JINA LA BWANA YESU NI NGOME IMARA , UKIKIMBILIA LEO UNAKAA SALAMA.




Shalom watu wa MUNGU.

BWANA YESU asifiwe.

Mimi ni mzima na nakukaribisha  tujifunze somo hili  ambalo MUNGU amenipa kwa ajili yako , na yangu na ya wengine wote watakaosoma miaka yote.

''Mithali 18:10- Jina la BWANA ni ngome imara; Mwenye haki huikimbilia akawa salama.''

-Mambo mawili(2) makubwa yanapatikana kwenye mstari wa Biblia hapo juu.

         1: JINA LA BWANA NI NGOME IMARA.

         2: MWENYE HAKI HUIKIMBILIA AKAWA SALAMA.

Umuhimu wa mambo haya mawili unategemeana yaana mwanadamu anahitaji kitu kwa BWANA na BWANA anaangalia sifa za mwanadamu huyo mhitaji, kama anastahili kupokea au hastahili.

                1: JINA LA BWANA NI NGOME IMARA.

BWANA hapa ni MUNGU mwenyezi.

MUNGU ameiweka ngome imara ndani ya jina la YESU KRISTO.(Wafilipi 2:9-11, Kwa hiyo tena MUNGU alimwadhimisha mno, akamkirimia Jina lile lipitalo kila jina; ili kwa jina la YESU kila goti lipigwe, la vitu vya mbinguni, na vya duniani, na vya chini ya nchi; na kila ulimi ukiri ya kuwa YESU KRISTO NI BWANA, kwa utukufu wa MUNGU Baba. ).

Kwa hiyo jina la BWANA YESU ni ngome imara,

BWANA YESU ndiye ambaye jina lake pekee tunaweza kuomba kwalo na kupokea.

Jina la YESU KRISTO ndilo jina kuu kupita majina yote, na jina hili BWANA YESU alipewa na MUNGU Baba.

Hata ujio wake hapa duniani, malaika wa MUNGU alisema yafuatayo kwa Yusufu mchumba wa Mariamu. ‘’Mathayo 1:21-Naye(Mariam) atazaa mwana, nawe utamwita jina lake YESU, maana,  yeye  ndiye atakayewaokoa watu wake na dhambi zao.’’

-Hivyo jina la YESU KRISTO ni ngome imara, na pale linapotajwa uzima unaingia. Nimewahi kuona kwa macho yangu jina la YESU KRISTO likitajwa na uzima kutokea. Dda mmoja alipona ukimwi mbele ya macho yangu kule Zanzibar maana aliombewa na kwenda kupima na kuleta majibu kutoka hospital 3 alizokua amenda kupima, kote huko walimwambia amepona, UTUKUFU KWA BWANA YESU. Watu wengi wamepona kifua kikuu, Malaria, uvimbe tumboni, kuharibika sehemu za siri na kila ugonjwa na kila udhaifu.

HAKIKA JINA LA BWANA YESU NI NGOME IMARA.

NGOME ni ulinzi uliozunguka pande zote, kama askari wataweka ngome sehemu fulani ina maana kila upande wa eneo kutakuwa na ulinzi, tena masaa yote, ni ngumu sana kuingia kwenye ngome kama hii. Lakini jina la BWANA YESU ni zaidi ya hizo ngome za kibinadamu.  Zaburi 27:1b inasema ‘’BWANA  ni ngome ya uzima wangu, Nimhofu nani?’’

Ndugu kimbilia kwenye ngome hii leo, kuingia kwenye ngome hii ni bure kabisa.

          2: MWENYE HAKI HUIKIMBILIA AKAWA SALAMA.
 

Jambo la pili katika andiko tuliloanza nalo ni MWENYE HAKI AKIKIMBILIA ANAKAA SALAMA.

Mwenye haki ni mtu gani? 
Na kwa nini sio kila mtu akikimbilia ngome hii anakua salama?

Je haki hii inatafutwaje?

Je haki hii hudumu kwa muda gani?

Je tunalipia pesa kiasi gani kuipata hii haki muhimu maishani?

Yawezekana unajiuliza maswali kama hayo hapo juu na hujapata majibu.

Ndugu haki hii ya kuiendea ngome hii na ukawa salama unaipa kwa kumpokea BWANA YESU. (Yohana 1:12-13Bali wote waliompokea aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa MUNGU, ndio wale waliaminio jina lake; waliozaliwa, si kwa damu, wala si kwa mapenzi ya mwili, wala si kwa mapenzi ya mtu, bali kwa MUNGU. ).

Jambo kuu kwa kila mwanadamu ni kumpokea YESU kama BWANA na MWOKOZI wa maisha yao.

BWANA wenyewe anasema kwamba kama tukimkabidhi maisha yeye. Yeye(YESU) na BABA yake watakuja na kufanya makazi ndani yako yaani kwa maana nyingine watakuja na kuweka ngome ndani yako.

-Mwenye haki wa kuiendea ngome hii ni yule aliyemkabidhi BWANA YESU maisha yake.

-Haki hii inatafutwa kwa wewe kuokoka na kulikulia neno la MUNGU pamoja na wengine kanisani.

-Haki hii hudumu siku zote za maisha yako kama tu na wewe utadumu kukaa ngomeni yaani kwa YESU KRISTO.

-Huhitaji kulipa pesa ili kuipata haki hii muhimu bali ni wewe tu kumpokea BWANA YESU. Warumi 10:9 -11 ( Kwa sababu, ukimkiri YESU kwa kinywa chako ya kuwa ni BWANA, na kuamini moyoni mwako ya kuwa MUNGU alimfufua katika wafu, utaokoka.  Kwa maana kwa moyo mtu huamini hata kupata haki, na kwa kinywa hukiri hata kupata wokovu. Kwa maana andiko lanena, Kila amwaminiye hatatahayarika. ).

-Baada ya wewe kuipata haki hii muhimu , kinachofuata ni wewe kuifuata ngome hii imara kwa maombi na hakika utakaa salama. Yeye MUNGU anasema hivi juu ya mtu uliyetimiza vigezo hapo juu (Isaya 54:17,Kila silaha itakayofanyika juu yako haitafanikiwa na kila ulimi utakaoinuka juu yako katika hukumu utauhukumu kuwa mkosa. Huu ndio urithi wa watumishi wa BWANA, na haki yao inayotoka kwangu mimi, asema BWANA. )    

Tena BWANA anasema kwamba juu yako mwenye haki ambaye umeamua kukaa ndani ya KRISTO maisha yako yote. Yeremia 1:19 ,(Nao watapigana nawe; lakini hawatakushinda; maana mimi nipo pamoja nawe, asema BWANA, ili nikuokoe. ) 

Ndugu zangu ni furaha sana kuwa ngomeni mwa BWANA YESU, Wacahwi watakuogopa wewe badala ya wewe kuwaogopa, na BWANA anasema kwamba Yohana 14:14, ( Mkiniomba neno lo lote kwa jina langu, nitalifanya. )

Ndugu zangu watu wa MUNGU wakati mwingine tunakosea kwa kuwa ngome wa BWANA YESU lakini tunashindwa kuomba au kukimbilia badala yake tunataka kutumia akili zetu wenyewe na wengine kwa sababu ya maarifa yao ya kibinadamu wanajaribu kuishi bila kumtegemea BWANA . ni mbaya sana.

Naomba tuwe na haki siku zote na siku zote tulikimbilie jina la BWANA YESU ili tukae salama siku zote.

Unganisha jina la YESU KRISTO na haki yako uliyopewa na MUNGU ili uombe na kukaa salama , omba pia kwa ajili ya ndugu zako, familia yako na taifa lako. Maana wewe ukiwa ngomeni mwa YESU unauwezo wa kuwasaidia hata ndugu zango maana haki yako itasikiwa na MUNGU na watakuwa salama wao kwa sababu ya maombi yako.

-Pia usisahau kwamba shetani naye huweka ngome zake lakini wewe uliye na ngome ya jina la YESU KRISTO unaweza kuziangusha ngome zote za giza kama walivyofanya hivyo watumishi wa MUNGU wa zamani ona mfano jinsi Daudi alivyoangusha ngome za adui  2 Samweli 5:7-10( Lakini Daudi aliipiga NGOME ya Sayuni; huu ndio mji wa Daudi. ..................Naye Daudi akazidi kuwa mkuu; kwa maana BWANA, MUNGU wa majeshi, alikuwa pamoja naye. ) na Daudi kwa sababu anamjua MUNGU wake anasema katika 2 Samweli 22:2 kwamba ‘’BWANA ndiye jabali langu  na mwokovu wangu, naam, wangu’’ na katika Mstari wa 33 wa hiyo hiyo 2 Wafalme 22 Daudi anasema  ‘’MUNGU ndiye ngome yangu yenye nguvu, Naye huwaongoza wakamilifu(wenye haki) katika njia yake’’

JINA LA BWANA YESU HAKIKA NI NGOME IMARA SANA, TUKIMBILIE LEO ILI TUWE SALAMA.


MUNGU akubariki sana na kama hujampokea BWANA YESU muda wa kumpokea ni leo wala sio kesho, amua leo na atakuandika jina lako katika kitabu cha uzima na utaanza kuukulia wokovu kwa mafundisha kanisani. ROHO MTAKATIFU aliyenipa ujumbe huu ana makusudi kabisa na wewe, hataki upotelee motoni anataka uende uzimani aliko KRISTO BWANA.


                       MUNGU akubariki sana .

                        Ni mimi ndugu yako

                          Peter M Mabula

                    Maisha ya Ushindi Ministry.

                         0714252292

Comments