KUWEKWA ALAMA YA DAMU YA MWANAKONDOO WA MUNGU ALIYE HAI *sehemu ya mwisho *

mtumishi wa MUNGU Gasper Madumla


Bwana Yesu asifiwe....
Haleluya...

Tunasoma ;
" Kisha akamsongeza kondoo mume wa pili, huyo kondoo wa kuwaweka wakfu; na Haruni na wanawe wakaweka mikono yao kichwani mwa huyo kondoo.
Kisha akamchinja; na Musa akatwaa katika damu yake, na kuitia katika ncha ya sikio la kuume la Haruni, na katika chanda chake cha gumba cha mkono wake wa kuume, na katika kidole cha gumba cha guu lake la kuume. " Walawi 8:22-23

Andiko hilo hapo juu ndilo andiko letu la msingi wa fundisho hili zuri mahali hapa.Leo ikiwa ni siku ya tatu na ni siku ya mwisho wa fundisho hili. Ninakukaribisha rasmi katika tafakari ya leo fupi,kisha tuombe pamoja mimi na wewe kwa njia ya simu yangu iliyopo hapo chini.Damu ya Yesu Kristo i hai,halisi tangu enzi hata enzi na hata sasa,kwa njia ya damu yake Bwana,siku ya leo tutakausha na kusambaratisha kila aina ya ugonjwa na udhaifu wowote ule.

Haleluya....
Nasema haleluya...

Sasa angalia hapa; (Walawi 8:22-23)
Biblia inasema Haruni na wanawe wakaweka mikono yao kichwani mwa kondoo,wakimaanisha kuhamisha dhambi na makosa yao kwa kupeleka kwa huyo kondoo.Hapo awali walitumia damu ya fahari na wanyama katika kujitakasa na kuleta upatanisho baina yao na Mungu Baba.
Na kabla ya kuitoa dhabihu hiyo ya mnyama,walikuwa wakiweka mikono yao kichwani mwa mnyama aliyekusudiwa kama ishara ya kuhamisha dhambi zao na kuzipeleka juu ya kichwa cha huyo mnyama.

Walikuwa wakifanya hivi kwa sababu ili makosa ya dhambi yaondolewe;
basi ilihitajika dhabihu ya damu itolewe.Hivyo badala ya kujitoa maisha yao walitoa maisha ya mnyama akiwawakilisha.
Kile kilicholengwa kwa huyo kondoo wa pili wa kuwaweka wakfu akina Haruni na wanawe,ilikuwa ni DAMU.Ili Damu ya kondoo huyo ipatikane ilihitajika kondoo kufanyika dhabihu kwa kuutoa uhai wake.

Alikadhalika Yesu Kristo naye alifanyika dhabihu ya dhambi kwa ajili yetu ingawa Yeye mwenyewe hakutenda dhambi maana tunasoma;

" Kristo alitukomboa katika laana ya torati, kwa kuwa alifanywa laana kwa ajili yetu; maana imeandikwa, Amelaaniwa kila mtu aangikwaye juu ya mti; " Wagalatia 3:13

Ili wewe na mimi tukombolewe ilihitajika dhabihu ya dhambi.
Yesu Kristo akafanyika dhabihu ili autoe uhai wake kwa ajili yetu sote;
Sasa;
Maovu na makosa yako na yangu pia ndio yalimpeleka Bwana Yesu pale msalabani na kufanyika laana ingawa hakutenda dhambi,maana mtu yeyote kwa kipindi kile anapoangikwa msalabani ni amefanyika laana kubwa sana ( Kumbukumbu 21:23).
Tulichorwa alama ya damu yake ndani yetu kwa njia ya msalaba wa Bwana Yesu,na hapo tukapokea haya yafuatayo ;

01.ONDOLEO LA DHAMBI.
Ondoleo la dhambi la uhakika lilifanyika pale msalabani kwa njia ya damu ya mwanakondoo wa Mungu aliye hai hata sasa.Biblia inatuambia ;
" Naye alituokoa katika nguvu za giza, akatuhamisha na kutuingiza katika ufalme wa Mwana wa pendo lake;
ambaye katika yeye tuna ukombozi, yaani, msamaha wa dhambi; " Wakolosai 1:13-14
Kwa njia yake tulipokea ondoleo la dhambi kwa mara ya kwanza ikiwa ishara ya ALAMA YA DAMU YAKE,tunasoma tena;

" kwa maana hii ndiyo damu yangu ya agano, imwagikayo kwa ajili ya wengi kwa ondoleo la dhambi. "Mathayo 26:28.

02. UWEZO WA KUSHINDA DHAMBI
Mwanadamu hakuwa na uwezo wa kuishinda dhambi nje ya kazi ya msalaba.Kwa uweza wa Damu ya Yesu Kristo pale msalabani tumepewa ushindi dhidi ya dhambi.
Damu ya fahari na mbuzi hazikuweza kabisa kuachilia ushindi dhidi ya dhambi.

Kikawaida kabisa,tunasema ya kwamba dhambi ni uchafu mbele za BWANA Mungu,nasi tulikuwa wachafu mbele za BWANA MUNGU,hivyo hatukuweza kushinda dhambi kwa sababu sisi wenyewe tulikuwa ni wachafu.Na palipo na dhambi pana uharibifu wa hali ya juu,

Maana;
Palipo na dhambi pana magonjwa,
Palipo na dhambi pana ufu,
Palipo na dhambi hapana kibali,
Palipo na dhambi pana umaskini,N.K
nguvu aliyoiachilia Bwana Yesu kwa njia ya damu yake pale msalabani ndio nguvu hiyo ya kushinda dhambi.

03.UREJESHO
Hapo awali sisi sote tulikuwa wafu sababu ya makosa na dhambi zetu ambazo kwa hizo zikauficha uso wa Mungu, hata tukashindwa kusikia neno la Bwana,maana imeandikwa;

" lakini maovu yenu yamewafarikisha ninyi na Mungu wenu, na dhambi zenu zimeuficha uso wake msiuone, hata hataki kusikia. "Isaya 59:2

Haleluya...

Ikumbukwe ;
Basi tena, kama kwa kosa moja watu wote walihukumiwa adhabu, kadhalika kwa tendo moja la haki watu wote walihesabiwa haki yenye uzima.
Kwa sababu kama kwa kuasi kwake mtu mmoja watu wengi waliingizwa katika hali ya wenye dhambi, kadhalika kwa kutii kwake mmoja watu wengi wameingizwa katika hali ya wenye haki. " ( Warumi 5:18-19)

Hivyo sote tukaingizwa kwenye dhambi, dhambi ilitutenga mbali na Mungu.
Hata hivyo sisi hatukuwa na Mungu bali tulikuwa na miungu na kuwa machukizo mbele ya BWANA Mungu.Hapo sasa tukawa mbali sana na uso wa Mungu.

Yesu akaja akatuleta kwa Mungu wa kweli,tena akatuleta karibu kwa njia ya msalaba wa Bwana,tukachorwa kama mali ya Bwana Mungu kwamba shetani hana nafasi kabisa kabisa ndani yetu;

" Lakini sasa, katika Kristo Yesu, ninyi mliokuwa mbali hapo kwanza mmekuwa karibu kwa damu yake Kristo.
Kwa maana yeye ndiye amani yetu, aliyetufanya sisi sote tuliokuwa wawili kuwa mmoja; akakibomoa kiambaza cha kati kilichotutenga.
Naye akiisha kuuondoa ule uadui kwa mwili wake; ndiyo sheria ya amri zilizo katika maagizo; ili afanye hao wawili kuwa mtu mpya mmoja ndani ya nafsi yake; akafanya amani. " Waefeso 2:13-15

Haleluya....
Jina la Bwana Yesu lisifiwe sana....

Ule ukaribu wa Mungu na sisi uliopotea tangu Adamu,ukaribu wetu na Mungu Baba ulirejeshwa kwa njia damu ya Yesu Kristo.Mwanadamu wa kwanza alipofukuzwa bustanini sababu ya dhambi,Yesu Kristo akaturejesha kwa upya.

04. UKOMBOZI WA UHAKIKA.
Kwa njia ya damu ya msalaba sisi tu huru,tumekombolewa.
Bwana Yesu alihakikisha anatupa alama ya ukombozi,

" Naye alituokoa katika nguvu za giza, akatuhamisha na kutuingiza katika ufalme wa Mwana wa pendo lake; "Wakolosai 1:13

05. ULINZI
Mahali pale msalabani alipotuchovya kwa damu yake ya msalaba aihakikisha anaachilia ulinzi wa kweli dhidi kila aina ya nguvu za giza.
Alama ya damu ya mwanakondoo hututambulisha kwamba sisi hatupo tena upande wa shetani bali tu mali ya Bwana.( 1 Petro 1:18)

06. USHINDI NDANI YA DAMU YAKE BWANA.
Upo ushindi wa kipekee damuni mwa Yesu mwanakondoo wa Mungu aliye hai,maana imeandikwa;
" Nao wakamshinda kwa damu ya Mwana-Kondoo, na kwa neno la ushuhuda wao; ambao hawakupenda maisha yao hata kufa. " Ufunuo 12:11

07.UZIMA NDANI YA DAMU YA YESU.
Imeandikwa;
" Basi Yesu akawaambia, Amin, amin, nawaambieni, Msipoula mwili wake Mwana wa Adamu na kuinywa damu yake, hamna uzima ndani yenu. " Yohana 6:53

• Hayo yote ni baadhi ya mambo yapayikanayo ndani ya Damu ya Bwana Yesu.
• Nasema yapo mambo mengi sana yapatikanayo damuni mwa Yesu,lakini kwa uchache tumeyaangalia hayo.

Haleluya....

Siku ya leo,kila aina ya udhaifu uliopo mwilini mwetu,uwe ni magonjwa au mapepo yanapigwa kwa jina la Yesu Kristo.
Nami ninayaamuru yakutoke kwa jina Yesu Kristo wa Nazareti na kwa njia ya damu yake Yesu,damu inenayo mema kuliko damu ya Habiri.

Leo hii, akiwapo mchawi kati yetu ni lazima akimbie mbele yetu maana atakapo iona alama ya damu ya Bwana Yesu ndani yetu,ni lazima akimbie,sababu kila mkristo aliye ndani ya Yesu,ana alama ya damu yake kama ishara ya utambulisho kwamba u mali ya Bwana Mungu.

Bwana Yesu asifiwe....

Magonjwa yote si sehemu yako,
Udhaifu wote si sehemu yako,
Maana imeandikwa kwa kupigwa kwake Bwana Yesu sisi tumeponywa ( 1 Petro 2:24)
Sasa;
Chukua hatua tuombe pamoja siku ya leo juu ya kila udhaifu,juu ya kila magonjwa,tukayakemee kwa uweza wa jina la Yesu Kristo wa Nazareti nawe uwe huru kweli kweli.
Piga namba yangu hii hapa chini;
0655-111149

MWISHO.

UBARIKIWE.

Comments