USHINDI DHIDI YA ADUI ZAKO

Na Frank Philip


Angalia jambo hili, “Kama mkienda katika amri zangu, na kuyashika maagizo yangu, na kuyafanya; (Lawi 26:3) Nanyi mtawafukuza adui zenu, nao wataanguka mbele zenu kwa upanga. Na watu watano wa kwenu watawafukuza watu mia, na watu mia wa kwenu watawafukuza watu elfu kumi; na adui zenu wataanguka mbele yenu kwa upanga. Nami nitawaelekezea uso wangu, na kuwapa uzazi mwingi, na kuwaongeza; nami nitalithibitisha agano langu pamoja nanyi” (Lawi 26:7-9).

Kisha angalia hapa, “Lakini msiponisikiza, wala hamtaki kuyafanya maagizo hayo yote; nanyi mkizikataa amri zangu, na roho yenu ikichukia hukumu zangu, hata ikawa hamtaki kuyafanya maagizo yangu yote, bali mwalivunja agano langu; mimi nami nitawatenda jambo hili; nitaamrisha uje juu yenu utisho, hata kifua kikuu na homa, zitakazoharibu macho yenu, na kuidhoofisha roho; nanyi mtapanda mbegu yenu bure, kwa kuwa adui zenu wataila. Nami nitauelekeza uso wangu kinyume chenu, nanyi mtapigwa mbele ya adui zenu; hao wawachukiao watatawala juu yenu; nanyi mtakimbia wakati ambao hapana awafukuzaye” (Lawi 26:14-17).

Hii mbaya sana, “Tena hao wa kwenu watakaobaki, nitawatilia woga mioyoni mwao, katika hizo nchi za adui zao; na sauti ya jani lililopeperushwa itawakimbiza; nao watakimbia, kama mtu akimbiavyo upanga; nao wataanguka hapo ambapo hapana afukuzaye” (Lawi 26:36).

Najaribu kulinganisha mistari hii na hali ya sasa. Namshukuru Mungu kwa sababu ya Neema inayotufunika; kwayo hatuhesabiwi kushinda kwa matendo ya sheria ila katika Imani katika Mwana wa Mungu. Haki yetu hupatikana kwa njia ya Imani na tunarithi baraka zetu kwa Imani pia. Lakini jifunze jambo hili, walio mjua sana Bwana watakuwa hodari na washindi. Wamchao Mungu wataumiliki mlango wa adui zao. Umeona hiyo siri ya ushindi? Watu wale wale ambao 5 watawafukuza adui zao 100; na ambao 100 watawafukuza adui zao 10,000, ndio hao hao wakikorofishana na Mungu wanakimbia unyasi upeperushwao na upepo tu!

Hebu angalia hofu ilivyo mbaya; mtu anakimbia unyasi ukipeperushwa na upepo kama kukimbia upanga! Sasa unaweza kudhani ni utani, waulize waganga wa kienyeji kama kuna kitu wanakosa wakitaka kwa mteja wao; naam, hata wengine wamewatoa wazazi au watoto wao kwa sababu ya HOFU ya madhara kama hawatakubaliana na masharti ya mganga. Anaheri mtu yule ambaye Bwana ni Mungu wake, hatakosa usingizi kwa vitisho vya adui zake.

Frank Philip.

Comments