Ushuhuda:KUFUNGA NA KUOMBA KULIFUTA DHAMBI YA UZINZI ILIYONITESA KWA MIAKA MINGI.


Pamoja na kwamba nilikuwa nimemuamini Yesu katika maisha yangu lakini nilijikuta nimerudi nyuma sababu ya dhambi ya uzinzi ilinisumbua sana maishani mwangu. Nilijitahidi kumtafuta Mungu lakini kila mara nilianguka katika dhambi ya uzinzi.
Nilivyokuwa nikijaribu kutafakari baada ya muda mwingi sana ikafika wakati nikakata tamaa na wokovu. 
Nilikata tamaa na wokovu maana nilijiona namfanyia Mungu maigizo tu. Nami sikuwa tayari kuendelea na maigizo hayo.
Kuna sababu nyingi zilinifanya nikate tamaa.
Kwanza maandiko yalikuwa yakisema nami kila leo kwamba "Mtu aziniye na mwanamke hana akili kabisa; Afanya jambo litakalomwangamiza nafsi yake" - Mithali 6:32
Hili ni kati ya andiko ambalo lilikuwa likiniumiza sana. Kila wakati neno hili lilinijia na kusema nami. Niliumia ndani yangu maana lilikuwa likiniumiza sana. Nilikuwa najiona mpumbavu nisiye na akili. Na ilikuwa ni kweli maana nilikuwa nikianguka katika dhambi ya uzinzi katika hali nisiyoitegemea. Kumbe kweli akili zote zilikuwa zimeniishia. 
Wakati mwingine nilivyojitahidi kujitakasa na kujikuta nimeanguka neno la Mungu lilinijia na kusema "Msidanganyike; waasherati hawataurithi ufalme wa Mungu" - 1Kor 6:9. Nikajiuliza nitafanya nini mie. Wakati mwingine nikawaza kwamba labda mie sikuandikiwa kuurithi ufalme wa mbinguni. Na ilifika mahali nikajifariji kwa maneno hayo. Nikajiona mie niliandikiwa ziwa la moto. Tena nikawa nikijifariji kwa maneno hayo na baadhi ya vijana wenzangu. Si kwamba nilikuwa siendi kanisani. Kanisani nilienda. Na kila nikienda neno linaniingia kweli na nikitoka kanisani tu kurudi nyumbani nakuwa mtupu sina kitu moyoni mwangu. Niliteseka ndani yangu. Roho Mtakatifu aliendelea kuniandama kila leo kuniambia habari ya toba ya kweli. Nikawa sina namna ya kufanya. Nikaanguka na kulala katika lindi la dhambi ya uzinzi.
Kwa sababu hiyo nikaona ni heri hata jumapili nisiende kanisani kabisa. Na kweli nikakaa nyumba takribani miaka 5 siendi kabisa kanisani. Na kila leo Roho Mtakatifu siku kwa siku alizungumza nami kwa habari ya kumrudia Mungu ili nimtumikie. Wakati nikisoma niliweka nadhiri kwamba Mungu akinipa kazi nitamtumikia. Na kweli nilivyomaliza masomo yangu tu nikapata kazi nzuri Serikalini. Lakini wakati napata kazi tayari nilikuwa nimeshaanguka katika dhambi. 
Baada ya kipindi cha miaka ipatayo 5, nilivyokuwa nikijifariji kwamba mie nimeandikiwa kwenda kuzimu siku moja neno la Mungu likanijia kusema "injili ni uweza wa Mungu uletao wokovu kwa kila aaminiye". Neno hili lilianza kuleta mabadiliko chanya ndani yangu. Kwamba kumbe sijaandikiwa kuishi jehanamu. Lakini nikiamini tu basi nitaokoka. Hii ilikuwa hatua ya kwanza kwangu kwamba suala ni kuamini tu. Maana kilaa aaminiye ataokolewa.
Wema wa Mungu uliendelea kusema nami na ndipo nilipoamua kurudi kwa Kristo. Roho Mtakatifu aliamua kunipokea vizuri  sana na kwa wema usio wa kawaida. Niakaanza upya katika kumtumikia Mungu. Mtihani wa dhambi ya uzinzi ulikuwa pale pale.
Siku moja neno la Mungu likanijia kusema kwamba kuna mambo mengine siwezi kuyashinda isipokuwa kwa kufunga na kuomba.

Ndipo ufahamu wangu ukafunguka. Lakini nikatii ufahamu huu. Nikaanza kufunga mara moja kwa wiki kwa ajili ya kuutafuta uso wa Mungu.
Roho Mtakatifu alikuwa mwaminifu kunifundisha namna ya kuenenda. Tangu siku hiyo nimekuwa nikitembea katika nguvu ya Mungu. Si kwamba majaribu ya uzinzi hayaji, la. Majaribu yanakuja lakini Mungu ananipa nguvu ya kushinda dhambi. 

Nikalikumbuka neno la Mungu kwamba "kwa jina lake kila amwaminiye atapata ondoleo la dhambi". Namshukuru Mungu naendelea kumtumikia.
Na niwatie moyo wale ambao wameshindwa kusimama kwa sababu ya uzinzi. Mungu yuko tayari kukusaidia.
Ikimbieni zinaa. Dhambi ya zinaa ni mbaya kuliko ujuavyo. Kuja kujitoa ni gharama kubwa ndugu yangu.
Ubarikiwe sana.


Ushuhuda huu umeletwa na kijana ambaye hakupenda kuweka wazi jina lake katika Makala hii.

Comments