MAOMBI YA KILA SIKU YAMELETA MABADILIKO MAKUBWA NYUMBANI KWANGU






Mpendwa huyu katushirikisha ushuhuda toka inbox yetu ya facebook.

MAOMBI YA KILA SIKU YAMELETA MABADILIKO MAKUBWA NYUMBANI KWANGU
Ndugu,
Nakusalimuni katika jina la Yesu.
Nina ushuhuda ambao ningependa kuwashirikisha wapendwa.
Katika familia yetu tumekuwa tukiishi kama wakristo wengine ambavyo wamekuwa wakiishi. Kuna utofauti sana kwa kweli wa maisha ya Ukristo ya kumaanisha kumuishia Mungu na ule Ukristo wa mazoea. Tulizoea kwenda ibadani kama kawaida na kweli tumeokoka kwa sababu tumemwamini na kumkiri Yesu kama Bwana na Mwokozi wa maisha yetu. Lakini kuna jambo moja ambalo mume wangu alikuja kulifanya nyumbani limeleta mabadiliko makubwa sana katika familia yangu. Nalo ni MAOMBI YA KUMAANISHA YA KILA SIKU.
Mume wangu siku moja alikuja toka safari na kuleta mfumo mpya wa maombi na kujifunza neno la Mungu nyumbani. Hatukujua nini kilimtokea huko safarini mpaka akaja na mfumo huo. Lakini mfumo huo wa kuwa na maombi ya kila siku asbh na usiku na kujifunza neno kila siku hasa usiku na kuomba kumeleta mabadiliko makubwa sana katika familia yangu. Tumemuona Mungu kwanza akileta Amani na furaha kubwa sana katika familia yetu. Sio kwamba majaribu na misukosuko mingine ya maisha haitupitia, la hasha lakini inapotupitia neema ya Mungu imekuwa ikitufunika kwa kiwango kisicho cha kawaida. Maana maandiko yasema “Mungu ni mwaminifu; ambaye hatawaacha mjaribiwe kupita mwezavyo; lakini pamoja na lile jaribu atafanya na mlango wa kutokea, ili mweze kustahimili”. Kwa hiyo amekuwa akitustahimilisha tunapopita katika majaribu pia.
Lakini pia kwa maombi haya ya kila siku tumekuwa tukimwambia Bwana mahitaji yetu ya kila siku na Bwana amekuwa akifanya. Kweli tunamshukuru sana Mungu kwa kutusaidia katika program yetu ya maombi na kujifunza neno kila siku. Imeleta matokea chanya katika nyumba yetu. 
Mungu awabariki watumishi na tuendelee kuombeana.
Na pia napenda nimshukuru Mungu kwa kazi mnayoifanya ya kuineza injili hasa kwa kupitia mitandaoni.
Tungependa pia kuwaulizeni je tukiwakaribisha kwa ajili ya huduma kama semina na mikutano ya Injili mwaweza kuwa tayari kuja kuhudumu wapendwa?

Comments