Askofu Mdoe akemea wazazi wanaofanyia watoto ukatili


IMG-20140611-WA0005

ASKOFU msadizi wa Jimbo Kuu Katoliki Dar es salaam, Mhashamu Titus Mdoe amesema kuwa, hatima ya Kanisa na taifa ipo mikononi mwa familia zenyewe. Ameeleza hayo hivi karibuni katika semina ya wazazi na walezi wa watoto wa Shirika la Kipapa la Utoto Mtakatifu, iliyofanyika viwanja vya Msimbazi ikilenga kuwaeleza wazazi faida za watoto wao kushiriki kongamano la watoto na shughuli nyingine za kikanisa. Askofu Mdoe amesema kuwa, hatima ya Kanisa na taifa ipo mikononi mwa familia ambazo zinatakiwa kutoa malezi mema kwa watoto na kuwajengea mstakabali mzuri wa maisha yao ya baadaye na taifa kwa ujumla. “Hatima ya Kanisa na taifa inategemea familia jinsi gani zitaandaa watoto wakiwa wadogo, jambo litakalo sababisha jamii kuwa na watu wema,wanaojali utu na wenye kumcha Mungu. Kutokana na hali hiyo Kanisa limeamua kuwaandaa kuwa wamisionari wa sasa na kesho.” ameeleza Askofu huyo. Aidha, Kanisa na taifa litakuwa na watumishi wazuri kutokana na msingi watakao kuwa wamepewa tangu utoto wao tofauti na wale watakao kosa malezi mema kutoka kwa wazazi na walezi wao. Amesema kuwa kutokana na hazina hiyo iliyowekwa na Kanisa kwa watoto, kazi ya malezi wanayofanya wazazi ni kutimiza agizo la Mungu aliyewaagiza wazae na kuongezeka na wautiishe ulimwengu. Askofu Mdoe ameeleza kuwa, agizo hilo siyo kuzaa peke yake, bali na kuwapa malezi yanayostahili watoto wao ikiwa ni malezi ya kiroho na kimwili. “Mungu hakuagiza watu wazae tu, bali wawalee ili wapate malezi bora kulingana na taratibu za Kanisa, hali hiyo ya kuzaa na kulea inafanya utukufu wa Mungu uonekane kwa watu wake,” amesisitiza Kwa upande mwingine Askofu huyo amesikitishwa na kitendo cha baadhi ya wazazi wanaowazaa watoto na kuwafanyia vitendo vya kikatili bila ya kuwa na hofu ya Mungu. “Inashangaza wazazi mnazaa watoto na kuwafanyia vitendo vya kikatili vinavyokiuka maadili ya Kanisa na sheria za nchi,” amesema Askofu Mdoe. Ameeleza kuwa hali hiyo ya ukatili unaofanywa na baadhi ya wazazi inatakiwa kukemewa kwa njia ya sala ili mwovu ashindwe na wazazi hao wazidishe upendo kwa watoto wao. Aidha amewashukuru wazazi waliohudhuria semina hiyo kwa kuwalea watoto wao kwa kufuata maadili ya Kanisa. Kwa upande wake Mkurugenzi wa Mashirika ya kipapa Jimbo Kuu Katoliki Dar es salaam, Padri Thimetheo Maganga amesema kuwa, wazazi wanatakiwa kuwalea watoto wao katika mwelekeo chanya ili kuwajengea maisha mazuri ya mbeleni. Amesema kuwa wapo baadhi ya watu au makundi fulani yanayoweza kuwachukua watoto na kuwalea katika mwelekeo hasi kwa malengo yao binafsi ikiwa ni pamoja na kuwaingiza katika makundi ya kigaidi. “Tunashuhudia baadhi ya wazazi au makundi yakiwemo ya kigaidi yanavyowalea watoto katika mwelekeo hasi, jambo linalopelekea watoto hao kukua kwa mtazamo huo huo wanaokuwa wamepewa na watu hao,” amesema mkurugenzi huyo. Ameongeza kuwa, iwapo wazazi watawalea watoto katika mwelekeo chanya watoto hao watakuwa viongozi bora katika nyanja mbalimbali watakazo fanyia utume wao. Pia amesema kuwa yale yote ambayo mama Kanisa anayapanga katika maisha ya watoto yanatakiwa kusindikizwa na moyo wa upendo kutoka kwa wazazi kwenda kwa watoto wao. Wazazi wanatakiwa kufuatilia mwenendo wa watoto wao kila siku. Hali ya wazazi kutowalea watoto katika misingi ya kidini ndiko kunakopelekea watoto na watu wazima kukana dini zao na kujiunga katika madhehebu mengine. “Akitokea mtu mzima akakana dini yake, siwezi kushangaa ingawa nitaumia, lakini mtoto akikana dini yake nitalia na mzazi ambaye anajukumu la kumlea mtoto katika misingi ya Kanisa  ili aweze kukabiliana na changamoto mbalimbali,” ameeleza. Wazazi wanawashirikisha watoto wao zaidi katika nyanja mbalimbali zikiwemo za elimu na afya, lakini wanashindwa kuwashirikisha katika masuala ya Mungu. Wazazi wanatakiwa kutambua kuwa hawawezi kujua nafasi ya watoto wao kwa siku zijazo lakini wananafasi ya kuzitengeneza nafasi hizo kwa sasa. Naye Mkurugenzi wa Miito Jimboni humo Padri Henry Kachelewa amesema kuwa safari ya watoto huko Tunduru Masasi ni kuiga mfano wa Yesu Kristo ambaye katika udogo wake alishirikishwa hija na wazazi wake. Kutokana na watoto kuiga mfano wa Yesu, wazazi hawana budi kuwasaidia watoto ili safari za kimisionari wanazozifanya zilete manufaa kwa Kanisa, familia na taifa kwa ujumla. Padri Kachelewa ameongeza kuwa, matunda ya safari za kumisionari zinazofanywa na watoto yataonekana kwa fadhila zitakazoonyeshwa na watoto wenyewe katika maisha yao ya baadaye. Kwa upande mwingine Mkurugenzi huyo amekemea kitendo cha baadhi ya wazazi kuwapeleka watoto wao katika shule za bweni kwa kigezo cha kuwapatia maisha bora wakati wanawaharibu. “Wazazi mnatakiwa muangalie umri wa mtoto anayefaa kupelekwa shule ya bweni kwani baadhi yenu mnawapeleka watoto katika shule hizo wakiwa na miaka miwili au mitatu kwa kisingizio cha kuwapa fursa ya kufanya mambo yenu kwa uhuru bila kujali athari anazozipata mtoto,” Ameendelea, “Kitendo hicho kinamkosesha mtoto malezi mema kutoka kwa wazazi pamoja na kumuathiri kisaikolojia, kwani watoto hao wanawachukulia walezi wao wa shuleni kuwa ndio wazazi wao,”

Comments