IMANI yako IKO WAPI?

Na Frank Philip


“Ikawa siku zile mojawapo alipanda chomboni yeye na wanafunzi wake, akawaambia, Na tuvuke mpaka ng’ambo ya ziwa. Wakatweka matanga. Nao walipokuwa wakienda, alilala usingizi. Ikashuka tufani juu ya ziwa, chombo kikaanza kujaa maji, wakawa katika hatari. Wakamwendea, wakamwamsha, wakisema, Bwana mkubwa, Bwana mkubwa, tunaangamia. Akaamka, akaukemea upepo na msukosuko wa maji, vikakoma; kukawa shwari. Akawaambia, Imani yenu iko wapi? Wakaogopa, wakamaka, wakisema wao kwa wao, Ni nani huyu basi hata anaamuru upepo na maji, navyo vyamtii?” (Luka 8:22-25).

Nimekutana na watu wengi wameanza safari zao za maisha (uchumba, ndoa, kazi, shule, nk.), na wamefika NJIANI wamekubwa na TUFANI, ghafla! Wanasema hii safari “haikuwa Mungu”; wanageuka, wanakimbia, au kurudi nyuma na kufuata NJIA zingine ambazo sio za Mungu; wanamtenda Mungu dhambi.

Bwana Yesu mwenyewe aliambia wanafunzi wake wapande chomboni ili wavuke ng’ambo, walijua wanakoelekea, walijua njia, na walikuwa na uhakika kwamba ni Bwana mwenyewe amewaagiza, safari imeanza, ghafla! Tufani hii hapa, wanakuwa katika HATARI ya kuangamia. Bwana alipoamka, alishughulika na tufani, kisha akawauliza “imani yeni iko wapi?” Jua neno hili, tufani na vurugu mbali mbali ni sehemu ya safari. Katika kila safari kutakuwa na tufani tu, hata kama Yesu yuko hapo unamwona kwa macho ya damu na nyama, tufani zitakuwepo siku zote, ili KUONESHA imani yako kwa Mungu na sio kukuangamiza. Sasa ukikosa MAARIFA utaangamia kwa hakika, japo sio kusudi.

Umewahi kufikiri Mungu anawatuma Musa na kundi lote la wana wa Israel kwenda NG’AMBO ya Yordan, na hawana hata mtumbwi? Nisikilize vizuri, hapakuwa na hata mmoja wao akiwemo Musa, aliyejua kwamba iko siku watakatiza baharini wakitembea pa kavu. Ndio maana wote walipofika ufukweni walichanganyikiwa, huku nyuma adui anakuja kuwaangamiza, Musa akamuuliza Mungu cha kufanya. Kazi ya Mungu maishani mwako ni kukuonesha matendo yake makuu na hujitukuza kwenye matatizo na vita zinazokukabili. Ukiona vita inakuja, jiandae kumwona Mungu akijitukuza, ila usisahau, “Mungu hujionesha mwenye nguvu kwa watu ambao mioyo yao imemwelekea”. Ukitumaini upanga wako na nguvu zako, adui zako watakumaliza kwa hakika, ukimtumaini Bwana, hakika utakuwa mshindi hata kama hujui kupigana vita, ila mtumaini, mwamini na moyo wako umwelekee tu, hicho ndicho anachotaka ili AJIONESHE mwenye nguvu kwako. Jina lake ni Bwana wa vita. Kupigana na kuokoa ndio kazi yake.

Angalia maisha yako, vita ulizokutana nazo, na tufani mbali mbali, na ujiulize, je! Ulimwita Bwana? Je! Ulitumia njia za Kimisri kutoka kwenye shida yako? Je! Ulitafuta faraja kwenye kambi ya adui kwa kumsujudia ili usipigane vita vyako vya imani? Endelea kukagua maisha yako na vita ulivyo pita, na ujiulize IMANI YAKO IKO WAPI?

Frank Philip.

Comments