UMEBEBA TAARIFA GANI KATIKA MOYO WAKO?


Na Peter M Mabula
                    Maisha ya Ushindi Ministry.

BWANA YESU asifiwe.

Nakukaribisha tujifunze somo hili la muhimu kwako na kwako, ni maombi yangu kwamba nguvu ya MUNGU iliyo katika neno lake hili ikuzalie matunda katika maisha yako.

Kila mtu amebeba taarifa katika moyo wake. 

Askari akiambiwa amlenge adui vitani, atamlenga na kumpiga adui kwa sababu ana taarifa sahihi kuhusu silaha yake na pia ana taarifa kuhusu kupiga risasi. Ni tofauti na yule ambaye hajui chochote kuhusu silaha na risasi, hawezi kufanya lolote maana hana taarifa sahihi kuhusu silaha



Wewe umebeba taarifa gani moyoni mwako?

Anayeuza mchele anauwezo wa kuupembua mchele kilo 1 na kuuweka juu ya gunia la kilo 200 ili kila mteja akija aseme ‘’mchele huu ni mzuri sana’’ kumbe mchele mzuri ni kilo moja tu ya juu. Huyu mfanya biashara ana taarifa sahihi katika biasahara yake.


Najua unataarifa ya jambo fulani lakini huwezi kufanya kazi hiyo ili ikutajirishe.

Wangapi wanajua kushona kushona cherehani lakini kwa miaka 3 wamekosa pesa ya kukunua cherehani?

Ili uwe na taarifa sahihi moyoni mwako lazima kwanza uwe umebadilishwa na MUNGU. Ezekieli 36:26-27 ( Nami nitawapa ninyi moyo mpya, nami nitatia roho mpya ndani yenu, nami nitatoa moyo wa jiwe uliomo ndani ya mwili wenu, nami nitawapa moyo wa nyama. Nami nitatia roho yangu ndani yenu, na kuwaendesha katika sheria zangu, nanyi mtazishika hukumu zangu, na kuzitenda.)

MUNGU ametuahidi kutupa moyo wa nyama yaani moyo wa upole, moyo wa kusikiliza ushauri mzuri,na ni moyo wa kumsikiliza ROHO MTAKATIFU.

Ndani ya moyo wa mtu kuna siri nyingi sana, moyo ni kama nyumba yaani wakati mwingine ndani ya nyumba hufanyika mambo mengi. Walio nje ya nyumba hiyo hawawezi kujua kama ndani ya nyumba hakuna amani, ndani ya nyumba kuna mapigano.

Mazingira mazuri ya kazi yako uitakayo yako ndani ya moyo wako. 

Nina uhakika una taarifa njema kuhusu unavyokusudia moyoni mwako mtu wa MUNGU, Lakini vikwazo vimekukwamisha na kuna baadhi ya watu huabudu vikwazo badala ya kuendelea kuifanyia kazi taarifa njema walionayo ya baraka zao.

VIKWAZO VYA KUTOKUFANIKIWA KWA TAARIFA YAKO NI.

1.   Hufanyi maombi.

2.   Unawaza kushindwa tu.

3.  Unawaza hasara tu ambayo unaweza kuipata kama mambo yakienda vibaya.

4.  Kujilinganisha na wenginewaliofanikiwa..



Kutoka 4:1-7( Musa akajibu akasema, Lakini, tazama, hawataniamini, wala hawataisikia sauti yangu; maana watasema, BWANA hakukutokea. BWANA akamwambia, Ni nini hiyo uliyo nayo mkononi mwako? Akasema, Ni fimbo.  Akamwambia, Itupe chini; akaitupa chini, nayo ikawa nyoka; Musa akakimbia mbele yake.  BWANA akamwambia Musa, Nyosha mkono wako, kamshike mkia; (akaunyosha mkono wake akamshika, naye akageuka kuwa fimbo mkononi mwake;)  ili kwamba wapate kusadiki ya kwamba BWANA, MUNGU wa Ibrahimu, MUNGU wa Isaka, MUNGU wa Yakobo, amekutokea.  BWANA akamwambia tena, Sasa tia mkono wako kifuani mwako. Akautia mkono wake kifuani mwake; naye alipoutoa, kumbe! Mkono wake ulikuwa una ukoma, umekuwa mweupe kama theluji.  Akasema, Tia mkono wako kifuani mwako tena. Akautia mkono wake kifuani mwake tena, na alipoutoa kifuani mwake, kumbe! Umerudia hali ya mwili wake. ).

Kwanini Musa aliambiwa maneno hayo?

Ni kwa sababu Musa hakuwa na taarifa sahihi juu ya MUNGU wa Ibrahimu, Isaka na Yakobo.

-Musa alikuwa na taarifa ya kuchunga kondoo tu.

-Musa hakuwa na taarifa ya utumwa wa Waisraeli kwamba umefika mwisho.

-Musa hakuwa na taarifa kwamba inawezekana kumshinda Farao.

-Musa alikuwa na taarifa tu ya kwamba kama akienda Misri atakufa kwa sababu ya kumwua Mmisri miaka ya nyuma.

-Musa hakuwa na taarifa za kumalizika mika a430 za utumwa wa Waisraeli kule Misri.



Yoshua 1:8( Kitabu hiki cha torati kisiondoke kinywani mwako, bali yatafakari maneno yake mchana na usiku, upate kuangalia kutenda sawasawa na maneno yote yaliyoandikwa humo; maana ndipo utakapoifanikisha njia yako, kisha ndipo utakapositawi sana. )

Hapa Yoshua anafundishwa utii wa neno la MUNGU.
 Hata wewe umekutana na neno mara nyingi sana iwe ni kanisani,Radioni, Mtandaoni au hata kwenye simu kupitia SMS. Je ulibeba taarifa gani kutokana na mafundisho hayo ambayo itakuletea Baraka katika maisha yako?

-Yawezekana umetaka kuwa mtu Fulani maishani mwako, lakini tambua kwamba direction ya kuifikia hatima yako iko ndani ya neno la MUNGU.

Mwongozo wako wa kukufikisha huko kwenye hatima nzuri ya maisha yako ni neno la KRISTO.

-Yawezekana unataka kuwa rubani maishani mwako, neno la MUNGU linakuambia ‘’ Mshike sana elimu, usimwache aende zake.’’ Kasomee urubani huku ukimwomba MUNGU akufikishe kwenye taarifa yako hiyo ya kuwa rubani. Ni kweli taarifa ya kuwa rubani unayo lakini ukipewa ndege leo uendeshe hutaweza kwa sababu hujasomea.

Taarifa inatangulia kwanza kabla ya tukio.

Hebu tujifunze kitu hapa Isaya 38:1-5 (Siku hizo Hezekia aliugua, akawa katika hatari ya kufa; na Isaya nabii, mwana wa Amozi, akaenda kwa mfalme, akamwambia, BWANA asema hivi, Tengeneza mambo ya nyumba yako; maana utakufa, wala hutapona.)

Mfalme Hezekia alikuwa na taarifa ya kufa kwa sababu ya ugonjwa lakini Nabii Isaya analeta taarifa mpya kwamba kama atarekebisha baadhi ya vitu  na kumwomba MUNGU ataishi.

Wewe je una taarifa gani katika moyo wako?

Kama una taarifa njema ya kwenda uzima wa milele mpe BWANA YESU maisha yako.

Yoshua akaambiwa alishike neno na aliishi neno ndipo atakapofanikiwa  sana kihuduma, kimaisha na kikazi pia.

-Ukiona nyumbani mwako una TV basi hiyo TV uliiona moyoni mwako kabla ya kuinunua, hiyo ndio taarifa.

-Kama una mafanikio Fulani maishani mwako, hakika uliyaona kabla hata ya kuyapata, hiyo ndio taarifa. Taarifa hii inakuja kuwa kweli baada ya kuitendea kazi.Wengine wanakaa nazo taarifa zao bila kuzitendea kazi, hiyo ni mbaya.

-Kama mama anaenda kununua mwiko sokoni, na hata akiwa njiani ukimuuliza  ‘’unaenda wapi’’ atakuambia ‘’naenda sokoni kununua mwiko’’ Hiyo ndio taarifa  na mama huyo atanunua maana taarifa ilikuja kabla ya tukio na yeye kuifanyia kazi taarifa hiyo.

AONAVYO MTU NAFSINI MWAKE, NDIVYO ALIVYO-Mithali 23:7.

Je wewe unaona nini moyoni mwako? Unachokiona katika BWANA ndio taarifa njema ya mafanikio yako ya baadae.

Tambua hii 

‘’PASIPO MABADILIKO ,HAKUNA HATUA’’

‘’PASIPO TAARIFA, HAKUNA TUKIO’’
 

Kwa leo naishia hapo, MUNGU akitupa nafasi tutajifunza tena siku nyingine.na kama hujampokea BWANA YESU muda wa kumpokea ni leo wala sio kesho, amua leo na atakuandika jina lako katika kitabu cha uzima na utaanza kuukulia wokovu kwa mafundisha kanisani. ROHO MTAKATIFU aliyenipa ujumbe huu ana makusudi kabisa na wewe, hataki upotelee motoni anataka uende uzimani aliko KRISTO BWANA.

                       MUNGU akubariki sana .

                        Ni mimi ndugu yako

                          Peter M Mabula

                    Maisha ya Ushindi Ministry.

                         0714252292

Comments