WOKOVU KWANZA *sehemu ya tatu *

Na Mtumishi Gasper Madumla


Haleluya....

" Zakayo akasimama, akamwambia Bwana, Tazama, Bwana, nusu ya mali yangu nawapa maskini, na ikiwa nimenyang'anya mtu kitu kwa hila namrudishia mara nne.

Yesu akamwambia, Leo wokovu umefika nyumbani humu, kwa sababu huyu naye ni mwana wa Ibrahimu.
Kwa kuwa Mwana wa Adamu alikuja kutafuta na kuokoa kile kilichopotea. " Luka 19:8-10

Zakayo aliona bora apoteze vitu vyote alivyokuwa navyo alivyopata kwa njia isiyo halali,ili ampate Yesu. Jambo hili si rahisi kabisa,la kuvitoa vitu uvipendavyo kwa ajili ya Kristo.
Unajua Zakayo alitazama mbali sana,maana alijua kama atakuwa na Yesu kisha aendelee kuvishikilia mambo au vitu alivyopata kwa hali ya dhambi,alijua atampoteza Bwana Yesu,moyo wake Zakayo gafla ukageuka kutoka katika uharibifu na kumuelekea BWANA,

Ndiposa akasema ;
" Bwana, nusu ya mali yangu nawapa maskini, na ikiwa nimenyang'anya mtu kitu kwa hila namrudishia mara nne. "

Haleluya...

Sasa unisikilize vizuri;
Kanuni ya kupenda inasema hivi;
Yeye atoaye hupenda kwanza.

Huwezi ukatoa kitu cha thamani na kubarikiwa pasipo kupenda.
Yeye anayetoa hupenda.
Mungu alipoupenda ulimwengu,AKATOA mwanaye wa pekee,Yesu Kristo.(Yoh.3:16)

Ok,
Kwa lugha nyingine,Zakayo alikamatwa na nguvu ya pendo kwanza kabla hajaamua kutoa nusu ya mali yake,maana alipompenda Bwana akaona uzuri ulio ndani ya Bwana Yesu,akaona ndani ya Bwana Yesu hakuna doa la dhambi,wala doa la unyanga'nyi ndiposa akasema nusu ya mali yake awape maskini. Lakini pia na kuwarudishia wale wote aliowanyanga'nya kwa hila,warudishie mara nne.

Je unafikiri,
Zakayo alikuwa mjinga?

La hasha! Hakuwa mjinga hata kidogo,
Aliweza kufanya maamuzi hayo magumu kwa sababu WOKOVU ULIINGIA NDANI YAKE.

Hakuna jambo gumu linalomshinda Mungu,Ni uwepo wa Mungu ndio ulio msukuma Zakayo kufanya hayo yote,lakini pia uelewe kwamba ilikuwa si rahisi mtu kutoa nusu ya mali yake na kuwapa maskini. Zingatia hapo sio suala la kutoa kidogo mali yake BALI KUTOA NUSU YA MALI YAKE.

Hakika sio rahisi kabisa jambo hili. Zakayo anaona ni bora ashuke na kupungua ili Bwana ainuliwe,kwa sababu Biblia takatifu inatueleza kwamba Zakayo alikuwa ni mtu tajiri,mtu tajiri atoapo nusu ya mali yake,maana yake ni kutoa nusu ya utajiri wake,hivyo hushuka kwa ajili ya kumpata Kristo.

Bwana Yesu asifiwe....

Sasa,
Ukitaka kumgusa Bwana Mungu,mtolee kilichobora,na si cha kinyonge.
Shida ya leo ni hii;
Ukitaka kumgusa mkristo wa leo,nenda kaguse mali zake,na hapo ndipo utamjua ya kwamba mkristo huyo ameokoka au la?
Kipimo hiki hata Bwana Mungu anakijua maana alimpima Ayubu,pale shetani aliporuhusiwa akashike kwa kuharibu mali za Ayubu

Imeandikwa;
" Lakini nyosha mkono wako sasa, uyaguse hayo yote aliyo nayo, naye atakukufuru mbele za uso wako. " Ayubu 1:11

Lakini hata hivyo Ayubu hakuteteleka kwa uharibifu wote wa mali zake,bali yeye alikaza kumpenda Bwana Mungu muumba wa vyote.
Wokovu ulipoingia kwa Zakayo,akajua ya kwamba WOKOVU KWANZA vingine vitafuata;
Ndio maana hakuona shida kurudisha mali zote za udhalimu.
Kwa lugha nyingine,mali zote za kunyanga'nya aliziona kama mavi ili ampate Kristo,maana imeandikwa;

" Naam, zaidi ya hayo, nayahesabu mambo yote kuwa hasara kwa ajili ya uzuri usio na kiasi wa kumjua Kristo Yesu, Bwana wangu; ambaye kwa ajili yake nimepata hasara ya mambo yote nikiyahesabu kuwa kama mavi ili nipate Kristo; " Wafilipi 3:8

Kanisa la leo;
Leo hii watu wengi humkaribisha Bwana Yesu huku mioyoni mwao wameshikilia mambo maovu waliyotoka nayo Misri.
Watu wa namna hii hawawezi kupata mpenyo katika maisha yao ya imani,maana ni sawa na watu wasiookoka tu.

Haleluya...
Ooh...groly to God,glory to God....
Haleluya....

Kuokoka ni kukutana na Yesu,Zakayo hakuwahi kuokoka hata mara moja pale alipokuwa hajakutana na Yesu. Lakini siku ile alipokutana na Yesu Kristo wa Nazareti,ndio ilikuwa siku ya kwanza ya wokovu kuingia ndani yake. Laiti kama asinge'onana na Yesu,basi Zakayo ange'kaa katika hali yake ile ile.
Sisi sote tuliookoka,tuliokoka kwa sababu tulikutana naye Bwana Yesu Kristo.

Sasa angalia;
Hakuna maisha halisi pasipo kuokoka. Kila kitu fanya lakini WOKOVU KWANZA. Kwa sababu sisi tuliookoka tumepewa ahadi ya kuishi maisha ya umilele ( Yoh.11:25-26)

Baada tu ya kuokoka,inakupasa kuyaacha mambo yote ya kimisri,yaani kuyaacha mambo yote ya kidunia uliyokuwa ukiyafanya hapo awali.
Mfano mdogo;
Kama ulikuwa mnywaji pombe,unastahili KUACHA,hata unastahili kuacha kupiga dili za pesa au mipango danganyifu,N.K hata;
Kujitenga mbali na marafiki wa zamami wa kidunia maana ukiendelea kuambatana nao,watakupeleka kwenye upotevu.

Ni lazima nikuambie hili kabla sijaendelea;
Kwamba,
Maisha tuishio katika mwili huu wa damu na nyama ni maisha mafupi sana,tuna takribani siku chache mno za kuishi kuliko watu wadhaniavyo. Laiti kama ungelijua muda wako uliokuwa nao hapa duniani nchi idumupo,basi ungeshtuka na kurejea kwa Bwana kwa toba,na kusii WOKOVU KWANZA ili utakapolala ulale kwa Kristo Yesu ukipokea uzima wa umilele.

Msingi wa fundisho hili tumemwangalia Zakayo kama mtu aliyeamua kuyaacha yote kwa ajili ya kumpata Yesu.
Tamaza Yesu alipomuaona Zakayo,akasema;

" Yesu akamwambia, Leo wokovu umefika nyumbani humu, kwa sababu huyu naye ni mwana wa Ibrahimu. " Luka 19:9

Zakayo alikuwa ni mtu mwenye dhambi lakini kusudi la Mungu lilikuwa ndani yake. Vile alivyokuwa ni mnyanganyi lakini bado Bwana Mungu alimpenda na kumuhurumia. Bwana alimjua tokea mbali kabla ya kuzaliwa sawa sawa na neno la Mungu katika kitabu cha Yeremia;

" Kabla sijakuumba katika tumbo nalikujua, na kabla hujatoka tumboni, nalikutakasa; nimekuweka kuwa nabii wa mataifa. " Yeremia 1:5

Haleluyaa...
Ooh Jesus...

Hii ni hata kwako mpendwa,jinsi ulivyokuwa mbali,Bwana Mungu alikujua,akakuchagua na hatimaye UMEOKOKA. Au yamkini inawezekana bado U mbali kwa habari ya dhambi,sasa ndio wakati wa kurejea kwa Bwana,kuokoka na kuishi maisha ya wokovu. Ninakuambia ipo raha ilioje ndani ya Yesu.

Wengi tulikuwa kama wewe tu,watu wenye dhambi sana,watu wasiofaa,Lakini kwa neema ya Mungu tu sasa ni watu wenye kufaa.
Nampenda Zakayo alivyo fanya jitihada zake za kutafuta kuonana na Yesu.
Jitihada za Zakayo zilizaa matunda maana alifanikiwa kuonana na Yesu mwenyewe.

Zakayo anatufundisha jambo moja la msingi siku ya leo,kwamba ili tumpokee Bwana Yesu yatupasa tuufungue moyo wetu,tuwe na kiu ya kutafuta kumjua.
Laiti kama hatutakuwa na moyo wa KUTAFUTA KUMUONA basi kamwe hatutamuona.

Zakayo alipozingatia moyoni mwake akachukua hatua ya KUTAFUTA KUMUONA YESU ndiposa tunamuona akifanikiwa,na wokovu ukaingia nyumbani mwake.

Yesu Kristo ndio Bwana wa WOKOVU,au kwa lugha rahisi kabisa,lugha isiyohitaji hata kwenda shule,tunasema hivi:
Yesu kristo ndio wokovu wenyewe,hivyo ninavyokuambia WOKOVU KWANZA ni sawa na kusema BWANA YESU KWANZA.
Maana Yesu alipoingia tu kwa Zakayo,
Kilichoingia ni WOKOVU

Mungu wa mbinguni akusaidie sana uyaelewe haya niyasemayo mahali hapa.
Haleluya...

Kuokoka ndio dili la nguvu,katika madili yote chini ya jua,kwa kuyafanya mapenzi ya Baba wa mbinguni pekee.
Maisha ambayo Mungu anatutizamia ni maisha ya WOKOVU KWANZA mengine yoote hayana maana hata kidogo.
Ni bora ukose yote,lakini sio kumkosa BWANA YESU.

Zakayo alipoigundua siri hii akaona haina maana ya kuwa na vitu vingi viovu vitakavyoondoa furaha yake aliyoipokea kwa Bwana Yesu pale alipoingia nyumbani mwake. Yapo mambo mpendwa yanayoweza ondoa furaha ya Bwana ndani yako,yakupasa uyaachilie...

ITAENDELEA...

Usikose kabisaa muendelezo wa fundisho hili zuri sana.
Kwa huduma ya maombi na maombezi,nipigie katika namba yangu hii;
0655111149.

BWANA MUNGU wa mbinguni akulinde na kukupigania ili tuonane katika fundisho lijalo mahali hapa hapa.

UBARIKIWE

Comments