TUFUNGE WAKATI GANI?



BWANA YESU asifiwe.

Mwanzoni mwa mwaka 2009 yaani miezi michache tu baada ya kuokoka, BWANA alisema nami  usiku baada tu ya kutoka kanisani . kwamba mtu hataishi kwa mikate tu(Chakula) bali kwa neno la MUNGU. Muda huo huo nilipanga kufunga kwa siku 3 bila kula wa kunywa chochote , nilifunga ila masaa 8 ya mwisho nilishindwa kumaliza na kufungua. Nilisema nitafunga tena baada ya wiki 1 na kweli nilifanikiwa kufunga siku 3 na huo ulikuwa ni mwanzo mzuri sana kwangu maana ilisababisha  kuona mambo mengi sana katika ulimwengu wa Roho. BWANA alinionyesha hata nguvu zangu za kiroho, alinionyesha silaha zangu na ukubwa wake na jinsi ambavyo zinauwezo wa kuangamiza mipango yote ya adui, alinionyesha maadui zaidi ya 100 wakinisaka lakini kwa msaada wake niliwashinda wote. Ukweli kufunga ni muhimu sana kwa kila mtu.


Kufunga ndani yake kuna maombi Hivyo kufunga na maombi huambatana.Mtu akifunga harafu hakuomba wakati wa kufunga kwake , mtu huyo amefanya tu mgomo wa kula .
 Mathayo 17:21’’Lakini namna hii haitoki ila kwa kusali na kufunga’’



Miezi miwili iliyopita niliota ndoto ya ajabu sana . Niliona nikiwa na watu wengi ninaowafahamu na kila mmoja wetu alikuwa amejifunika shuka lake na kusinzia, wengine wanakoroma isipokuwa mimi tu ambaye nilikuwa nimejifunika shuka ila naangalia kutokea ndani ya shuka na kuona nje, ilichukua muda kidogo nikaona mtumishi mmoja wa MUNGU  katika wale wanaofanya vyema sana katika injili Tanzania, akawa anawaangalia watu wote tuliokuwa tumelala katika uwanja huo. Lakini cha ajabu wengine aliwaangalia mara moja tu lakini mimi aliniangalia muda wote huku nikidhani hanioni ila mimi ndio ninayemuona maana tulikuwa kimya sana kiasi kwamba angekuwa mtu wa kawaida angejua wote tumelala, kumbe mimi sijalala. Mtu Yule ghafla akaniambia kwamba ‘’amka uombe, na tena omba sana, ‘’ nikaamka na kumwomba samahani maana kumbe hakuwa mwanadamu wa kawaida, nikasimama huku wenzangu wote wamelala, nikasema nitaomba akapotea. Wiki hiyo hakika ROHO MTAKATIFU alitaka niombe maana kuna matukio zaidi ya 4 ya hatari sana yalitokea, sikufunga ila niliomba, moja ya matukio yaliyotokea wiki hiyo ni kwamba siku 2 baada ya ndoto hiyo nilikuwa natoka Kawe naenda Gongolamboto kupitia Buruguni kwenye daladala, tulipofika kisiwa yaani kituo kimoja baada ya TMJ Hospital gari letu lilisimama ili kubeba abilia wengine waliokuwa kituoni hapo lakini jambo la ajabu lilitokea ambapo gari yetu ilipokaribia tu kusimama, watu waliokuwa nje walianza kupiga kelele na kusema ‘’mnakufaaaaaaaaaaa’’ tukaanza kuwashangaa na mmoja wao akasema gari yenu inawaka moto chini kote, kitendo kile kilipelekea watu kugombania mlangoni ili kuokoa maisha yao, na nilishangaa mzee mmoja kikongwe sana ambaye nilimpisha siti aliruka na kuwa wa kwanza kutoka nje , nikabaki nacheka. Wakati watu wakigombania mlangoni Rohoni mwangu niliambiwa kwamba nisihofu ni amani kubwa ipo. Nilishuka kwenye gari nikiwa wa mwisho na hakika nikakumbuka kwamba ndio maana BWANA aliniambia kuomba siku ile maana alijua kipi kiko mbele yangu.

Konda na dereva wake walianza kulaumiana na kusema wamesahau kuweka maji kwenye gari kwa muda mrefu sana tukaanza gari inaungua moto na tukatembea hadi moroco kupanda gari zingine tukaondoka. Ilikua ni hatari sana lakini BWANA YESU alisikia maombi yangu ya wiki ambayo niliyaomba baada ya ndoto ile.

Leo tunazungumzia habari za kufunga.

Kufunga ni jambo muhimu sana kwa wateule wa KRISTO.

BWANA YESU anatuambia kwamba Mengine tunayoyahitaji ili yafanikiwe tunahitaji kufunga na kuomba.

Ninachotaka kukuambia leo ni kwamba JE NI WAKATI GANI TUFUNGE?


                  Kuna nyakati 3 za kufunga kwa watu wa MUNGU.



  1.    TUNAFUNGA WAKATI AMBAO ROHO MTAKATIFU ANATUTAKA NA KUTUONGOZA KUFUNGA.

Luka 4:1-2 ( Na YESU, hali amejaa ROHO MTAKATIFU, alirudi kutoka Yordani, akaongozwa na ROHO muda wa siku arobaini nyikani, akijaribiwa na Ibilisi. Na siku hizo alikuwa hali kitu; hata zilipotimia, aliona njaa. ).

ROHO MTAKATIFU anatujua kuliko vile ambavyo sisi tunajijua, anapokuambia kufunga ni upendo wake mkuu sana na ajabu sana maana yeye anajua yote yaliyopo na yajayo yote. Hivyo kwa sababu unaishi na MUNGU ndani yako kama Biblia inavyosema basi mtii yeye maana ndiye kiongozi mwema.



2.   TUNAFUNGA WAKATI AMBAO TUNAITWA NA VIONGOZI WA KANISA KWA AJILI YA KUFUNGA.

Waebrania 13:17 (Watiini wenye kuwaongoza, na kuwanyenyekea; maana wao wanakesha kwa ajili ya roho zenu, kama watu watakaotoa hesabu, ili kwamba wafanye hivyo kwa furaha wala si kwa kuugua; maana isingewafaa ninyi. ). 
Tusome tena Ezra 8:21( Ndipo nikaamuru kufunga, hapo penye mto Ahava, ili tupate kujinyenyekeza mbele za MUNGU, na kutafuta kwake njia iliyonyoka, kwa ajili yetu sisi wenyewe, na kwa ajili ya watoto wetu, na kwa mali yetu yote. )

Ezra hapa kama kiongozi wa kundi au kama mfano wa viongozi wetu wa kanisa anaagiza kufunga baada ya kuona jambo Fulani halijakaa vizuri. Nivizuri sana ndugu zangu tuwe watii kwa vingozi wetu wa kanisa katika mambo kama haya maana hadi Mchungaji au Askofu au Mtume au Nabii anasema kwamba tufunge ina maana katika ulimwengu wa Roho kuna jambo ameona. Na yawezekana baada ya maombi hayo kuna ushindi mkuu sana kwako na kwa kanisa hivyo usiache kufunga,



3.      TUNAFUNGA BAADA YA KUAMUA KUFUNGA.



Hii hua ni kuchagua tarehe na kutenga ili kufunga hivyo ni jambo jema sana  kwa kila Mkristo.

Kufunga kunakusaidia wewe mwenyewe mfungaji.

Kufunga kunakuboresha sana kiroho chako.

Maombi ya kufunga huwapiga waliotumwa na shetani hata kama hawataki wataondoka tu ila ni kufunga na maombi maana ukifunga harafu kwa muda wote huo wa kufunga kwako ukawa kukuomba basi tambua kwamba ulifanya tu mgomo wa kula na sio kufunga ili kupokea jambo kutoka kwa MUNGU.



 -Kufunga kunaonyesha hitaji letu kuu kwa MUNGU

 -Kufunga kusifanywe ili kujionyesha.

 Kwa leo naishia hapo, MUNGU akitupa nafasi tutajifunza tena siku nyingine.na kama hujampokea BWANA YESU muda wa kumpokea ni leo wala sio kesho, amua leo na atakuandika jina lako katika kitabu cha uzima na utaanza kuukulia wokovu kwa mafundisha kanisani. ROHO MTAKATIFU aliyenipa ujumbe huu ana makusudi kabisa na wewe, hataki upotelee motoni anataka uende uzimani aliko KRISTO BWANA.
                     MUNGU akubariki sana .
                      Ni mimi ndugu yako
                       Peter M Mabula
                 Maisha ya Ushindi Ministry.
                           0714252292


Comments