NANI ANAUPENDA WOKOVU WA KIMASIKINI?

Na Mwl C. Mwakasege

“Nani anaupenda wokovu wa Ukristo wa kimaskini?” Ukiona mtu amefika hali ya kujiuliza swali la jinsi hii, ujue ana hali ngumu sana kiuchumi.

Hili swali nilijikuta najiuliza mwenyewe baada ya kuwa na hali ngumu sana kimaisha baada kuokoka. Kuna wakati fulani baada ya kuokoka mimi na mke wangu tulijikuta tumefika mahali pa kukosa hata dawa ya mswaki, nguo, viatu, na chakula kizuri. Licha ya shida hizi zote bado zilifuata zingine baada ya ndugu zetu wawili tuliokuwa tunawalipia masomo yao kufukuzwa na kurudi nyumbani kwa kukosa ada. Na waliambiwa wasirudi shuleni bila nusu ya ada!

Unadhani tulikuwa na furaha tena? Ingawa tulikuwa tunasema tumeokoka, na mtu akituambia ‘Bwana asifiwe’ tuliitika ‘Amina’ ndani ya mioyo yetu tulikuwa na vita vikali na maswali mengi.
  Ni vigumu kuieleza hali hiyo tuliyoipitia ilivyokuwa ngumu kwa maneno. Lakini utaelewa mtu mwenye familia anavyojisikia anapoona anakosa hata fedha za kuwanunulia mke na watoto wake chakula licha ya mavazi. Wakati huo tulikuwa na mtoto mmoja.

Hali ilivyozidi kuwa ngumu, ndivyo nilivyozidi kusongwa na mawazo. Ilifika wakati ambapo nilikuwa naona aibu hata kukaa sebuleni, maana niliogopa hata kuwaangalia wale vijana waliofukuzwa shule, nikijua kuwa wataniangalia kwa macho ya huruma ili niwape ada warudi shule. Lakini si kwamba nilikuwa siwahurumii, bali sikuwa na fedha za kuwapa.

Ningeanzaje kuwaambia kuwa sina fedha, wakati wanajua nafanya kazi, na pia waliona nilikuwa na fedha nyingi kabla sijaokoka? Jambo hili lilinifanya niwaze sana. Inakuwaje kabla sijaokoka nilikuwa na fedha nyingi na baada ya kuokoka najikuta nimefilisika? Ingawa ni kweli kwamba kabla ya kuokoka fedha zingine nilizipata kwa njia zilizo kinyume cha ukristo lakini nilikuwa nazo. Na baada ya kuokoka ilibidi niziache njia hizo – na matokeo yake nilijikuta nimefilisika.

Lakini nilikuwa nimesoma katika Hagai 2:8 kuwa fedha na dhahabu ni mali ya Mungu. Na pia nilijua kuwa vyote vya Mungu ni vyangu nikiwa ndani ya Kristo. Kwa hiyo ilikuwa vigumu kuelewa kwa nini Mungu aseme fedha ni mali yake, halafu mimi niliye mtoto wake nisiwe nazo.

Ningewezaje kusema wokovu ni mzuri wakati baada ya kuokoka nimejikuta sina fedha za kutosha kununua chakula, nguo, dawa ya mswaki na hata kukosa ada za watoto! Je ndivyo Mungu anavyotaka tuwe baada ya kuokoka?

Wakati huo ndipo nilipoelewa kwa nini wana wa Israeli waliyakumbuka masufuria ya nyama ya Misri, ingawa walikula nyama hizo wakiwa utumwani. Ni rahisi sana mtu aliyeokoka kurudia njia au maisha mabaya ya kutafuta fedha kwa njia zilizo kinyume cha ukristo anapokuta anabanwa na matatizo ya kiuchumi maishani mwake. Na hata wakati mwingine unakesha katika maombi ili kumlilia Mungu akupe chakula na mavazi unaona kama vile hasikii.

Nilipokuwa nasumbuliwa na hali hii ndipo nilipojikuta najiuliza mwenyewe; “ Nani anaupenda wokovu wa kimaskini?” Nilijikuta siupendi kabisa. Ni wokovu gani huu ambao haunisaidii hata kutunza familia yangu?

Siku moja nilimuuliza mke wangu; nikasema; “Je! wewe unaupenda wokovu wa kimaskini?”

Akajibu; “Hapa, siupendi!”

Nikasema; “Naona tuna mawazo yanayofanana. Kwa hiyo naona ni muhimu tumuulize Mungu katika maombi kwa nini tulipokuwa kwa shetani tulikuwa na fedha za kutosha, lakini baada ya kuokoka na kuja kwake tunajikuta hatuna fedha hata za kununulia vitu muhimu?”

Baada ya kukubaliana hayo, mimi na mke wangu tulianza kumwomba Mungu kwa mfululizo wa siku tatu juu ya jambo moja hilo hilo. Namshukuru Mungu kwa kunipa mke ambaye aliweza kusimama pamoja nami katika maombi juu ya jambo hili. Sijui ningekuwa na hali gani kama angelalamika. Namshukuru Mungu mke wangu hakulalamika bali ALIOMBA PAMOJA NAMI.

Mungu alitujibu maombi na akaanza kutufundisha mambo mengi ambayo mengine nawashirikisha katika ujumbe huu.

Tulijua hakika kuwa hayakuwa MAPENZI YA MUNGU tuwe na hali ngumu ya kimaisha namna hiyo – kukosa fedha za kutosha kununulia nguo, chakula na vitu vingine muhimu. Na baada ya kuyaweka katika matendo yale tuliyoambiwa na Bwana yaliyo katika neno lake, hali yetu ilibadilika. Na matatizo tuliyokuwa nayo wakati ule yakaisha. Tukaanza kuona furaha tena katika maisha haya ya wokovu.

Ni vizuri kujua kuwa Mungu wetu hapendi tuwe maskini. Wala hapendi wokovu wa kimaskini! Ndiyo maana alimtuma Mwana wake wa Pekee, Yesu Kristo kutukomboa.

Kwa kukumbusha tu, Yesu Kristo aliyafanya yafuatayo kwa kufa na kufufuka kwake:

"Yesu Kristo alifanyika dhambi kwa ajili yetu, ili sisi tuhesabiwe haki bure ndani yake ya kusimama tena mbele ya Mungu"
(2Wakorintho 5:21)

"Yesu Kristo aliuchukua udhaifu wetu, ili katika mambo yote tuzitegemee nguvu zake"(Mathayo 8:17; Wafilipi 4:13)
Yesu Kristo aliyachukua magonjwa yetu, ili tusitawaliwe na magonjwa tena na kwa kupigwa kwake tumepona (Isaya 53:4,5; Mathayo 8:17; 1 Petro 2:24)
Yesu Kristo aliyachukua masikitiko na huzuni zetu, ili tukae katika amani yake ipitayo fahamu zote (Isaya 53:34; Wafilipi 4:6,7)
Yesu Kristo alikuwa maskini kwa ajili yetu ingawa alikuwa tajiri, ili sisi tupate kuwa matajiri katika Yeye (2 Wakorintho 8:9)

Ndiyo maana matunga Zaburi 23 aliandika hivi:

“Bwana ndiye mchungaji wangu, SITAPUNGUKIWA NA KITU.Katika malisho ya majani mabichi hunilaza, kando ya maji ya utulivu huniongoza. Hunihuisha nafsi yangu; na kuniongoza katika njia za haki kwa ajili ya jina lake …. Hakika WEMA
NA FADHILI zitanifuata siku zote za maisha yangu; nami nitakaa nyumbani mwa Bwana milele”.

Ni rahisi sana kusema. “Bwana ndiye mchungaji wangu, SITAPUNGUKIWA NA KITU, lakini je! Ni kweli hujapungukiwa na kitu? Je! Zaburi hii ni ya kweli, au ni maneno mazuri tu ya kutungia nyimbo?

Lakini napenda kukutia moyo kuwa maneno haya ni ya kweli, ukikaa ndani ya Kristo hutapungukiwa na kitu. Ndiyo maana Mungu alimwambia Yoshua ya kuwa atii maagizo yake yote na kuyafanya HATAMPUNGUKIA WALA KUMUACHA (Yoshua 1:5)

Kwa kuwa maneno haya ni ya kweli, mbona basi wakristo wengi WAMEPUNGUKIWA NA VITU? Tatizo haliko kwa Mungu, bali kwetu sisi. Na tuwe watendaji wa neno na tutaona mafanikio.


WAJIBU WA WAKRISTO:
Ni wajibu wa wakristo (a) kusaidiana sisi wenyewe kiuchumi; na (b) Kuwasaidia kiuchumi watu wengine wasio wakristo. Kuna wakati fulani mtu mmoja alikuja kwangu kuomba ushauri.

Nikamuuliza. “Una tatizo gani linalokukabili?”

Akasema; “ Baada ya kuokoka ilibidi niache njia fulani fulani ambazo zilikuwa zinanisaidia kupata fedha kwa kuwa zilikuwa ni kinyume cha maadili ya kikristo. Lakini sasa naona napata shida, sina fedha za chakula, wala sijui kodi ya nyumba mwezi huu nitapata wapi. Licha ya hayo, wale niliowakopa fedha kufanyia biashara hizo nilizoziacha wananidai fedha zao. Hata naogopa kukutana nao. Hebu nisaidie mawazo, najua nimeokoka kweli, lakini NITAISHIJE KATIKA HALI HII?”

Unadhani swali lilikuwa jepesi kujibu? Si swala la kumwambia tuombe halafu umwache aende zake! Yeye anachotaka baada ya kuomba aone msaada unamjia. La sivyo maombi hayo yanakosa maana kwake.

Swali hili “Nitaishije katika hali hii?” Linawasumbua walio wakristo wengi siku hizi. Na umefika wakati wa kulijibu.

Ngoja nikuulize swali jingine. Unadhani mwanamke ambaye anafanya uasherati ili kupata fedha za kuwalishia watoto wake hajui kuwa uasherati ni dhambi? Nina uhakika anajua kwa kuwa kuna mwingine hata kama anafanya hayo hakosi kila jumapili kanisani, na wakati mwingine hutoa sadaka kwa fedha hiyo hiyo. Unadhani hajui kuwa uasherati ni dhambi? Unadhani hamwelewi mchungaji anaposema acheni dhambi? Unadhani haogopi magonjwa ya zinaa? Unadhani anapenda kufanya hivyo? Nina hakika walio wengi hawapendi kufanya hivyo. Lakini jambo linalomsumbua, akiacha uasherati atapata wapi fedha za kuwatunza watoto wake? Nina uhakika akijibiwa swali hili ni rahisi kuacha tabia hiyo chafu.

Wasichana wengi mashuleni wamejikuta wamebeba mimba na kuharibu usichana wao kwa kudanganywa na fedha wanazozihitaji kwa ajili ya kununulia mafuta ya kupaka, nguo, na kutengeneza mitindo ya nywele.

Vijana wengi wa kiume wamejikuta wamejiingiza katika biashara haramu kwa sababu ya kutaka utajiri wa haraka haraka.

Kwa sababu ya kutokujua la kufanya wakristo wengi wamepoteza ushuhuda wao kwa sababu ya matatizo ya kiuchumi.

Wakristo wenzetu walifanyaje? Tusome kitabu cha Matendo ya Mitume 4:32,34,35.

“Na jamii ya watu waliamini (Wakristo) walikuwa na MOYO MMOJA NA ROHO MOJA; wala hapana mmoja aliyesema ya kuwa kitu cho chote alicho nacho ni mali yake mwenyewe; bali walikuwa na VITU VYOTE SHIRIKA. WALA HAPAKUWA NA MTU MMOJA MIONGONI MWAO MWENYE MAHITAJI; kwa sababu watu wote waliokuwa na viwanja au nyumba waliviuza, wakaileta thamani ya vitu vile vilivyouzwa; wakaiweka miguuni pa mitume, kila mtu akagawiwa KWA KADRI YA ALIVYOHITAJI”


Utaona katika habari hii ya kuwa kwa sababu ya Ukarimu na kutokuwa na ubinafsi wakristo hao waliweza kupambana na tatizo la umaskini katikati yao. Ndiyo maana ikandikwa kuwa; “WALA HAPAKUWA NA MTU MMOJA MIONGONI MWAO MWENYE MAHITAJI”. Jina la Bwana libarikiwe!

Matokeo ya usharika namna hii ni haya; “Na mitume wakatoa ushuhuda wa kufufuka kwake Yesu kwa nguvu nyingi, na neema nyingi ikawa juu yao wote” (Matendo ya Mitume 4:33)

Je! Siku hizi hakuna wakristo wenye mahitaji kati yetu? Na tunafanya nini ili kuwasaidia? Je! Kuwaombea tu kunatosha? Je! Unashangaa kwa nini ushuhuda wa kufufuka kwake Yesu hautangazwi kwa nguvu na wakristo? Nadhani wakristo wengi wanatumia muda wao mwingi sana kujitafutia mahitaji yao kiasi ambacho muda unaobaki hautoshi kufanya kazi ya kushuhudia.

Wenzetu walisaidiana, na sisi tusaidiane. Wazazi mara nyingi huwa wanawasaidia vijana wao waliowaoza kuanza maisha mapya. Na fahamu kuwa wokovu ni maisha mapya. Tunawajibika sana kuwasaidia wale wanaookoka kiroho na kimwili kuanza maisha mapya ndani ya Kristo. Kwa kukosa msaada wa kiuchumi, wengi wamepoa na kurudi nyuma.

Niliwahi kushirikishwa ushuhuda mmoja ambao naamini utakusaidia kukuelewesha jambo hili ninalokuambia.

Kuna mtu mmoja aliokoka baada ya muda mrefu kuwa mganga wa kienyeji na mchawi. Baada ya kuokoka ilibidi aache uchawi na uganga wa kienyeji, shughuli hizi ndizo zilizokuwa zinamsaidia kupata fedha ya matumizi.

Baada ya kukaa miezi michache katika wokovu, bila ya kuwa na njia nyingine ya kupata fedha, ilibidi atumie akiba yote aliyokuwa nayo. Baada ya hiyo akiba kuisha akaanza kupata shida namna ya kuishi.

Akiwa katika mahangaiko hayo, wakaja watu nyumbani kwake wakiomba msaada wa kutibiwa magonjwa yao. Hao watu walisikia kuwa yeye ni mganga wa kienyeji, wala hawakujua kuwa alikuwa ameokoka na kuacha uganga huo.

Kwa sababu ya kukosa fedha, huyo mtu aliyeokoka akawaza moyoni mwake; “Hawa watu hawajui kuwa nimeokoka, kwa hiyo hakuna haja ya kuwaambia, kwani kuna ubaya gani nikienda kuwachimbia dawa ninazozifahamu halafu wanipe fedha inisaidie?”

Kwa hiyo akaenda akawachimbia hizo dawa akawapa. Na hao watu wakaondoka baada ya kumlipa fedha. Lakini usiku, huyo aliyeokoka alipokuwa amelala aliona katika maono. Katika maono hayo akayaona majini mawili yaliyokuwa yanamsaidia katika uchawi zamani kabla ya hajaokoka. Hayo majini yakasema; “Tulikwaambia hutafanikiwa katika wokovu, sisi ndiyo tumekufilisi mali yako. Na pia sisi ndiyo tuliowatuma wale wagonjwa waje kwako. Ulipochima zile dawa ukatuita tulikokuwa. Sasa tumekuja, mwache Yesu njoo kwetu nasi tutakutajirisha”.

Huyo mtu aliyeokoka aliposikia hayo, akatambua kosa lake, na mara hiyo akalikumbuka jina la Yesu Kristo. Kwa hiyo akayakemea yale majini nayo yakatoweka. Akamka akiwa anatetemeka.

Kama asingelikumbuka uwezo wa jina la Yesu Kristo, angefanya nini? Naamini kama angepata msaada wa mahitaji yake toka kwa wakristo wenzake, asingebanwa na mtego huo. Wakristo naomba kuwakumbusha kusaidiana. Ni muhimu sana kwa maisha yetu ya kila siku.

Ndiyo maana Mtume Paulo aliongozwa na Roho Mtakatifu kuandika hivi:

“Kwa habari za kuwahudumia watakatifu (Wakristo) sina haja ya kuwaandikia. Maana najua utayari wenu, ninaojisifia kwa ajili yenu kwa Wamakedonia, kwamba Akaya ilikuwa tayari tangu mwaka mzima; na bidii yenu imewatia moyo wengi wao ……. Maana utumishi wa huduma hii hauwatimizii watakatifu (Wakristo) riziki walizopungukiwa tu, bali huzidi sana kuwa na faida kwa shukrani nyingi apewazo Mungu, kwa kuwa mkijaribiwa kwa utumishi huo, wanamtukuza Mungu kwa ajili ya utii wenu katika kuikiri Injili ya Kristo, na kwa ajili ya ukarimu wenu mliowashirikisha wao na watu wote”(2Wakorintho 9:1,2,12 – 15)

Ndiyo maana pia katika makanisa kuna mgawanyiko wa huduma. Kuna wengine kazi yao ni kuhubiri na kuwaambia watu waache dhambi kama, uasherati na wizi. Ni wajibu wa wale wanaoshughulika na mambo ya miradi ya maendeleo katika kanisa ni kusaidiana na wahubiri hao kuwaongoza watu waishije baada ya kuacha uasherati na wizi.

Napenda kukuhimiza hata wewe unayeyasoma haya kuwa, ukiona mwenzako ni mhitaji wa kitu fulani ambacho unacho, usisite kumsaidia. Kumbuka huduma hii ina thawabu yake kama Mtume Paulo anavyosema.

Hebu jibu swali hili; “Lakini mtu akiwa na riziki ya dunia, kisha akamwona ndugu yake ni mhitaji, akamzuilia huruma zake, je! Upendo wa Mungu wakaaje ndani yake huyo?" (1Yohana 3:17)

Mzee Yohana anatushauri anasema, “Watoto wadogo, tusipende kwa neno, wala kwa ulimi, bali kwa tendo na kweli” (1Yohana 3:18).

Ni kweli Bwana Yesu Kristo alipokuwa hapa duniani alikuwa maskini, lakini baada ya kufufuka alirudishiwa utajiri wake. Ndiyo maana Mtume Paulo anazungumzia juu ya “……… utajiri wake Kristo usiopimika” (Waefeso 3:8). Na katika Wafilipi 4:19 tunasoma hivi; “Na Mungu wangu atawajazeni kila mnachokihitaji kwa kadri ya utajiri wake, katika utukufu, ndani ya Kristo Yesu”.

Kumbuka ya kuwa; Yesu Kristo alichukua madhaifu yetu na magonjwa yetu yote, na kwa kupigwa kwake sisi tumepona (Isaya 53:5; Mathayo 8:16, 17; 1Petro 2:24). Na kwa kujua hili kanisa linajihusisha na kuombea wagonjwa na kutoa huduma za afya kwa wagonjwa.

Kumbuka ya kuwa; Yesu Kristo alichukua dhambi zetu na akafanyika dhambi kwa ajili yetu,“Ili sisi tupate kuwa haki ya Mungu katika Yeye” (2 Wakorintho 5:21). Na kwa kujua hili kanisa linahubiri habari za ondoleo la dhambi kwa ye yote atakayemwamini Kristo.

Kumbuka ya kuwa; Yesu Kristo alikuwa maskini, ingawa alikuwa tajiri, ili kwa umaskini wake sisi tupate kuwa matajiri (2Wakorintho 5:21). Na kwa kujua hili kanisa linajihusisha na miradi mbalimbali ya kimaendeleo ili mtu aondokane na umaskini. Wakristo binafsi pia wanashauriwa kuwa na miradi isiyovunja maadili ya kikristo, ili waondokane na umaskini.


Mwl. C. Mwakasege

Comments