BWANA MUNGU NI MTETEZI ALIYE HAI.

Na Frank Philip


“Mbona BWANA anatuleta mpaka nchi hii ili tuanguke kwa upanga? Wake zetu na watoto wetu watakuwa mateka; je! Si afadhali turudi Misri? Wakaambiana, Na tumweke mtu mmoja awe akida, tukarudi Misri. Ndipo Musa na Haruni wakaanguka kifudifudi mbele ya mkutano wa kusanyiko la wana wa Israeli. Na Yoshua mwana wa Nuni, na Kalebu mwana wa Yefune, waliokuwa miongoni mwao walioipeleleza nchi, wakararua nguo zao; wakanena na mkutano wote wa wana wa Israeli wakasema, Nchi ile tuliyopita kati yake ili kuipeleleza, ni nchi njema mno ya ajabu. Ikiwa BWANA anatufurahia, atatuingiza katika nchi hii atupe iwe yetu, nayo ni nchi yenye wingi wa maziwa na asali. Lakini msimwasi BWANA, wala msiwaogope wale wenyeji wa nchi, maana wao ni chakula kwetu; uvuli uliokuwa juu yao umeondolewa, naye BWANA yu pamoja nasi; msiwaogope. Lakini mkutano wote wakaamuru wapigwe kwa mawe. Ndipo utukufu wa BWANA ukaonekana katika hema ya kukutania, mbele ya wana wa Israeli wote. BWANA akamwuliza Musa, Je! Watu hawa watanidharau hata lini? Wasiniamini hata lini? Nijapokuwa nimefanya ishara hizo zote kati yao.12Nitawapiga kwa tauni, na kuwaondolea urithi wao, nami nitakufanya wewe kuwa taifa kubwa, kisha yenye nguvu kuliko wao” (Hesabu 14:3-12).

Katika maisha ya kila siku, haijalishi wewe ni mwema kiasi gani au mtu wa haki kiasi gani, utakutana na watu watakao kupinga tu. Japo kuna kundi la watakao simama na wewe, na kukuelewa, lakini nakwambia lipo kundi, na si dogo, la watu ambao kila wakikutazama wanatamani wakuangamize mara moja! Hii hali inawakumba wote, wanaomjua Mungu na wasio mjua. Heri yao wamjuao Mungu, kwa maana Mungu kwao ni MTETEZI wao asiye shindwa.

Ninachofahamu ni kwamba, kila mtu duniani anamhitaji Mungu, ila watu tunatofautiana kwa KIASI cha kumhitaji Mungu. Kwa mtu yule ambaye Mungu wake ni mambo yote, kila saa atamtafakari yeye na njia zake, na kudumu katika maombi na kusoma Neno. Kinacholeta tofauti baina ya watu na watu kwa habari za Mungu, ni UHUSIANO baina ya mtu husika na Mungu wake. Kwa mfano, haiwezekani uishi nyumba moja na baba yako mzazi, halafu hamuongei! Kila ukiondoka nyumbani, au ukirudi, unampita tu hapo sebuleni kama hayupo. Ukitaka kuanzisha biashara, au ukitaka kufanya jambo lolote, unakurupuka tu bila kumshirikisha baba yako, japo anajua. Mara nyingine, unamkuta mtu huyu huyu anakamatana na kahaba huko, anakuja na kahaba lake nyumbani, wamekumbatiana na kahaba mbele za baba yake, na anapitiliza kuelekea chumbani; baba anaona live. Baba anaona, anaumia sana, ila anakaa kimya. Ok. Wakati wa kulala unafika, mtu hata humwambii baba yake “good night dad”! anakatiza mbele za baba yake hapo kimya kimya, anajitupa kitandani na kuuchapa usingizi wake. Anamwacha Baba yake macho akikesha kumlinda kwa maana “hasinzii wala halali, Yeye ni Mlinzi wa Israel”. Hii hali inaonesha UHUSIANO fulani. Kwa mtu wa namna hii, kwa kweli “kiasi cha kumhitaji baba yake” ni kidogo sana, hata kama ANAKIRI kwamba anamhitaji; matendo yake yanasema kinyume na maneno yake. Hivi ndivyo ilivyo kwa Mungu wetu. Watu wengi sana wanamhitaji Mungu wakisikia vita, ugonjwa, njaa, uhitaji, nk. Lakini wanamtumia kama DAWA tu; ugonjwa ukitulia, dawa inawekwa pembeni.

Nitakwambia habari za Musa, Yoshua na Kalebu. Wakati huu Wana wa Israel wanapita jangwani, Musa ni Mzee na Yoshua na Kalebu ni vijana tu. Lakini tangu utoto wao wamejifunza njia za Mungu kupitia Musa, kiongozi wao wa kiroho. Walipoenda kuipeleleza nchi, Yoshua na Kalebu, waliona MAJITU kama wenzao walivyoona. Pamoja na UDOGO wao, walimjua MTETEZI wao ana NGUVU kiasi gani. Wakati UMATI mzima wa wana na Isarael umetaharuki, watu wanalia usiku kucha, hofu imetanda kila kona, japo hawajaona MAJITU bado, ni hadithi tu! Ila wame-panic, amani imetoweka hata kabla MAJITU hayajaja. Hawa vijana wawili, Yoshua na Kalebu, wanawatuliza na kuwaeleza jinsi “nchi ni ya ajabu kwa uzuri wake”! bila kuzingatia hata kutaja tena MAJITU, kwa maana kwao MAJITU sio kitu cha kutisha. Watu wakakasirika na kutaka kuwaangamiza kwa kuwatwanga mawe hadi wafe. Ona jambo hili, “Lakini mkutano wote wakaamuru wapigwe kwa mawe. Ndipo utukufu wa BWANA ukaonekana katika hema ya kukutania, mbele ya wana wa Israeli wote”. Ghafla! Kabla hawajanyanyua jiwe, Bwana wa Majeshi akashuka mwenyewe KUWATETEA vijana wale! Ghafla tu, hata Yoshua na Kalebu hawakupata muda wa kuomba msamaha, wala kukemea kwa Jina la Yesu, Bwana wa Majeshi huyu hapa kaja kuwatetea! Hebu fikiri umati wa watu zaidi ya Milioni moja unainuaka kinyume nawe kwa mara moja, sembuse hako ka-boss kako kanakokunyanyasa hadi unamtenda Mungu dhambi kila siku kwa machozi! Kumbuka siku zote, ukijijengea UHUSIANO mzuri, na wa karibu na Mungu, unakuwa MBONI ya jicho la Mungu. Hakuna mahali utasikia mkono unaitwa uje kusaidia wakati kitu kinataka “kugusa” jicho, ghafla! Mkono huja kuingilia kati, mara moja tu na kwa speed ya ajabu, hicho kitu kinachotaka kugusa jicho “kinaona cha mtema kuni”. Hivyo ndivyo ilivyo jana, leo na hata milele. Mungu huwatetea watu wake, na hatakaa kimya.

Nitakupa ushuhuda wa kijana mmoja wa kitanzania. Huyu kijana ni mcha Mungu na ni mtumishi wa umma. Katika ofisi yake kuna wakuu ambao wanafanya ufisadi. Siku moja hawa wakuu wakapanga mbinu za kufanya ubadhirifu wa pesa ya umma. Wakaona haiwezekani kumshirikisha huyu kijana, lakini kwa nafasi yake lazima wamtumie ili aandike barua fulani, ili baadae wamtumie huyu kijana kama yeye vile alihusika katika mchakato toka mwanzo. Kijana huyu bila kujua, akaandika barua kama ailvyotakiwa na wakuu zake, akatoa maelezo juu ya hilo jambo, kumbe! Kulikuwa na mtego wa adui.

Mchakato ukaendelea na ulikuwa unahusisha pesa nyingi za kigeni. Baadae kijana akagundua kwamba alitumika katika mchezo mchafu. Kilichotokea alisema ukweli, kwamba aliandika sio kuunga mkono hilo jambo ila alitoa tu maoni ya ujumla kama mtaalamu katika eneo hilo. Kukatokea vita mbaya sana kati ya kijana huyu na wakuu wake pale ofisini. Kwa mara moja, huyu mkuu mmoja akamwambia kijana, “nitakufukuza kazi”, na mwingine akajitahidi kufanya maisha ya kijana kuwa magumu, hata kudhulumu malipo yake ya halali. Huyu kijana “hakuwalaani wala kuwaombea mabaya kwa Mungu, japo aliweza kufanya hivyo”. Haikupita muda, wakati lile jambo limefikia kilele chake, malipo yanatakiwa kufanyika, mmoja wa wale wakuu zake, akapumzika pamoja na baba zake. Amekuja kazini asubuhi kama kawaida, kumbe jioni ni marehemu. Huyu mkuu mwingine aliyebaki, mkataba wake wa kazi ukakwama, na akaondoka ofisi ile bila kutarajia. Wote wawili hawakuona hayo malipo yakifanyika wakiwa katika nafasi zao kwenye ile ofisi. Hadi kesho, yule kijana ni mfanyakazi katika ofisi ile na anaendelea kuchapa Injili kama kawaida. Tazama, kwa ushuhuda huu, kijana “hakujua kwamba Mungu alikuwa anamtetea muda wote huo”! Alipata ufunuo wa jambo hili baadae baada ya mambo yote kupita! Mungu alimfungua kuona jambo alilofanya kwa ajili yake, naye akamshukuru Mungu wake, na maisha yakaendelea.

Kama unamjua Mungu wako, uwe na amani siku zote. Huna haja ya kugombana na watu na kuwalaani. Wakijifanya MAJITU mbele zako, liitie Jina la Bwana wa Majeshi, kisha kaa kimya. Vita ni vya Bwana. Siku zote jua MAJITU yamewekwa kupima IMANI yako kwa Mungu, na kama MLANGO ya kukufungulia Baraka nyingine za juu zaidi. Angalia neno hili la vijana Yoshua na Kalebu, “Lakini msimwasi BWANA, wala msiwaogope wale wenyeji wa nchi, maana wao ni chakula kwetu; uvuli uliokuwa juu yao umeondolewa, naye BWANA yu pamoja nasi; msiwaogope”. Jua Mtetezi wako anaishi LEO. Chunga uhusiano wako na Mungu. Asali na Maziwa ni vyako milele, na MAJITU ni chakula laini.

Frank Philip.

Comments