MTETEZI WANGU YU HAI.


Na Frank Philip


"Lakini mimi najua ya kuwa Mteteaji wangu yu hai, Na ya kuwa hatimaye atasimama juu ya nchi. Na baada ya ngozi yangu kuharibiwa hivi,
Lakini, pasipokuwa na mwili wangu nitamwona Mungu; Nami nitamwona mimi nafsi yangu, Na macho yangu yatamtazama, wala si mwingine.
Mtima wangu unazimia ndani yangu!" (Ayubu 19:25-27).

Maneno haya sio mepesi. Ayubu anasema kwa kinywa chake baada ya kuona mambo yanaenda tofauti na matarajio yake. Alikuwa na mali nyingi, sasa hakuna tena hata moja; alikuwa na watoto 10, hakuna tena hata mmoja, wamekufa wote; alikuwa na heshima yake katika jamii, sasa watu wanamcheka kwa jinsi hali yake ilivyobadilika; alikuwa na afya yake nzuri, sasa mwili mzima umejaa majipu yenye kuwasha na maumivu makali; alikuwa na ndoa yake, ghafla! mke wake hasimami tana naye katika mapito yake, huyu mama anamshauri mambo magumu ya kumpoteza badala ya kumtia moyo na kumfariji. Mke wa Ayubu anaenda kinyume na Mungu wake na kumtaka Ayubu amkufuru Mungu afilie mbali! Mke wa Ayubu amefika mahali anaona "ni aheri huyu baba afe tu", hakuna mahali tunaona akimlilia Mungu ili amponye mume wake; mama amechoka na mume wake na sasa anaona aheri afe zake maisha yaendelee. KATIKA MAMBO YOTE, AYUBU HAKUTENDA DHAMBI, WALA KUMWAZI MUNGU KWA UPUMBAVU.

Usidhani ilikuwa rahisi, kila JAMBO na HALI zilikuwa sababu ya kutosha kabisa kwa Ayubu kusema "potelea mbali, kama hali ndio hii na huyu mama ananisaliti namna hii, potelea mbali, nitamtenda Mungu dhambi. Nimevumilia vya kutosha na Mungu anajua ni huyu mama amenisukuma kwenda kumkufuru Mungu sio mimi mwenyewe, kila mtu anajua huyu mama anavyonichanganya hapa. Siku zote nimemheshimu ila amenivunjia heshima yangu, na mimi natoka sasa". Ayubu aliweza kufanya hayo. Lakini ALICHAGUA kukaa na Mungu wake hata kama watu wote wememgeuka, ikiwemo na mkewe! Ayubu alisimama na Mungu tu.

Wakati mambo ya Ayubu yanakwenda vibaya kabisa, ndipo wanakuja marafiki zake. Wanamtaabisha badala ya kumvusha alipo chini majivuni. Ayubu anatizama nakutambua kwamba, kumbe! Mtetezi wake PEKEE ni Mungu wake. Pamoja na kwamba kila kitu kimeharibika, kila alichokipenda kimeporomoka kwa MKONO WA ADUI, hata sasa ATAMWONA Mungu wake kwa maana ni MTETEZI wake. Ayubu akavuka hapo. Palikuwa ni mahali pa gumu, lakini alimwona Mungu akimzidisha na kumwongeza maradufu.

Nisikilize vizuri, yamkini kuna mahali mambo yanatokea kinyume na maombi yako. Tofauti kabisa na matarajio hata na ukiri wako. Unaona dalili za kushindwa tu. Giza limeshuka na huoni mbele. Kila ukisikiliza husikii sauti za faraja kwa mtu yeyote; uliodhani wako amoja na wewe wamegeuka na kuanza kukusengenya. Wale waliokuwa msaada kwako wamekugeuzia kisogo. Kila ukijaribu kusema "sasa nitakaa kimya", bado unasikia sauti za Ibilisi akikuzomea mawazoni mwako. Nisikilize, Mungu hajakuacha. Tizama, Mungu wako atasimama juu ya nchi na kukushika na kukuvusha katika hali yako. Japo unaona giza, jua giza hallimfichi Mungu kitu. Japo unadhani uko peke yako, jua Mungu yuko karibu nawe kuliko pumzi yako; Mungu atakuvusha, naam, hata sasa UTASHINDA tena.

Frank Philip.

Comments