![]() |
Kukaa katika neno la MUNGU ni jambo jema sana , na wengi wanaorudi nyuma ni kwa sababau hawana muda na MUNGU. |
Nakusalimu ndugu yangu katika jina la Yesu.
Nabii Isaya akitabiri kwa habari ya Yuda na Yerusalemu alisema "Ole
wake, taifa lenye dhambi, watu wanaochukua mzigo wa uovu, wazao wa
watenda mabaya, watoto wanaoharibu; wamemwacha Bwana, wamemdharau yeye
aliye Mtakatifu wa Israeli, wamefarakana naye na kurudi nyuma" - Isaya 1:4
Nataka
nikusaidie wewe ndugu yangu uliyerudi nyuma katika kumtumikia Mungu.
Nataka nikusaidie wewe ambaye umekuwa ukitamani umtumikie Mungu kwa
uaminifu kabisa lakini umekuwa ukishindwa. Nataka nikusaidie wewe ambaye
umekuwa ukitamani kuihubiri injili ya Yesu pasipo uoga lakini umerudi
nyuma. Nataka nikusaidie wewe ambaye umerudi nyuma hata sasa huwezi hata
kuomba tena. Kila ukijitutumua nguvu huna za kuomba. Nataka nikusaidie
wewe uliyerudi nyuma na sasa hata kanisani au katika ibada za katikati
ya wiki huwezi hata kujihudhurisha pamoja na wapendwa wenzio. Nataka
nikusaidie wewe ambaye umeoa lakini huachi kuchepuka kila iitwapo leo.
Nataka nikusaidie wewe uliyerudi nyuma sababu ya dhambi iwayo yote.
Babu yetu Yohana anatufundisha tukiwa tumerudi nyuma tufanyeje. Asema hivi:
"Watoto
wangu wadogo, nawaandikia haya ili kwamba msitende dhambi. Na kama mtu
akitenda dhambi tunaye Mwombezi kwa Baba, Yesu Kristo mwenye haki, naye
ndiye kipatanisho kwa dhambi zetu; wala si kwa dhambi zetu tu, bali na
kwa dhambi za ulimwengu wote" - 1 Yoh. 1:1-2
Nabii Isaya yeye anatuambia kwamba 'tukikubali na kutii tutakula mema ya nchi' na kwa habari ya kumkosea Mungu sababu ya dhambi zetu Mungu anena kwa kinywa cha Isaya akisema "Jiosheni,
jitakaseni; ondoeni uovu wa matendo yenu usiwe mbele za macho yangu;
acheni kutenda mabaya; jifunzeni kutenda mema; takeni hukumu na haki;
wasaidieni walioonewa; mpatieni yatima haki yake; mteteeni mjane" - Isaya 1:16,17
Ndugu yangu njia ni moja tu. Acha kutenda mabaya na jifunze kutenda mema full stop! Hakuna njia mbadala nje ya hapo. Matendo mema ndiyo tuliyowekewa tuyatende tangu kuumbwa kwa ulimwengu huu. "Maana
tu kazi yake, tuliumbwa katika Kristo Yesu, tutende matendo mema,
ambayo tokea awali Mungu aliyatengeneza ili tuenende nayo" - Efe 2:10. Ndiyo, tunapaswa kutenda mema.
Na
wataka kuniuliza najifunzaje kutenda mema? Ni rahisi. Akili ya
mwanadamu ni mfumo. Ni mfumo ambao ukizoezwa kufanya jambo fulani
unazoea na kuendelea kuufanya maishani mwake.
Paulo anatufundisha hivi: "nawe ujizoeze kupata utauwa"
- 1 Tim 4:7. Kujizoeza maanake nini? Maanake umekuwa ukifanya jambo
hilo mara kwa mara kiasi kwamba mwili, akili na nafsi vimeshazoea.
Unadhani mtu kuamka alfajiri kuomba ni jambo jepesi bila kujizoeza? Au
wadhani mtu au familia kukutana kila siku kuomba ni jambo linalotokea
kwa bahati? Ni lazima kujizoeza. Petro asema kuna watu "wenye mioyo iliyozoezwa kutamani" - 2 Petro 2:14.
Sijui
unanielewa hapo ndugu? Kuna watu wamezizoeza akili zao kufanya mambo
fulani fulani na tayari imeshakuwa sehemu ya maisha yao ya kila siku.
Kuna
watu wameshajizoeza kuvuta sigara kila siku. Asipovuta anakuwa kama
mjinga fulani hivi. Kuna watu wamejizoeza kulewa. Asipolewa hajisikii
kama yuko duniani. Hujawahi kuona au kusikia kwamba kuna daktari bila
kulewa hawezi kufanya kazi?
Kuna
watu wameizoeza miili yao pasipo zinaa hawawezi kuishi. Wanaubadili
hata ukweli wa Mungu kwamba kijana kama hajaoa au kuolewa hawezi kuishi
bila kufanya tendo la ndoa. Wamezizoeza akili na miili yao hivyo. Lakini
kwetu tulio katika Kristo tujifunze kuzizoeza akili, na miili na mioyo
yetu katika utakatifu.
Mwandishi
wa kitabu cha Waebrania atufundisha jambo jingine jema akisema
"..Chakula kigumu ni cha watu wazima, ambao akili zao, kwa kutumiwa,
zimezoezwa kupambanua mema na mabaya" Ebr 5:14. Kwa hiyo ndugu yangu
anza kujifunza kutenda mema. Ulirudi nyuma katika maombi anza kujifunza
kuomba. Izoeze akili, moyo na mwili wako kutenda mema.
Na Mungu wa
mbinguni akubariki.
Ushuhuda wa injili
Comments