MUNGU AKIKUPA KAZI YAKE,ATAKUPA NA MAELEKEZO SAHIHI.

Imeandikwa;
" Mungu akamwambia Nuhu, Mwisho wa kila mwenye mwili umekuja mbele zangu; kwa sababu wameijaza dunia dhuluma, basi nitawaharibu pamoja na dunia.
Ujifanyie safina ya mti wa mvinje; fanya na vyumba ndani ya safina, ukaifunike ndani na nje kwa lami.

Hivi ndivyo utakavyoifanya; mikono mia tatu urefu wa safina, mikono hamsini upana wake, na mikono thelathini kwenda juu kwake. " Mwanzo 6:13-15
Haleluya....
Na Mtumishi Gasper Madumla
Nuhu anatumwa kazi na BWANA Mungu,akipewa maelekezo sahihi kabisa.
Kazi hii haikuwa rahisi hata kidogo maana ilihitajika usikivu wa hali ya juu. Usikivu wa neno la Mungu ni IMANI,Hivyo kwa lugha nyingine kazi hii anayotumwa Nuhu ilimuhitaji Nuhu awe na imani ya hali ya juu,

Sababu kile alichokuwa akiambiwa,kilikuwa ni hakika ya mambo yatarajiwayo,ni bayana na mambo yasioonekana.
" Basi imani ni kuwa na hakika ya mambo yatarajiwayo, ni bayana ya mambo yasiyoonekana. "Waebrania 11:1
Ninakuambia kwamba Nuhu alihitajika awe na IMANI sababu yale mambo aliyokuwa akiambiwa yalikuwa hayaonekani kwa macho haya ya damu na nyama,tazama ;
Safina aliyoambiwa aitengeneze ilikuwa kwa ajili ya kujiokoa na mvua kubwa,lakini kipindi kile hapakuwa na mvua wala dalili ya mvua. Hivyo ni kama vile Nuhu alionekana kana kwamba ni mtu asiye na akili,maana kipindi ambacho ni ukame yeye ndio anatengeneza Safina.
Yaani mfano wa haraka haraka,chukulia kwamba mpo kundi la watu fulani hivi katika maombi ya kuombea mvua inyeshe,kisha muongozaji maombi aseme kesho kutakuwa na mvua kubwa wakati nyakati hizo ni nyakati za ukame kweli kweli. Kisha mmoja wenu aje na mwamvuli siku ya kesho,maana aliamini neno la kiongozi wa maombi.
Ukweli ni kwamba wengine hawatakuja na miamvuli,na yamkini watamshangaa yule aliyekuja na mwamvuli.
Sasa,
Aliyekuja na mwamvuli wakati wa kiangazi ndie mwenye IMANI.
Mazingira ya mtu huyu,yanataka kufanana na Nuhu.

Haleluya...
Leo tunasoma kwamba Nuhu anapewa kazi ya kutengeneza safina,lakini Mungu anahakikisha anampa maelekezo yakinifu juu ya safina.
Mungu angeliweza kumwambia Nuhu atengeneze safina pasipo maelekezo yoyote,lakini Bwana Mungu hakufanya hivyo sababu ulikuwa sio mpango wake. Bwana Mungu anampa Nuhu maelekezo yote ya jinsi safina itakavyokuwa.

Kwa lugha nyingine ni kwamba safina ile,Bwana Mungu alishaiona,na kuijua kabla hata ya kutengenezwa, ndipo anampa maelekezo yote Nuhu aifanye jinsi ipasavyo.
Laiti kama Nuhu asingepewa vipimo na mahitaji yote,yamkini angetengeneza lakini isingelifanana na safina ile ya Mungu. Ona katika hilo andiko hapo juu,BWANA Mungu anampa na vipimo sahihi vya hilo safina.

Haleluya....
Bwana Yesu asifiwe sanaa...

• Mungu hawezi kukutuma kazi pasipo kukuelekeza kwa usahihi juu ya kazi hiyo.
• Maelekezo na vipimo vya kazi hiyo vipo tayari kwa yule aliyetumwa kuifanya kazi ya Mungu.

Hata tunapomuangalia Musa,tutagundua kwamba maisha yake ya utumishi yote yalikuwa yanaongozwa na maelekezo sahihi kwa kila kazi aliyopewa na Mungu,kuanzia kuitwa kwake katika utumishi hadi kuwaendea ndugu zake huko Misri.
Tazama tu hata pale alipowaendea ndugu zake huko Misri,BWANA Mungu hakumuacha aende peke yake,na ndio maana alihitaji USO WA BWANA uende pamoja naye,tena alizidi kuumpa maelekezo sahihi,
Napapenda pale alipoambiwa aitumie ile fimbo kugawanya bahari,nao wana wa Israeli wapite,
Tunasoma;

" Nawe inua fimbo yako, ukanyoshe mkono wako juu ya bahari, na kuigawanya; nao wana wa Israeli watapita kati ya bahari katika nchi kavu. " Kutoka 14:16
Haya nayo yalikuwa ni maelekezo makubwa sana.
Nasi tunahitaji sana kuyasikia maelekezo ya Roho mtakatifu kwa kazi ya Bwana tuzifanyazo,sababu wenyewe hatuwezi kufanya kwa akili zetu,maana si kazi yetu,bali ni kazi ya Bwana.
• Kama tukishindwa kuyasikia maelekezo ya Mungu kwa usahihi wake,basi kazi tuzifanyazo ni bure.

Unafikirije?
Kama Musa,Nuhu wasingeisikiza kwa makini sauti ya Bwana Mungu wangefaulu?

*Wengi tunafeli kwa kushindwa kuisikiza sauti ya Mungu.
Mfano mdogo tu ni huu;
Chukulia liwapo kundi la wanamaombi sehemu fulani,na kama vile ujuavyo kuwa maombi ni silaha katika ulimwengu wa roho na wa mwili pia,sasa watu hawa wanapoongozwa na kiongozi wa maombi waombee ombi fulani,mfano kiongozi anaweza sema " tuombee kwa kumsukuru Bwana Mungu tu "
Sasa hapo ndipo kazi inaanza:
Utakuta kila mmoja ameelekeza silaha yake juu,wengine kweli wataanza kushukuru kama kiongozi alivyosema,na wengine wataanza maombi ya kuvunja,kuteketeza na kuharibu kinyume na neno la kiongozi.

Watu hawa kama ukiwaona katika ulimwengu wa kiroho,utaona risasi zikipigwa bila mpangilio,maana nyingine zitapigwa juu,nyingine chini,nyingine zitapigwa pembeni, Yaani hawakuweza kulenga sehemu moja sababu ya KUTOKUISIKIZA KWA BIDII SAUTI YA BWANA n.k
Siku zote Bwana Mungu husema nasi kwa njia tofauti tofauti,akitutuma kazi na kutupa maelekezo sahihi.
• Kama ukifanya kazi ya Mungu pasipo maelekezo,kazi hiyo itakuwa ngumu.
• Ukiona huna maelekezo yoyote ujiulize,kwamba hiyo ni kazi ya Mungu aliyokutuma ? Au ni kazi yako mwenyewe uliyotumwa?

Ngoja tuangalie katika ujio wa Yesu Kristo akiwa Bwana na mwokozi wetu.
Mitume wote hawakufanya kazi yake Bwana,pasipo kuelekezwa namna ya kufanya, tazama hapa;

" Hata alipokuwa amekutana nao aliwaagiza wasitoke Yerusalemu, bali waingoje ahadi ya Baba, ambayo mlisikia habari zake kwangu;
Lakini mtapokea nguvu, akiisha kuwajilia juu yenu Roho Mtakatifu; nanyi mtakuwa mashahidi wangu katika Yerusalemu, na katika Uyahudi wote, na Samaria, na hata mwisho wa nchi. " Matendo 1:4&8

Mitume wanaambiwa wasikwende mahali popote pale wakifanya huduma,mpaka wapokee ahadi ya Roho mtakatifu. Haya ni maelekezo sahihii kabisa kabla ya kufanya hiduma.
Huduma ya kina Petro ilikuwa ni huduma yenye nguvu sana,udhihirisho wa kazi ya Roho mtakatifu ulionekana sababu,si wao walifanya bali Roho alikuwa kazini,kwanza kwa maelekezo sahihi.
• Leo hii,ipo shida katika huduma tuzifanyazo.
• Wengi tunapenda huduma pasipo kupenda kusikiza sauti ya maelekezo ya Roho mtakatifu.
• Mungu atusaidie sana, ndio maana huduma inakuwa ngumu sana,kiasi kwamba mpaka unajiuliza kwamba " hii ni kazi ya Mungu kweli?"
• Tunahitaji kusikia zaidi,kabla ya kufanya.

UBARIKIWE
Kwa huduma ya maombi na maombezi,tafadhali USISITE KUNIPIGIA SIMU YANGU;

0655111149.

Comments