JOSEPHAT MWINGIRA: JINSI NILIVYOTOKEWA NA BWANA YESU:SAFARI YA KWANZA YA MWINGIRA MBINGUNI.(2)

Photo: APOSTLE N PROPHET MWINGIRA
Na mtumishi wa MUNGU Mtume na Nabii Josephat Mwingira
BWANA YESU asifiwe ndugu zangu.

Leo tunaendelea na sehemu ya pili ya ushuhuda wa mtumishi wa MUNGU Josephat Mwingira, mbeba maono wa huduma ya Efatha yenye makanisa zaidi ya 200 hadi sasa.


leo tunaangalia Safari ya kwanza kwenda mbinguni kwa mtumishi huyu wa MUNGU, Maana MUNGU kwa neema yake unaweza kwenda popote katika ulimwengu wa roho, na kwangu mimi Peter hii naona ni neema ya ajabu mno na ni watumishi wachache sana ambao ambao nawafahamu ambao BWANA YESU aliwachukua mbinguni na kuwapa agizo, huu ni wito mkubwa na hii ni neema ya ajabu sana na kama hukusoma sehemu ya kwanza FUNGUA HAPA


karibu kwa sehemu ya pili ambayo ni maelezo ya mtumishi wa MUNGU Josephat Mwingira. 


Nilipofungua macho, nikaona mwanga mkali sana na katika mwanga ule niliwaona Malaika wengi sana, nikawa sioni mwisho wao. Basi nikasikia sauti inaita kutoka juu ikiwaamuru wale Malaika, ikisema “Njooni, mleteni huku”. Nikainua macho yangu juu, nikaona ngazi inatelemka mpaka pale chini nilipo. Akaja Malaika mmoja akanichukua. Wakati tunapanda nikaona kitu cha ajabu sana! Maana, kila nilipokuwa napanda na wale Malaika walikuwa wanapanda pamoja nami! Malaika walikuwa wengi sana. Nikaona mwanga mkali sana kule juu. Nikaanza kuogopa kwenda huko, nikawa nataka kurudi nyuma. Lakini nilipoangalia chini nikakuta, kumbe kila tulipopanda ngazi ya juu, zile ngazi za chini zilikuwa zinaondoka. Kwa hiyo nikabaini kuwa nisingeweza tena kurudi chini. Nikawa naendelea tu na safari pamoja na kwamba nilikuwa naogopa. Kwani nisingeliweza tena kurudi nyuma vinginevyo ningelidondoka na kuvunjika vunjika. Ikanibidi niendelee na safari. Nikapanda mpaka nikafika kule juu.
Malaika mmoja akaningoza, tukaenda mpaka tukafika kwenye lango. Tukaingia katika lile lango na kupelekwa moja kwa moja alikokuwako BWANA YESU. Nikaona watu wengi sana wako kule; siyo Malaika, ila ni watu wa kabila mbalimbali- waafrika na Wazungu. Sikuongea nao ila katika hali ya kuangalia angalia, nikawatambua Ibrahim, Musa na Eliya. Kulikuwa na hali ya kumwelewa kila niliyemwona kwamba ni Fulani na huyu ni Fulani. Kasha akanipeleka mpaka kwa BWANA YESU. 


Nakutana na BWANA YESU na MUNGU BABA


Nilipomwona tu, nikamtambua nikasema, “Ahaa… BWANA wangu!!” Akatabasamu, na mimi nikatabasamu. Ndipo akanikumbatia na kusema kitu Fulani ambacho, wakati huo, sikukifahamu maana yake. Nikawa namwangalia sana BWANA YESU kwa kuwa alikuwa anang’aa sana.

Kisha akaniita kwa jina langu akasema, “Josephat, twende huku.” Akimaanisha twende kwa BABA. Kabla hatujaanza safari hiyo, Yule Malaika aliyekuja kunichukua kule duniani, alisema, “Eee Josepahat, mtu upendwaye sana, umekusudiwa mema “BWANA YESU akanichukua, tuaanza safari ya kuelekea juu. Hata tulipofika kule juu, akanikumbatia tena na kusema, “Josephat, nilikutafuta sana ili nifanye yale ambayo niliyakusudia kabla hujazaliwa.” Kisha akanichukua na kunipeleka kwenye kiti cha Enzi, cha MUNGU BABA. Tukafika pale, lakini wakati tunakikaribia kiti hicho, sikuweza kukitazama maana kilikuea na ‘Utukufu wa ajabu’. Ndipo nikaangukia miguuni pake.

Nikawaona Makerubi na Maserafi- watu wenye macho yanayoona mbele, na nyuma, na pembeni. Pia wana asili ya mabawa. Huwezi kujificha kwao. Katikati ya hao Malaika ndipo amekaa MUNGU BABA ambaye anaonekana mfano wa mtu. Siyo mtu kama tulivyo sisi, lakini anaonekana kuwa tunafanana naye kabisa. Huwezi ukamuona uso (sura) yake na mavazi yake kwa sababu ya ; ‘Utukufu Mkuu’ unaomfunika. Yaani, mavazi yake yanaonekana kama ya dhahabu lakini si dhahabu, kama ya fedha lakini si fedha hayaelezeki!.

Kiti kile cha Enzi, ni kikubwa na kizuri ajabu. Nikaangalia, nikawaona Malaika wengi wakikizunguka pembeni. Lakini Makerubi walibaki pale pale. Nikawa naona Kiti cha Enzi kama kinacheza cheza hivi: nikasogea pale, lakini sikuweza kumwangalia BABA MUNGU usoni. Nikadondoka chini, miguuni pake. Basi wakaongea wenyewe kwa wenyewe, nikawasikia wakiwasiliana kati ya BABA MUNGU na YESU. BWANA YESU akamwambia BABA yake “Tumempata Yule tuliyekuwa tunamtafuta, atakayesimama kwa ajili yetu duniani na kwa ajili ya jamii ya watu walioko duniani, kwa kuwa ndiye atakayesimama kwa ajili ya KUSUDI”. Wakaendelea kuongea mimi nikiwa nimeishiwa nguvu kabisa, lakini nikawa nasikia yote waliyokuwa wanazungumza.


Moyo uliotayari kufa kwa ajili ya BWANA


Baadaye, alinigusa tena, naye akaniinua. Ama kweli, ule ‘Utukufu’ ulinimaliza kabisa! BWANA YESU akaniambia, “Twende”.
Wakati tunatembea tukielekea tulikokuwa tunakwenda, akaanza kuongea na mimi na kunieleza kwamba wengi aliotaka kuwatumia, walionyesha hali kama ya utayari, lakini walitumia uwepo wake kwa kusudi la Ki-binadamu. Kwa hiyo akasema, “Walitumia uwepo wa Ki-ungu kwa kusudi la Binadamu”. Halafu akasema, “Lakini wewe,” Yaani mimi Josephat “Umekusudiwa mema. Na tumeuangalia moyo wako na utakwenda kufanya yale yale tuliyokusudia. Tunaona moyo wako uko tayari kufa kwa ajili ya BWANA” mimi nikamuuliza niko tayari kufa kwa ajili yako?” YEYE akajibu, “MiMi ndiye asili ya hayo yote”. Sasa tukatoka pale tukiwa tunatembea kwenye njia nzuri sana, ya mfano wa dhahabu inayong’aa vizuri, yaani unaiona kama almasi lakini siyo almasi, dhahabu lakini siyo dhahabu. Yaani ni kuzuri sana. Ningeshauri kila mtu afike huko. Kama ingelikuwa inawezekana, hakika ningelichukua hata kanisa lote nilipeleke huko likaone uzuri ulioko huko. 

ITAENDELEAAAAA.....................

Usikose sehemu inayofuata hapa hapa Maisha ya ushindi blog pia unaweza kwenda Efatha na ukanunua kitabu hicho hapo chini ambacho ndio kina ushuhuda hu wote.
MUNGU akubariki sana na endelea kutembelea hapa



Comments