UCHUMI WA UFALME WA MBINGUNI (sehemu ya 2)

Na Mwl. Mwakasege



Mwenye haki ataishi kwa imani
Nabii Habakuki aliishi katika kipindi kilichokuwa kigumu sana kiuchumi. Hali hii iliwafanya watu wengi kuingia katika dhuluma, udanganyifu na mambo mengine maovu ili tu waweze kuishi.
Lakini kilichoumiza moyo wa Nabii Habakuki ni kuona kuwa kulikuwa na watu wachache ambao hawakufuata mambo maovu – lakini waliishi maisha magumu na kuonewa na matajiri wa wakati huo. Hali hii ilimfanya Nabii Habakuki aingie katika maombi ya kumlalamikia Mungu, huku akihitaji kujua mpango wa Mungu juu ya watu waliosimama upande wake. Soma kitabu cha Habakuki sura ya 1 na 2.
Kati ya jibu ambalo Mungu alimpa Nabii Habakuki juu ya maisha ya watu wake katikati ya hali ngumu ya uchumi ni maneno haya;
"….mwenye haki ataishi kwa imani yake" (Habakuki 2:4)
Huu ndio uliokuwa mpango wake kwa watu wake wakati ule ili uwasaidie kuishi katikati ya dhuluma na maovu yanayotokana na hali ngumu ya uchumi.
Katika siku hizi za mwisho, kumetabiriwa kutokea tena hali ngumu ya uchumi inayoambatana na dhuluma pamoja na maovu mbalimbali. Mungu amekwisha andaa mpango mzuri kwa ajili ya wote watakaoipokea na kuikiri injili ya Kristo inayookoa. Na mpango huu ni sawa na ule aliopewa Nabii Habakuki.
Kwa uwezo wa Roho Mtakatifu, Mtume Paulo alisema maneno muhimu yafuatayo:
" Kwa maana siionei haya Injili; kwa sababu ni uweza wa Mungu uuletao wokovu, kwa kila aaminiye, kwa Myahudi kwanza, na kwa Myunani pia. Kwa maana haki ya Mungu inadhihirishwa ndani yake, toka imani hata imani; kama ilivyoandikwa , MWENYE HAKI ATAISHI KWA IMANI" (Warumi 1:16-17). Huu ndio mpango wa Mungu kwa watu wote wanoipokea Injili ya Kristo na kuokolewa. Katikati ya dhuluma,wizi, uasherati na maovu mbalimbali yanayoambatana na hali ngumu ya uchumi iliyopo sasa na ile itakayotokea miaka si mingi iliyo mbele yetu kuanzia sasa – Mungu anawataka watu waishi kwa kufuata mpango wake – WAISHI KWA IMANI.
Kuishi kwa Imani ndiyo utaratibu wa uchumi wa mbinguni ambao kila mkristo anatakiwa kuufuata akitaka kuishi maisha ya mafanikio na matakatifu katikati ya hali ngumu ya uchumi – badala ya kujikuta amewezwa na masumbufu ya maisha haya.
Inasikitisha kuona kuwa wakristo wengi wameyatafsiri na kuyatumia vibaya maneno haya "kuishi kwa Imani". Na kwa ajili hiyo mpango wa Mungu uliomo ndani ya maneno haya haujaeleweka na wengi.
Wakristo wengine wanafikiri kuishi kwa imani ni kuacha kazi wanazozifanya na kuanza kuishi maisha ya omba omba na ya kubahatisha. Wamesahau kuwa biblia inasema mtu asipofanya kazi asile – soma 2Wathesalonike 3:6 – 12.
Ingawa kuna wakristo ambao wamelifanya neno hili "kuishi kwa Imani" lisieleweke vizuri; hali hii haiwezi wala haitaweza kubadilisha mpango wa Mungu uliomo ndani yake.
Mawazo yetu siyo mawazo ya Mungu; njia zetu si njia za Mungu; na mipango yetu si mipango ya Mungu. Hakuna njia ya mkato kwa mkristo safi ya kufanikiwa katika maisha, isipokuwa ni kwa kuishi ndani ya mpango wa Mungu uliofunuliwa katika Kristo Yesu.
"Mwenye haki ataishi kwa imani" maana yake nini? "Mwenye haki" maana yake Mkristo, au Mtakatifu, au Mwongofu, au Mteule, au Aliyeokoka. Kwa hiyo tunaweza kusema Mkristo ataishi kwa imani.
Pia tunasoma katika Waebrania 11:1 ya kuwa:"Basi imani ni kuwa na hakika ya mambo yatarajiwayo, ni bayana ya mambo yasiyoonekana"
Tena imeandikwa katika Warumi 10:17 ya kuwa;"Basi imani, chanzo chake ni kusikia; na kusikia huja kwa neno la Kristo".
Tena imeandikwa katika Yakobo 2:26 ya kuwa;"Maana kama vile mwili pasipo roho umekufa, vivyo hivyo na imani pasipo matendo imekufa".
Kwa mistari hiyo michache na mingine mingi iliyomo katika Biblia inatusaidia kujua ya kuwa "Mwenye haki ataishi kwa imani" maana yake kila mkristo anatakiwa kuishi kwa kuwa mtendaji wa Neno la Kristo na siyo msikiaji tu – kila wakati na katika kila eneo la maisha yake.
Roho Mtakatifu alipokuwa anatufundisha haya mimi na mke wangu, tulijua hakika ya kuwa tunatakiwa kutumia muda mwingi kulisoma na kulitafakari Neno la Kristo, ili tuweze kulitenda Neno hilo katika maisha haya. Tulianza kusoma Neno la Mungu na vitabu mbalimbali vilivyoandikwa na watumishi wa Mungu na bado tunaendelea kufanya hivi hata leo, na tumeona mabadiliko makubwa katika maisha yetu – maana mahangaiko tuliyokuwa nayo yametoweka kwa jina la Yesu Kristo! Sasa tunaishi katika maisha ya ushindi na amani ndani yake Kristo.
Tatizo ambalo mtu analipata anapookoka, ni namna ya kuishi katika maisha mapya ya wokovu (2Wakorintho 5:17)
Biblia inatuambia ya kuwa sisi ni raia wa nyumbani mwake Mungu (Waefeso 2:19). Pia inatuambia kuwa sisi si wa ulimwengu huu (Yohana 17:14). Kwa hiyo maisha yetu hayatakiwi kuongozwa na utaratibu wa hapa duniani.
Kuna tofauti kati ya utaratibu wa uchumi wa duniani na utaratibu wa uchumi wa ufalme wa mbinguni. Ingawa sisi tulio wake Kristo tumo humu ulimwenguni hatutakiwi kuishi kwa kutegemea utaratibu wa uchumi wa dunia hii unaoyumba, bali tutegemee utaratibu wa uchumi wa ufalme wa mbinguni – usioyumba wala kubadilikabadilika kwa kuwa umejengwa juu ya mwamba imara – Neno la Kristo.
Wakristo wengi kwa kutokujua hili wamejikuta wakipata shida ya kutaka kuwatumikia mabwana wawili – yaani Mungu na Mali ambapo Yesu Kristo alikwishasema haiwezekani. Matokeo yake ni kupoteza ushuhuda wa kikristo na kuishi maisha ya mahangaiko.
Kutegemea utaratibu wa uchumi wa dunia hii kuna shida sana kwa kuwa uchumi huo ukiyumba kidogo, na wewe unayumba kimaisha. Lakini ukiutegemea utaratibu wa uchumi wa ufalme wa mbinguni huwezi kuyumba wakati uchumi wa dunia ukiyumba – kwa kuwa tumaini lako halimo mikononi mwa dunia na wanadamu – bali ndani ya Kristo Yesu ambaye ni mwamba imara usiotikisika.

Mwl. Mwakasege

Comments