UHUSIANO MGUMU

Na Frank Philip.


"BWANA akamwambia Musa, Hapo utakaporudi Misri, angalia ukazifanye mbele ya Farao zile ajabu zote nilizozitia mkononi mwako; lakini nitaufanya mgumu moyo wake, naye hatawapa ruhusa hao watu waende zao" (Kutoka 4:21).

Kila uhusiano una makusudi maalumu. Kuna mahusiano ya aina mbali mbali: uchumba, ndoa, familia, kazini, nk. Katika mahusiano haya yote kutakuwa na michakato na mawasiliano kati ya mtu na mtu ili kufanikisha mambo fulani lakini pia ili kumpatia kila mmoja wao masilahi fulani (kiwili au kiroho) katika uhusiano husika.

Musa na Farao walikuwa na UHUSIANO MGUMU. Musa anatumwa kwa Farao kuomba jambo huku anajua kabisa kwamba ATANYIMWA, lakini alikwenda. Sio jambo rahisi kujua kwamba umenyimwa jambo kabla hata ya kuomba na ukapata nguvu ya kwenda kuomba. Musa hakubishana na Mungu na kumwambia "kama unajua kwamba Farao atakataa kwanini unanituma sasa?" Musa alimtii Mungu katika hali zote, japo kuna wakati ilikuwa ngumu kurudi kwa Farao kwa ukorofi wa Farao lakini alirudi tena kila siku alipoagizwa kwenda.

Nisikilize. Musa alikuwa "darasa" na Farao alikuwa "darasa". Kupitia "ugumu wa moyo wa Farao", Mungu aliweza kufanya ajabu zake zikawa nyingi juu ya Misri. Kwa kupitia ajabu hizi, Farao, Wamisri, Wana wa Isarael na Musa, wote "walijifunza" ukuu wa Mungu. Kwa kupitia Musa, Farao na watu wote walijua yuko Mungu mwenye UWEZA katikati ya wanadamu. Kilikuwa ni kipindi cha shule ya Mungu kwa watu wote; Musa akiwa darasa na Farao akiwa darasa pia. Kila darasa lilikuwa na masomo yake ya maana sana.

Jua jambo hili. Musa hakuomba mapigo juu ya Misri ila aliomba mapigo yaondoke yalipokuja. Kila pigo haikuwa "wazo" la Musa, ila alisikia kwa Mungu aina ya pigo na aliagizwa kitu cha kufanya ili hayo mapigo yatimie; kama Farao hatawapa wana wa Israel ruhusa. Angalia, Musa alikuwa na uwezo wa kulaani, au kuita mapigo juu ya watesi wake, ila hakufanya hivyo isipokuwa "lile Mungu alilosema" ndilo lilitendeka! Musa alipewa uwezao wa kufanya MIUJIZA ila hakufanya muujiza wowote bila kuagizwa afanye kwa KUSUDI na MAHALI maalumu. Kila pigo ambalo liliteremka juu ya Misri, Musa aliliona kabla na kujua cha kufanya, ila alienda kwanza kuongea na Farao na kuomba ruhusa ya wana wa Israel kuondoka. Nikitazama kwa makini naona kabisa Musa hakuwa anafurahia mapigo na wala hakuomba watu wapigwe, ila uaminifua wake uliruhusu "mkono wa Mungu uwe na nguvu sana juu ya Misri".

Katika maisha yetu kuna makundi tofauti ya watu. Kuna watu watakupinga tu hata kama uko sahihi. Wengine watakufanyia ugumu katika njia yako ili uteseke. Wengine watafurahi uangukapo. Wengine watakasirika kila ufanikiwapo na watakuadhibu kwa kutokupa ushirikiwano. Wengine wachache watasimama pamoja na wewe katika shida zako kama jinsi ambavyo kila siku Haruni alisimama na Musa mbele za Farao. Jua siri hii, Mungu anashughulika na watu wanaoshughulika na wewe, hata kama huoni; Mungu hatakaa kimya uangamizwe. Yeye amejiita "Mlinzi wa Israel, hatasinzia usiku na mchana, anakulinda na kukuzunguka kwa ukingo". Hii siri ni kubwa, wewe huoni kama ambavyo Ayubu alikuwa haoni; ila Ibilisi aliona na kuona wivu jinsi ambavyo Ayubu alizingirwa na Mungu. Kwa kadri unavyokuwa mwaminifu mbale za Mungu, Mungu anashughulika na mambo yako na adui zako pia. Huna haja ya kulaani mtu, kama wewe ni "mboni ya jicho lake", acha mtu akaguse mboni ya jicho la Mungu halafu Mungu atajua mwenyewe cha kumfanya. Jicho huwa halijitetei, Mkono utakuja kutetea jicho; kama wewe ni mboni ya jicho la Mungu, Mkono wa Mungu utakuja kukutetea ukiguswa.

Maadui watakuwepo maishani mwetu siku zote. Hutaweza kuwamaliza kwa sababu wengi wa hawa maadui wanakuwepo kwa KUSUDI la Mungu pia. Hata ukiwafayia wema, bado watatafuta kukuangamiza, kumbe! Ni Mungu amewaleta ili akupime utakavyoshughulika nao! Angalia mfano wa Daudi na Sauli. Ilifika mahali Daudi akasema "adui zangu ni wengi kuliko nywele za kichwa changu", na ikafika mahali akakata tamaa ya kuishi hata akasema "bado kidogo tu Sauli ataniua". Nisikilize, usiogope wala usiwachukie adui zako; hao ni ngazi ya kupandia juu. Unapowachukia au kukasirishwa nao, jua unajipunguzia nguvu na ushindi dhidi yao. Jinsi unavyomtizama Mungu, kumshukuru na kuwaombea adui zako; hali ya uchungu nao inakwisha ila MKONO wa Mungu unakuwa na nguvu juu yao; huku wewe ukibarikiwa na kuinuliwa. Adui zako watamwona Mungu akishughulika nao kwa namna ya tofauti; wengine wataokolewa na wengine wataangamia bila wewe kujua. Utawatafuta na kumbe! hawapo.

Angalia tena habari ya Daudi; kabla hajashughulika na Goliathi alishughulka na dubu na simba WENGI. Unafikiri Mungu hakujua kukemea dubu na simba wasije kwenye kondoo wa Daudi? Je! Mungu hakuwaleta dubu na simba kumjenga musuli Daudi kupambana na Goliath? Je! Sauli alipoamua kuwa ADUI wa Daudi, na kutaka kumwangamiza kwa kumtuma kwenye kambi ya Wafilisi ili akauwawe, Je! haikuwa njia ya kumwimarisha Daudi ili awe Mfalme mwenye heshima kati ya watu wake? Kila adui utakaye pambana naye na kumshinda kwa HAKI ujue utapata heshima kwake na kupandishwa cheo na Mungu. Sio kitu rahisi kupata heshima mbele ya adui yako kama hujui kumsikiliza Mungu na kujifunza kumpenda adui yako. Jifunze pia kwamba maadui huja kwa msimu. Kila msimu na adui wake; wote watakuja kwako kama DARASA, ili umwone Mungu akikuokoa na pia ujue hao wamekuwa MTIHANI wa wewe kupanda cheo kwenda kwenye ngazi nyingine. Usilalamike wakija, ukiisha kujua kwamba "watakupinga na kukukatalia kila kitu" kama Musa, jua msimu wa kuongezwa umekaribia. Mtizame Mungu, usiwalaani kwa saabu "ukilaani utalaaniwa", bariki siku zote na kumwacha Mungu ashughulike na adui zako.

Wakati Musa na wana wa Israel wanatoka Misri, walifika mahali wanahitaji "njia pasopo na njia". Hapa mahali Mungu alipaona, lakini aliacha tu wapafike kwanza. Mahali pagumu pako mbele yako ili Mungu ajitukuze juu ya adui zako. Uwe makini ukifika "ufukweni" wakati huna mtumbwi, huo ni wakati wa "kutembea juu ya maji au mahali pakavu baharini"! Nisikilize kwa makini hapa, narudia tena, "Uwe makini ukifika "ufukweni" wakati huna mtumbwi, huo ni wakati wa "kutembea juu ya maji au mahali pakavu baharini", usijitafutie MIUJIZA (attention kwa watu), wakati wa miujiza ukifika mijiza hutendeka kwa UTUKUFU wa MUNGU, kwa wakati na mahali maalumu Mungu alipokusudia, Je! unatamani miujiza itokee mbele za watu? Jiulize ili iweje? Acha kutaka kutamani KUONEKANA wewe, Mungu akitaka kujionyesha mwacha ajinyeshe mwenyewe, ili na wewe ushangae matendo makuu ya Mungu; sio wewe "kuwashangaza watu na matendo makuu ya Mungu ili kujitwalia heshima mbele zao", chunga hii roho imewaangusha wengi. Mungu akikufikisha mahali "pasipo na njia", hakika Atafanya njia, na adui zako na watu wengine watapata DARASA jingine hapo wakati wewe unavuka ng'ambo. Angalia hapo, Musa hakuomba Wamisri wafe, ila aliomba ajue NJIA ya kusonga mbele. Musa alisahau hata kama yeye ni mtu wa miujiza (a miracle woker), hadi Mungu anamkumbusha "umebeba nini mkononi?" Acha Mungu jitukuze kwenye njia zako na sio kujitukuza wewe kwa jina la Mungu. Achana na kushughulika na malipizi kwa adui zako, Mungu anajua cha kuwafanya! Usipoteze muda wako kulaani watu, chukua muda kuwaombea na kuwabariki, Mungu anajua cha kuwafanya. Musa akanyoosha fimbo juu ya maji yakapasuka, wakapita mahali pakavu. Njia ile ile walikovuka Musa na wana wa Israeli, ndipo walipoangamia Wamisri!

Mahusiano mengi sana yamekuwa magumu kwa sababu watu wameshindwa kumwona Mungu katikatiyao. Wamelaumiana na kushindwa kujua kwamba kila mmoja wao ni DARASA kwa mwenzake. Angalia usiwe Farao kwa maana mwenzako ataona unavyoangamia kwa sababu ya kushupaza shingo na kufanya moyo mgumu "kumtii Mungu". Kila siku UHUSIANO utakufikisha mahali pa kuchagua. Umtii Mungu au Shetani. Kila siku kuna mahali utafanya maamuzi tu, na haya maamuzi yatapanga hatua yako itakayofuata kwenye UHUSIANO wako; iwe ni ndoa au uhusiano wowote ule. Wengine walipofika "mahali pa gumu" kwenye uhusiano, walimtenda Mungu dhambi! Angalia hapo kwenye shida yako hutavuka hadi UFAULU huo mtihani, huku ukimpendeza Mungu. Jifunze kujua KUSUDI la Mungu katika uhusiano wako na usimame katika kusudi hilo na kumtii Mungu, hata kama mwenzako ni kama Farao. Kwa kufanya hivyo utakuwa na USHINDI siku zote na NGUVU juu ya adui yako au mwenzako.

Frank Philip.

Comments