Bomu lalipuka ndani ya kanisa la KKKT jijini Mwanza na kujeruhi Mhudumu wa Kanisa


Mhudumu wa nyumba ya kupumzikia wageni wa Kanisa la KKKT Dayosisi ya Mashariki ya Ziwa Victoria, jijijini hapa, amejeruhiwa vibaya baada ya kulipukiwa na bomu lililokuwa limewekwa kwenye korido la nyumba hiyo. 
Mhudumu wa nyumba ya kupumzikia wageni wa Kanisa la KKKT Dayosisi ya Mashariki ya Ziwa Victoria, jijijini Bernadetha Alfred (25) akiwa amelazwa katika Hospitali ya Bugando baada ya kulipukiwa na Bomu hilo jijini Mwanza
 Tukio hilo lilitokea jana (Jumatatu), kati ya saa 1:45 na saa 2:20 usiku, katika eneo la Makongoro wilayani Ilemela wakati mhudumu huyo Bernadetha Alfred (25) alipofungua kifurushi cha mzigo alichodhani kimesahaulika kwenye eneo hilo, kabla ya kumlipukia. 
Kwa mujibu wa Katibu wa Dayosisi hiyo, Mollel Rogart, kifurushi hicho kilichokuwa kwenye mfuko mweusi wa nailoni, kilikuwa juu ya kreti (tupu) za soda, karibu na eneo la kulia chakula lililopo katika nyumba hiyo. 
hili ndilo kanisa ambalo Bomu hilo lilipuka katika moja ya maeneo ya Jengo hilo
“Ule mfuko ulikaa pale siku tatu ndiyo usiku huo mhudumu wetu akakichukua kukiangalia akidhani ni mzigo wa mtu umesahaulika.” Alieleza Katibu huyo na kudai kuwa kifurushi hicho kilimlipukia mara tu alipokifungua na kujeruhi vibaya katika sehemu mbalimbali za mwili.  
“Bernadetha kajeruhiwa sehemu mbalimbali za mwili ikiwemo miguuni na usoni na siwezi kusema kwamba chanzo cha mlipuko huo ni mambo ya kidini japo ulinzi wetu haukuwa mkali kiasi cha kudhibiti watu walioingia na vitu.” Alisema

Kamanda wa polisi mkoani Mwanza, Valentino Mlowola akithibitisha tukio hilo, alisema kwamba uchunguzi wa awali uliofanywa na kikosi maalum kutoka Dar es salaam umebaini kuwa bomu hilo limetengenezwa kienyeji.

“Bado tunaendelea na uchunguzi wa tukio hilo ili tubaini ni nani kafanya ili kama ni mtu au kikundi kimehusika tuchukue hatua haraka. Natoa wito kwa wananchi kutochukua vitu ambavyo hawa uhakika navyo, wanapoona vitu vya aina hiyo, watoe taarifa kwetu.” Alisema Kamanda Mulowola.

Mlowola alieleza kuwa, Bernadetha aliyejeruhiwa vibaya katika sehemu mbalimbali za mwili, alikimbizwa katika Hospitali ya rufaa ya Bugando ambako anaendelea na matibabu.

Kamanda huyo alieleza kwamba, mabomu (yakiwemo ya kienyeji) yako katika mifumo mbalimbali hivyo wananchi hususan wahudumu wa sehemu za mikusanyiko wawe na tahadhari na vitu vinavyoonekana kusahaulika na wasisite kuwajulisha polisi vinapoonekana hivyo.

Mlipuko huo uliozusha hofu kwa waumini mbalimbali wakiwemo wa Kanisa hilo, umetokea ikiwa ni wiki moja baada ya maadhimisho ya ‘Huduma ya Mtoto’ kwa makanisa mbalimbali ya Kikristu jijini hapa yaliyofanyika kwenye kanisa hilo, yakitanguliwa na maandamano kutoka uwanja wa furahisha hadi KKKT
.
 
                                        Chanzo: Mjap inc

Comments