:-

(1)      JINSI YA KULIELEWA NENO LA MUNGU (MST. 17);
(2)      JINSI YA KUMTAMBUA NABII WA KWELI (MST. 18);
(3)      KUSHINDWA KWA WANADAMU WOTE KUISHIKA TORATI (MST. 19);
(4)      SABABU KUU YA KUMWITA MTUMISHI WA MUNGU KWAMBA ANA PEPO (MST. 19-20);
(5)      WAJIBU NA JINSI YA KUHUKUMU (MST. 21-24);
(6)      SABABU KUU YA WATU WENGI KUSHINDWA KUMPENDA MUNGU (MST. 25-29);
(7)      SAA YA KUKAMATWA (MST. 30);
(8)      NAMI NILIPO NINYI HAMWEZI KUJA (MST. 33-36);
(9)      MITO YA MAJI YALIYO HAI (MST. 37-44);
(10)    KOSA LA KUMHUKUMU MTU KABLA YA KUMSIKIA (MST. 31-32, 45-
             52).
(1)      JINSI YA KULIELEWA NENO (MST. 17)
Biblia, ni kitabu kinachochapishwa na kutolewa nakala nyingi sana na kusambazwa na kusomwa kwa wingi, kuliko Kitabu chochote kile kingine ulimwenguni, katika wakati wote na miaka yote.  Kwa mfano, kulingana na vitabu vyenye takwimu, “ENCYCLOPAEDIA BRITANNICA“ na “ENCYCLOPAEDIA AMERICAN“, mwaka 1932 peke yake Biblia zilizoschapishwa na kusambazwa kwa lugha mbalimbali duniani, zilikuwa 1,330,213,815.  Miaka 50 iliyopita kulingana na mtafiti anayeitwa HY PICKERING, ili kukidhi mahitaji ya Biblia, Chama cha Biblia cha BRITISH AND FOREIGN BIBLE SOCIETY, kililazimika kuchapa nakala moja ya Biblia kila baada ya SEKUNDE TATU mchana na usiku au karibu nakala 32,876 kila siku katika mwaka mzima.  Biblia hizi zilisambazwa katika ulimwengu mzima kwa kutumia makasha 4,583 yenye uzito wa karibu TANI 500!  Hata hivyo, jambo la kushangaza ni kwamba mamilioni ya watu wanaosoma Biblia hawaielewi!  Tunajuaje kwamba hawaielewi?  Maisha ya watu hawa hayabadiliki na kufuata maelekezo ya Neno la Mungu.  Tatizo ni nini?  Jibu tunalipata katika MST. 17 “MTU AKIPENDA KUYATENDA MAPENZI YAKE (MUNGU), ATAJUA HABARI YA YALE MAFUNZO“.  Kama mtu hayuko tayari kulitenda kila jambo atakalofundishwa na Mungu katika Neno lake, Roho Mtakatifu humwacha mtu huyo, hawezi kumfunulia chochote katika Neno la Mungu.  Matokeo yake hawezi kuelewa lolote!  Bila roho Mtakatifu hatuwezi kufunuliwa na kulielewa Neno la Mungu (1 WAKORINTHO 2:10, 13; YOHANA 16:13).  Wengi wetu hatulielewi Neno kwa sababu hatuko tayari kulitendas.  Hatua yoyote ya kushindana na kupingana na Neno la Mungu, humfanya Roho Mtakatifu kutuacha mara moja.  Kabla ya kulisoma neno au kujifunza Neno la Mungu kwa njia yoyote, ili tulielewe Neno la Mungu, hatuna budi kuwa na msimamo wa kutaka kulitenda Neno lake sawasawa na (YEREMIA 42:1-6).
(2)      JINSI YA KUMTAMBUA NABII WA KWELI (MST. 18)
Yeye anenaye kwa nafsi yake tu, huyo siyo nabii wa kweli.  Kunena kwa nafsi yake mtu, ni kuhubiri au kufundisha kinyume na Neno la Mungu.  Mtu wa jinsi hii, hatafuti Utukufu wa Mungu, bali wake mwenyewe.  Nabii wa kweli humhubiri Kristo, au kwa jinsi nyingine, hulihubiri Neno! (WAFILIPI 1:18;  2 TIMOTHEO 4:2).
 (3)     KUSHINDWA KWA WANADAMU WOTE KUISHIKA TORATI (MST. 19)
Wanadamu wote mble za macho ya Mungu, hakuna hata mmoja aliyeweza kuishika torati, maana mtu akiishika sheria yote, ila akajikwaa katika neno moja, anahesabiwa kukosa juu ya yote (YAKOBO 2:10).  Hivyo, mbele za Mungu, hakuna mwanadamu atendaye mema, la, hata MMOJA! (WARUMI 3:10, 12; 1 YOHANA 1:8).  Wanadamu wote tulistahili kuangikwa msalabani kama adhabu ya laana ya kutokuishika torati (WAGALATIA 3:10; KUMBUKUMBU 21:22-23).  Aliyempendeza Mungu sikuzote, na kufanya yaliyompendeza, ni Yesu Kristo pekee (MATHAYO 3:17; YOHANA 8:29).  Ni kwa sababu hii, tunahesabiwa haki BURE kwa neema yake, kwa neema yake, kwa njia ya ukombozi ulio katika Kristo Yesu kwa imani katika damu yake iliyomwagika msalabani, alipokufa kwa niaba yetu, ili awe upatanisho (WARUMI 3:24-26; 1 TIMOTHEO 2:5-6).
(4)      SABABU KUU YA KUMWITA MTUMISHI WA MUNGU KWAMBA ANA PEPO (MST.19-
               20)
Mtumishi yeyote wa Mungu anayeyafichua maovu yaliyo……………………………. katika jamii ya watu wanaojiita Wakristo, na kuyanena waziwazi kwamba hayampendezi Mungu, na kuisema kweli, huyu sharti watu hao watamwita ana pepo.  Dhambi zinapokubalika katika Kanisa lote la Mungu na watu wanaojiita Wakristo, wanapokuwa hawana tofauti na wapagani au mataifa, anapoinuliwa Mtumishi wa Mungu na kuleta mageuzi, sharti mtu huyo ataitwa ana pepo.  Yesu hapa alifichua maovu yao na kuisema kweli kwamba wanataka kumuua, wao wakakana, wakaipinga kweli hiyo wakati ilikuwa kweli; kinyume chake wakamwita ANA PEPO, ili kujikosa na kuhalalisha maovu yao!  (MST. 19-20, 23).  Hivyo ndivyo inavyokuwa wakati awote.  Haya yalimpata Martin Luther, John Wesley, Charles Finney na wote walioleta mageuzi ya jinsi hii nyakati zao.
(5)      WAJIBU NA JINSI YA KUHUKUMU (MST. 21-24)
“Ifanyeni hukumu iliyo haki“, ni mafundisho ya Yesu Kristo kwetu.  Hatupaswi kukaa kimya kwa visingizio vya Neno, “Msihukumu“, na kuacha kuyakosoa mafundisho potofu ya Mashahidi wa Yehova; Mormonism au Christ Church for Latter Day Saints, wanaoshika mafundisho ya Joseph Smith; au wanaojiita Wakristo na kusema wao siyo dhehebu, wanaofuata mafundisho ya William Branham; au mafundisho yanayofundisha watu kushika sabato leo, au mafundisho mengine yoyote yaliyo potofu.  Kukaa kwetu kimya na kuogopa “kuyasema madhehebu mengine“, siyo kufuata nyayo za Mchungaji Mkuu wa Kondoo, Yesu Kristo na kufanya hivyo, ni kuwaachia kondoo wetu wararuliwe na mbwa mwitu.  Huo ni uchungaji wa mshahara.  Yesu aliifanya hukumu iliyo haki, pale alipokuwa kinyume na kuishika Sabato, na tena pale aliposema “Jilindeni na *chachu* au mafundisho ya Mafarisayo na Masadukayo“. (MATHAYO 16:11-12; YOHANA 10:12; MATENDO 20:28-30).  Tunapaswa kufuata kielelezo cha Yesu.  Kanisa la Kwanza walizingatia kufanya hivyo (WARUMI 16:17; 2 YOHANA 1:9-11).  Watu wenye mafundisho potofu, hatupaswi kuwa na ushirika nao, tuwahesabu tu kama mataifa na kuwahubiria kweli na kutokukubali kusikia chochote kutoka kwao.
(1)         SABABU KUU YA WATU WENGI KUSHINDWA KUMPENDEZA MUNGU
            (MST.25-29)
Tangu zamani za kale, sababu kuu ya watu wengi kushindwa kumpendeza Mungu, ni watu hao kuacha kumwamini Yesu na kuokolewa, kwa kungoja kwanza WAKUU WAMWAMINI (MST. 26).  Wengine wanangoja kwanza baba na mama, mume au kiongozi wao wa dini aokoke, ndiyo eti nao waokoke, na wanafuata mafundisho yao tu kimkumbo.  Huu ni mtego mkubwa wa Ibilisi.  Ukitengwa ugali mezani kila mtu huchukua tonge lake mwenyewe!  Ndivyo ilivyo, damu imemwagika msalabani, wokovu tayari.  Kila mmoja anapaswa kuuchukua kwa imani.  Ni muhimu kukumbuka pia kwamba, kila mtu atalichukua furshi lake mwenyewe na kutoa habari zake MWENYEWE (WARUMI14:12; WAGALATIA 6:5).  Hakuna haja ya kungoja wakuu waokoke ndiyo nasi tuokoke.  Kufa hakufuati nani wa kwanza kuzaliwa!.
(7)      SAA YA KUKAMATWA (MST. 20).
Maadui zetu watatutafuta sana ili watushike na kutudhuru, hata hivyo, hatupaswi kuhofu.  Hatuwezi kufa mpaka saa yetu itakapowadia.  Juhudi zao zitagonga mwamba, wakati wote Bwana wetu atatupa mlango wa kutokea maana amesema atakuwa pamoja nasi hat ukamilifu wa dahari yaani mwisho wa mambo yote (MATHAYO 28:19-20; AYUBU 5:20, 26-27).
(8)      NAMI NILIPO NINYI HAMWEZI KUJA (MST. 33-36)
Hatuwezi kumwona Yesu pasipo Utakatifu na kutafuta kwa bidii kuwa na amani na watu wote (WAEBRANIA 12:14).  Ni wale tu wenye mioyo safi watakaomwona Mungu (MATHAYO 5:8).  Ikiwa tumejaa masengenyo, chuki, fitina, hasira, mawazo machafu, n.k. tutamtafuta Yesu tusimwone.
(9)      MITO YA MAJI YALIYO HAI (MST. 37-44)
Mtu akimpokea Roho Mtakatifu, ishara ya kwanza itakayoonekana kwake, ni kunena kwa lugha mpya kadri roho atakavyomjalia kutamka (MATENDO 2:4; 10:44-46; 19:6).  Maji yanapokuwa yanapita katika mto, hutoa aina fulani ya sauti isiyoweza kuelezeka.  Ndivyo alivyo mtu anenaye kwa lugha baada ya kumpokea Roho, mito ya maji hutoka ndani yake!
(1)            KOSA LA KUMHUKUMU MTU KABLA YA KUMSIKIA KWANZA NA KUJUA
             ATENDAVYO (MST. 31-32, 45-52)
Watu wengi hufanya kosa la kumhukumu Mtumishi wa Mungu kabla ya kumsikia kwanza anenavyo au anavyofundisha na kujua atendavyo.  Haitupasi kufanya hivi.  Watumishi waliotumwa na makuhani kumkamata Yesu, walikubali kwanza kumsikia na wakagundua kweli waliyokuwa wamefichwa na Shetani.  Kuna faida kubwa kuiga mfano wao.
…………………………………………………………………………………………………………………………………..
Ni sifa ipi ya kutuwezesha kuingia mbinguni?  Ni utakatifu (WAEBRANIA 12:14).  Ndani yake hakitaingia kamwe chochote kilicho kinyonge (UFUNUO WA YOHANA 21:27).  Kinyonge ni kipi?  Ni yule anayetenda dhambi.  Huyu ni mtu asiyefaa, ni mnyonge!  Je, wewe ni mtakatifu?  Jibu ni la!  Maisha yako yamejaa dhambi, pamoja na kusema una dini; hivyo wewe pia ni mnyonge, hufai kuingia mbinguni. Ukitubu leo dhambi zako zote kwa kumaanisha kuziacha, na kuifuata njia ya Yesu Kristo, ndipo utakapopata rehema ya kuingia mbinguni (MITHALI 28:13;  YOHANA 14:6).  Je, uko tayari kutubu sasa ili upate rehema hii?  Najua uko tayari.  Basi fuatisha sala hii ya toba kwa dhati kutoka moyoni;  Mungu Baba asante kwa ujumbe huu.  Hakika mimi ni mnyonge, mwenye dhambi.  Sistahili kuingia mbinguni. Natubu dhambi zangu zote kwa kumaanisha kuziacha.  Kuanzia leo nataka niifuate njia ya Yesu Kristo.  Bwana Yesu niwezeshe.  Asante kwa kunisikia katika Jina la Yesu.  Amen.  Mpendwa msomaji umekubaliwa kuingia mbinguni.  Ili uzidi kudumu katika utakatifu mpaka siku ya kuiaga dunia hii, hakikisha unahudhuria mafundisho katika Kanisa linalohubiri wokovu.  MUNGU AKUBARIKI !!!

  Neno la Uzima kutoka kwa  Askofu Zachary Kakobe     tembelea sehemu zifuatazo katika inernet  
Tovuti       : www.bishopzacharykakobe.org
Facebook : www.facebook.com/bishopkakobeministries
Youtube   : www.youtube.com/user/bishopkakobe

Comments