KWAYA ILIYOMTOA CHIDUMULE, KUZINDUA ALBUM YAKE ILIYOPENDWA SANA JUMAPILI HII



"Nakushukuru Mungu, Umenitoa Mbali kwenye shimo la dhambi, Sasa nafurahia ndani ya nyumba yako Baba Baba, sina cha kukulipa",  ni baadhi ya maneno yanayopatikana katika wimbo maarufu unaoitwa Nakushukuru Mungu ulioimbwa na Kwaya ya Vijana Msasani ambayo sasa inajulikana kama Kwaya ya Ukombozi, wimbo ambao ulitamba sana hasa enzi hizo kupitia redio Tumaini katika kipindi cha muziki na nyimbo za dini.

Kwaya hii ya Ukombozi ni moja kati ya kwaya ambazo zimejipatia umaarufu mkubwa katika ramani ya muziki wa injili na kumtukuza Mungu ndani nan je ya mipaka ya Tanzania.

Kwaya hii pia iliwahi kusikika miaka ya mwishoni mwa 90 waliposhirikiana na muimbaji mkongwe Cosmas Chidumule katika album ya Kiatu cha Yesu ambapo kwaya hii ilishiriki kuitikia nyimbo zote pamoja na kupiga muziki katika album hii iliyotoa nyimbo maarufu kama Yesu ni Bwana na Libarikiwe Neno.

Ukombozi ilianzishwa rasmi mwaka 1977 na ina makazi yake katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania Usharika wa Msasani ikiwa na takribani waimbaji 50 ambao kwa pamoja wamenia kumtumikia Mungu kwa kutumia vipaji vyao vya muziki na uimbaji.

Mabadiliko ya jina

Mwaka 2007 ndipo kwaya hii ilibadili jina na kuitwa Ukombozi kutoka kuitwa Vijana Msasani na mwenyekiti wa sasa wa kwaya hii Bwana Erick Mchome anaelezea sababu ya mabadiliko hayo.

‘’Yalikuwa ni mabadiliko makubwa kutokea kwenye usharika lakini ilikuwa ni mpango wa Mungu kutaka kupanua mipaka ya huduma yetu kwani kanuni za kanisa ziliagiza waimbaji wa vijana wawe na umri Fulani lakini ndani yetu kulikuwa na wengi waliozidi umri huo hivyo ililazimu tubadili jina,’’ anasema Bwana Mchome.

Kwa mujibu wa Bwana Mchome mabadiliko haya hayakuwa kitu rahisi, yaliipitisha kwaya katika mambo magumu na hayakuishia tu kwenye jina bali hata kubadili mtindo wa uimbaji ili kuamsha ari ya waimbaji na kupeleka injili kwa mtindo bora zaidi.

Njia ngumu ya utumishi

‘’Zipo nyakati kwaya ilibaki na watu saba tu wakihudumu ibadani, fikiria kutoka watu tisini waliokuwepo awali kubaki na watu saba lakini hatukukata tamaa ikabidi tusonge mbele,’’ anaelezea Bwana Mchome.

Kuporomoka kwa huduma ya Ukombozi miaka ya 2007 hadi 2009 mwanzoni kulichangiwa na mambo mengi hata hivyo kama maandiko ya Mungu yanavyosema neno la Mungu halitamrudia bure, Ukombozi ilifanikiwa kusimama tena kwa kishindo mwaka 2009 mwishoni kwa kutoa album ya video iliyoitwa Yatosha.

Mrs Margaret Kato akiimbisha wimbo ndani ya Ukombozi.

Yatosha ilikuwa ni mwanzo mwingine wa safari ndefu na kubwa ya huduma ya kwaya hii ambapo Ukombozi walijipatia mialiko mingi ya kwenda kuhubiri kwa njia ya nyimbo hata nje ya mipaka ya Tanzania.

‘’Ilikuwa ni kama mpambazuko wa siku nyingine njema, tulimuona Mungu akilirudisha kundi kwa kiasi cha ajabu na moyo mkuu wa utumishi na sasa kwaya iko katika hali nzuri,’’ anafafanua Bwana Mchome.

Nguvu mpya ya huduma

Mwaka jana mwanzoni kwaya ya Ukombozi iliingiza sokoni tena album ya video nyingine iitwayo Sabuni ya Roho ambapo ndani yake kulikuwa na wimbo maarufu uitwao Ni Kwa Neema na nyinginezo nyingi. Uzinduzi wa album hii ulishuhudiwa na wageni mbalimbali akiwemo Waziri Mkuu Mstaafu, Edward Lowassa aliyekuwa mgeni rasmi.

Mpaka sasa album ya Sabuni ya Roho imeshauza nakala takribani elfu tano na inazidi kufanya vizuri chini ya usambazaji wa kampuni ya Umoja Audio and Visual Company.

Kufuatia mafanikio haya kwaya hii inayofundishwa na walimu watatu imeamua kufanya ibada ya pekee ya kumshukuru Mungu siku ya tarehe 6 mwezi Aprili katika usharika wao wa nyumabani Msasani ambapo wageni mbalimbali wamealikwa kuhudhuria ibada hii.

Safu ya wapigaji wa Ukombozi kwaya wakiongozwa na Norman wa kwanza kushoto.


‘’Hakika mahali tumefika tumeuona mkono wa Bwana na tumeona tutoe sadaka ya shukrani kwa Mungu maana kama si mkono wake huduma yetu isingeendelea kuwepo hadi leo katika nguvu hii tuliyonayo sasa,’’ anaweka wazi Bwana Mchome.

Kwa sasa Ukombozi ni kati ya kwaya kubwa inayolinganishwa na CVC ya AIC Chang’ombe hasa kutokana na mtindo wa uimbaji wanaoutumia na wamekuwa wakipata mialiko mingi kwenda kuhudumu kanda ya ziwa na kwingineko.

Mwaka jana peke yake kwaya hii ilifanikiwa kwenda Mafinga Iringa, Lushoto Tanga na Vigwaza mkoa wa Pwani kwa ajili ya huduma ambapo Mungu aliinuliwa kipekee sana.

Uzinduzi wa Nakushukuru Mungu

Sadaka ya shukrani itakwenda sambamba na uzinduzi wa remix album ya Nakushukuru Mungu audio ambapo ndani yake kuna nyimbo kama Usinipite, Sema Kitu na Nakushukuru Mungu ambao umejizolea umaarufu miongoni mwa watanzania wengi.

Kwa mujibu wa mwenyekiti Bwana Mchome, Ukombozi walifikia maamuzi ya kuurudia wimbo huu ili uendane na teknolojia ya sasa maana watu wengi bado wanauhitaji na hivyo kwaya iliona ni vema kuitikia wito.

Kama ilivyo kwa album ya Sabuni ya Roho, Nakushukuru Mungu pia imefanyiwa kazi katika studio za CVC Chang’ombe chini ya mtayarishaji Steven Deffa ambaye ametengeneza album nyingi zinazofanya vizuri kama Usiku wa Manane na Mtu wa Nne ya Kinondoni Revival Choir.


‘’Hii ni siku ya muhimu kwetu maana Daudi anatuagiza kumshukuru Mungu kwa kila jambo, hata kwa magumu tuliyopitia bado kumshukuru Mungu ni jambo muhimu sana,’’ anasema Mchome.

Mwenyekiti wa kwaya bwana Erick Mchome.
Siku hii pia itajumuisha mualiko wa waimbaji mbalimbali wa zamani waliombia kwaya hii ambapo wapo maaskofu kama Stephen Munga wa Dayosisi ya Lushoto na Profesa Godwill Mrema wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ambao hawa wote waliwahi kuwa wenyeviti huko zamani.

Kwa mwaka huu kwaya imedhamiria kupanua mipaka ya kufanya huduma kwa kutembelea mikoa mbalimbali kumtangaza Kristo na pia iko katika mchakato wa kupata basi la kutumuia kwa ajili ya huduma yao. 


                Chanzo: Gospel kitaa

Comments