JARIBU KAMA NGAZI

Na Frank Philip


"Ndipo malaika wa BWANA akamwita kutoka mbinguni, akasema, Ibrahimu! Ibrahimu! Naye akasema, Mimi hapa. Akasema, Usimnyoshee kijana mkono wako, wala usimtendee neno; kwa maana sasa ninajua ya kuwa unamcha Mungu, iwapo hukunizuilia mwanao, mwanao wa pekee" (Mwanzo 22:11,12).

Imani huja kwa kusikia, na kusikia huja kwa Neno la Kristo. Imani katika Kristo inajengwa kwa kusikia Neno la Kristo. Kusikia inamaana ya kusikia sauti ya Kristo katika Neno, katika moyo wako au kupitia watu wengine na kisha KUTII. Kusikia ni zaidi ya kupokea sauti masikioni mwako; ni hali ya kupokea kwa KUTII kwa MATENDO (Yakobo 2:14-19). Kwa mfano, ukimtuma mtoto kufanya jambo, kisha asifanye, basi utasema "huyu mtoto hasikii". Kusikia huku haimaanishi kwamba mtoto ni KIZIWI au hajui alichaogizwa, hapana, anaweza kupokea sauti na maelekezo, ila hatendi, basi tunasema mtoto HASIKII.

Imani yetu katika Kristo haishii tu katika kupokea Neno katika mafundisho na mahubiri, bali katika KUTII kutenda sawa na HILO Neno; ndipo tunasema mtu amekuwa "mtendaji wa Neno".

Kuna Tofauti moja kubwa kati wanadamu na Ibilisi; Wote wanasikia Neno, na wote wanatenda Neno, ila kwa Wanadamu tunapewa thawabu au kupanda CHEO/BARAKA kila tukitii. Sasa najua utaniuliza Ibilisi anatenda Neno wapi, kumbuka mfano wa Ayubu. Angalia hapa, "BWANA akamwambia Shetani, Tazama, yote aliyo nayo yamo katika uwezo wako; lakini usinyoshe mkono wako juu yake yeye mwenyewe. Basi Shetani akatoka mbele za uso wa BWANA" (Ayubu 1:12). Mungu amliruhusu Ibilisi kufanya alichofanya kwa Ayubu kwa Neno alilotamka. Katika hili Neno, Mungu alimpa Ibilisi RUHUSA na MIPAKA, na Ibilisi alitenda kama alivyowekewa mipaka na Mungu. Ibilisi hakufanya zaidi ya kiwango alichopimiwa. Kinachotokea kwa MJARIBIWA (yaani mtu), ni KUONGEZWA/KUBARIKIWA kama atashinda kwa HALALI na kwa MJARIBU (Ibilisi) hakuna baraka; yeye ni mlaaniwa hadi mwisho.

Jaribu sio kitu chepesi au cha kuvutia sana. Mara nyingi jaribu huja kama TATIZO, SHIDA au MATESO fulani. Kila jaribu lijapo, njia ya kufaulu KIMUNGU huwa kama mlima wa kupanda, na iko gizani; njia ni ya kutafuta; bali njia ya KIBINADAMU/IBILISI huwa ni ya mteremko na iko karibu na wazi sana (ndio maana halisi ya jaribu, inakuwa vyepesi zaidi kufeli kuliko kufaulu). Jambo la kuchunga ni kuepuka kulalamika au kumlaumu Mungu upitapo majaribuni. Kila jaribu huja kwa nia njema ya kukuinua sio kukuangusha. Hebu angalia hapa, "Wala msinung’unike, kama wengine wao walivyonung’unika, wakaharibiwa na mharabu. Basi mambo hayo yaliwapata wao kwa jinsi ya mifano, yakaandikwa ili kutuonya sisi, tuliofikiliwa na miisho ya zamani. Kwa hiyo anayejidhania kuwa amesimama na aangalie asianguke. Jaribu halikuwapata ninyi, isipokuwa lililo kawaida ya wanadamu; ila Mungu ni mwaminifu; ambaye hatawaacha mjaribiwe kupita mwezavyo; lakini pamoja na lile jaribu atafanya na mlango wa kutokea, ili mweze kustahimili" (1Kor. 10:10-13).

Mara nyingi sana watu wamejifariji kwa sababu wanajua mistari mingi ya Biblia kwa kichwa, naam, hata kufundishwa wengine. Nisikilize, hilo Neno halijawa imani kwako hadi UPIMWE (ujaribiwe) kwa namna fulani ili KUTHIBITISHA kama kweli unaamini. Kwa mfano, Ibrahim alimwamini Mungu, na Mungu alijua kwamba Ibrahim anamwamini, lakini ilimchukua Mungu hatua ya KUPIMA kwa namna ambayo Ibrahim angefanya jambo kwa matendo ili KUTHIBITISHA ya kwamba kweli anaamini.

Ukiangalia Mwanzo 22: 1-11, utaona Ibrahim ANASIKIA sauti ya Mungu (anapokea maelezo na kutii kwa kutenda alichagizwa). Ukiangalia Mwanzo 22:12, utaona Mungu anathibitisha imani ya Ibrahim, Mungu "Akasema, Usimnyoshee kijana mkono wako, wala usimtendee neno; kwa maana sasa ninajua ya kuwa unamcha Mungu, iwapo hukunizuilia mwanao, mwanao wa pekee." Mungu anasema SASA NIMEJUA! Inamaana baada ya matendo ya Ibrahim, SASA Mungu amejua. Ukiangalia Mwanzo 22:15-18, utaona Ibrahim anapanda cheo baada ya kufaulu MTIHANI/JARIBU. Angalia hapa, "Malaika wa BWANA akamwita Ibrahimu mara ya pili kutoka mbinguni akasema, Nimeapa kwa nafsi yangu asema BWANA, kwa kuwa umetenda neno hili, wala hukunizuilia mwanao, mwanao wa pekee, katika kubariki nitakubariki, na katika kuzidisha nitauzidisha uzao wako kama nyota za mbinguni, na kama mchanga ulioko pwani; na uzao wako utamiliki mlango wa adui zao; na katika uzao wako mataifa yote ya dunia watajibarikia; kwa sababu umetii sauti yangu." (Mwanzo 22:15-18)

Kumbuka ilimgharimu Ibrahim, kutembea na kijana mwendo wa siku 3, wanatembea tu. Muda wa kujaribuwa mara zote huwa sio MFUPI hata kama ni saa/siku chache tu. Kwa muda huo utakuwa UNAWAZA na kufanya maamuzi mengi ndani ya MOYO wako. Hata kama husemi na mtu; Mungu anachunguza mioyo, Anasikia unachowaza wakati unapita majaribuni. Hapo napo unapimwa jinsi UMWAZIAVYO Mungu katika kujaribiwa kwako. Ndio maana Mungu alijua kwamba Ayubu "HAKUMWAZIA KWA UPUMBAVU". Mungu alijuaje kama ilikuwa ni mawazo tu? Kwa lugha nyingine ushindi mkamilifu katika majaribu ni kuweza KUWAZA vema na KUTENDA vyema ikiwemo na MANENO yetu.

Mungu atusaidie saa ya kujaribiwa kwetu kwa sababu JARIBU huja kama NGAZI ya kutupandisha ngazi nyingine; IMANI (kusikia na kutii Neno) hutusaidia kukupa maelekezo ya kutenda ikupasavyo na kukumulikia njia ya KUPANDIA.

Frank Philip.

Comments