KISINGIZIO

Na Frank Philip
“Mwanamke alipoona ya kuwa ule mti wafaa kwa chakula, wapendeza macho, nao ni mti wa kutamanika kwa maarifa, basi alitwaa katika matunda yake akala, akampa na mumewe, naye akala [………] Adamu akasema, Huyo mwanamke uliyenipa awe pamoja nami ndiye aliyenipa matunda ya mti huo, nikala.BWANA Mungu akamwambia mwanamke, Nini hili ulilolifanya? Mwanamke akasema, Nyoka alinidanganya, nikala” (Mwanzo 3: 6, 12, 13).

Dhambi ni hali ya KUAMUA kufanya au kuacha kufanya jambo fulani kinyume na maagizo ya Mungu. Kwa namna nyingine, tunaweza kusema dhambi ni kuasi maagizo ya Mungu.

Ni kweli tunaishi duniani ambapo kuna changamoto nyingi; ni kweli hatuwezi kuishi peke yetu bila watu wengine; ni kweli hatuwezi kuishi bila kupata mahitaji ya muhimu kwa jinsi ya mwilini, lakini nakwambia, kupitia watu wengine na mahitaji ya mwilini, watu wengi sana wamemtenda Mungu dhambi na kisha KUSINGIZIA hao watu na vitu vilivyohusika katika kutenda dhambi fulani.

Kutenda dhambi ni swala la “mtu na Mungu wake”, bila kujali watu wengine wamefanya nini kwako. Kumbuka ukienda uwanjani bila mshindani wako hata kama utakimbia sana, huwezi kuitwa mshindi kwa sababu hapakuwa na mtu wa kushindana naye. Kitu kinachotufanya tuwe washindi ni ULIMWENGU na mambo yake. Bwana wetu Yesu akijua hayo, akasema “Ulimwenguni mnayo dhiki; lakini jipeni moyo; mimi nimeushinda ulimwengu” (Yohana 16: 33b). Kuna taji ya watakaoshinda, lakini nakwambia bila WATU na MAHITAJI ya mwilini hatuna jambo la kutupima kiwango cha KUSHINDA au KUSHINDWA kwetu. Ucha Mungu wetu unapimwa kwa jinsi tunavyohusiana na watu wengine, na jinsi tunavyo shughulika na mahitaji yetu ya mwilini.

Mara nyingi tumejaribiwa na tamaa zetu wenyewe na kutenda dhambi, kisha tukahamisha lawama, kutoka kwetu kwenda kwa mtu mwingine au vitu vingine. Kwa mfano, utakuta mtu amekamatwa na dhambi fulani, na hapendi ile hali, ila kila saa akitaka kujifariji utamsikia “nisipokunywa siwezi kulala”, kisingizio ni usingizi; “huyu mama/baba ananichanganya sana, sasa nakunywa kupoteza mawazo”, kisingizio ni mke/mumewe na usingizi; “kama isingekuwa huyu baba/mama kunichanganya nisingekuwa mzinzi”, kisingizio ni mume/mkewe; “kila mtu anaiba, kwanza mshahara hautoshi, nitaishije na familia yangu?”, kisingizio ni ugumu wa maisha na hali halisi, nk. Kuna sababu nyingi, lakini nakwambia Mungu akiangalia mtu, anaona UASI hata kama kuna watu wengine au vitu vimehusika.

Ni kweli kuna watu na vitu vimehusika katika dhambi fulani, lakini kila kimoja kitapokea hukumu yake binafsi. Hawa alipomsikiliza Ibilisi na kumwasi Mungu, alikuwa na sababu nyingi za kujitetea: kwanza, huyu baba hakuwepo wakati anajaribiwa na nyoka. Yamkini angejitetea na kusema “Mungu, nimeyatenda haya kwa sababu mume wangu alikuwa mbali, nami nikadanganywa”; Pili, yamkini matunda ya miti mingine waliyoruhusiwa kula yalikuwa “sio ya kuvutia na kutamanika sana”, Hawa alipolinganisha na matunda ya “mti waliokatazwa kula”, akaona jambo hili, “Mwanamke alipoona ya kuwa ule mti wafaa kwa chakula, wapendeza macho, nao ni mti wa kutamanika kwa maarifa, basi alitwaa katika matunda yake akala, akampa na mumewe, naye akala”. Haijalishi kuna sababu ngapi za MSINGI kabisa, uasi ni uasi tu, hakuna jina jingine. Mungu anapima watu katika UHITAJI wao pia, ndio maana kila siku mtu atahitaji kitu, na akipata hicho kitu unauona mkono wa Mungu na hata kujisikia kumshukuru Mungu.


Hebu angalia hili jambo kwa Paulo “Naye akaniambia, Neema yangu yakutosha; maana uweza wangu hutimilika katika udhaifu. Basi nitajisifia udhaifu wangu kwa furaha nyingi, ili uweza wa Kristo ukae juu yangu. Kwa hiyo napendezwa na udhaifu, na ufidhuli, na misiba, na adha, na shida, kwa ajili ya Kristo. Maana niwapo dhaifu ndipo nilipo na nguvu” (2Kor. 12:9,10). Wakati Paulo anapambana kwenye huduma, aligundua sio kila siku atapata kila kitu anachohitaji kwa jinsi ya mwilini. Alifika mahali pa kupigwa, kuvunjiwa heshima yake, kutukanwa, kufungwa jela, nk. naam, hata udhaifu katika mwili wake. Haya ni mambo ambayo yanasababishwa na watu wengine, naam, hata mwilini mwake ulihitaji uponyaji! Lakini bado anapambana na sio rahisi. Ona jambo hili, “Kwa hiyo napendezwa na udhaifu, na ufidhuli, na misiba, na adha, na shida, kwa ajili ya Kristo. Maana niwapo dhaifu ndipo nilipo na nguvu”. Matatizo yalipokuja: udhaifu, ufidhuli, misiba, adha, shida, nk. havikumvunja moyo Paulo. Hakutenda dhambi kwa kisingizio cha hayo yote! Alisema neno hili “Neema yako yatosha Bwana”, na kusonga mbele. Akiichuchumilia mede ya dhawabu aliyoandaliwa siku ya mwisho, huku akiupiga mwendo na vita vizuri vya imani, naam, akaumaliza mwendo kwa ushindi. Usidhani kwamba Paulo alikuwa hakwazwi, ila ALICHAGUA kumtii Mungu katika hali zote. Hii ndio maana na KUSHINDA. Yaani kuweza kusimama katika KUSUDI la Mungu japo watu na vitu vinakuwekea vikwazo mbali mbali.

Sasa angalia tena habari za Eden. Hawa alipojaribu kumsingizia nyoka (Ibilisi), haikumsaidia sana; Adamu alipojaribu kumtupia lawama mkewe, haikusaidia sana; ardhi iliyoshuhudia haya yote pia ililaaniwa! Unapofanya dhambi, hata kama uko peke yako, mara nyingi sana madhara ya ile dhambi yanasambaa kwa watu wengine na kuwaathiri kwa kiwango ambacho Mungu angekuonesha ungeshangaa sana. Ngoja nikupe mfano. Uzinzi hufanyika katika mwili, lakini madhara yake ni kwenye nafsi. “Mtu aziniye na mwanamke hana akili kabisa; Afanya jambo litakalomwangamiza nafsi yake (Mithali 6:32). Sasa watu wanadhani hatari ya uzinzi ni magonjwa na kufumaniwa. Nitakwambia kwa ufupi. Madhara yanayotokea katika nafsi ni makubwa kuliko unavyofikiri. Kwa mfano utakuta mume/mke anakuwa na vifungo nafsini mwake na kahaba fulani aliyezini naye. Ghafla! hali ya ndoa yake inaanza kuwa tete tangu siku ile amefanya uzinzi hadi ukombozi utakapopatikana. Ile hali ya moyo/nafsi yake itasababisha ugumu wa mawasiliano na maelewano ndani ya nyumba. Kunatokea hali ya kushindwa kwenda pamoja katika mipango yao ya kifamilia na kuvuruga kabisa mstakabali (future) wa familia nzima, nk. Madhara ni makubwa kuliko mtu alivyofikiri, na kufuta hayo madhara ni gharama kubwa kuliko mtu alivyofikiri pia, kumbe, ilikuwa dakika chache tu mtu alifaidi dhambi! Ona sasa, wamefika mahali wanashindwa kusimama katika kusudi la Mungu! Na huyu mzinzi kwa sababu ya uchungu wa moyo uliompeleka kuzini, anawanajisi wengine wengi. Angalia madhara haya, mtu anajikuta anasababisha na watu wengine kushindwa kusimama kwenye kusudi la Mungu kwa jinsi ambavyo anaenenda, kumbe ni ule uzinzi ulioharibu nafsi yake! Na sasa hawezi tena kusimama katika mambo ya Mungu, kunena vyema, kuwaza vyema, kushughulika na mambo ya wito wake, nk. Maisha yamebadilika.

Ukiona mtu kazi yake ni kurusha lawama kwa wengine juu ya hali yake ya kiroho, jua Ibilisi yuko kazini. Ule uasi mtu aliofanya utamsukuma kutafuta faraja ili ajione kwamba “hata hivyo hayuko peke yake”. Watu wa namna hii wamejikita sana katika kufuatilia “dhambi za watumishi na wana wa Mungu”, na wasikiapo mtu fulani kaanguka dhambini, kwao inakuwa kama faraja kwamba kumbe hayuko peke yake. Kwa watu wengine walioko sawa na Mungu wao, wakisikia mwana wa Mungu kaanguka dhambini, kinakuja kilio na kukosa raha; wengine wanajikuta wakiingia kwenye maombi magumu sana kuwaombea hao watumishi walioanguka, kwa sababu wanasikia maumivu kama vile kiungo kimoja cha mwili kikipata shida ambavyo mwili mzima unapata shida. Ukiona wewe unafarijika usikaipo mtu fulani mashuhuri kaanguka, jiulize kwamba wewe ni kiungo cha mwili upi? Na wengine wamefika mahali wamesema “potelea mbali, maanadam nateswa, nitaendelea na uasi wangu” au “mbona watumishi wa Mungu kabisa wanafanya hii kitu, sasa mimi niliye mdogo mbona sio shida sana?” Watu wamejitia moyo, na kuwatupia wengine lawama, kumbe! Ibilisi yuko kazini kuwaangamiza bila wao kujua. Nakupa shauri, mrudie Bwana leo, lengo la Ibilisi ni kukuangamiza kabisa. Itakufaa nini watu kukusifu na kukupa jina jema huku unajua jina lako la uovu? Basi, nenda mbele za Bwana na jina lako la siri, futa hilo jina kwa Damu ya Yesu, geuka na Bwana atakurehemu.

Frank Philip.

Comments