Marian Bagamoyo Kuanzishwa chuo Kikuu


Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki Dar es Salaam Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo akiweka jiwe la Msingi la Chuo Kikuu Marian kinachotarajia kuanzishwa hivi karibuni.(Na Mpiga picha wetu)


KANISA Katoliki kupitia Shirika la Roho Mtakatifu ambalo ndilo linamiliki shule za Marian(wavulana/ wasichana) zilizoko Bagamoyo Jimbo Katoliki Morogoro, linaanzisha Chuo Kikuu cha Marian University College (MUCO) kwa lengo la kupata wataalamu wa sayansi nchini.
Makamu Mkuu wa Shirika hilo nchini Padri Florentin Mallya ameeleza kuwa, chuo kitaanza kama tawi la Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustino Tanzania (SAUT)  hadi hapo kitakapokamilisha hatua zote za kuwa chuo kikuu kinachojitegemea.

Ameeleza malengo ya kuanzisha chuo hicho kuwa ni kuendeleza mikakati ya serikali ambapo imeomba taasisi binafsi kuendeleza wataalamu wa sayansi ili kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazoendelea duniani.

“Huu ni mwendelezo wa taaluma inayotolewa katika shule ya Marian kwa upande wa wasichana na wavulana, ambapo wanafunzi wanafaulu kwa viwango vya juu, hivyo ni vyema wakaendelezwa katika elimu ya juu,” amesema Padri Mallya Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki Dar es Salaam Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo tayari ameshaweka jiwe la msingi la chuo hicho na wanatarajia kuanza kupokea wanafunzi Septemba mwaka huu huku kikiwa kinakamilisha ujenzi wa majengo hasa upande wa maabara ambayo wanatarajia kuyamaliza Julai mwaka huu. Makamu Mkuu huyo wa Shirika amesisitiza kuwa iwapo taifa halitakuwa na wataalamu waliyosomea masomo ya sayansi, nchi haitaweza kushindana kimaendeleo na nchi nyingine na nchi kuendelea kubaki nyuma kimaendeleo. “Baadhi ya wazazi wamekuwa wakihangaika kutafuta sehemu ya kuwapeleka watoto wao pindi wanapomaliza masomo yao kutokana na msingi bora wanaokuwa wamejengewa katika shule zetu,” ameeleza Padri Mallya. Hata hivyo uongozi wa Shirika la Roho Mtakatifu umeomba serikali kutoa ushirikiano katika juhudi zao za kuboresha elimu hapa nchini. Padri Mallya amesema kuwa iwapo wataungwa mkono, lengo lao la kuendelea kutoa elimu bora litaweza kukamilika kwani vijana wengi watapata elimu bora kutoka katika shule zao na chuo wanachokianzisha. “Sisi kama Shirika na Kanisa kwa ujumla tumeonyesha ushirikiano mzuri kwa serikali kwa kuanzisha shule za Marian kwa wasichana na wavulana ambazo zimekuwa zinatoa elimu bora kwa wanafunzi mbalimbali,” ameeleza huku akiongeza kuwa, “Serikali inatakiwa kutuunga mkono kama sisi tulivyoiunga mkono kwa kuanzisha shule zinazotoa elimu bora kwa wanafunzi wa kike na wakiume ili kupata viongozi bora katika nchi yetu,” Pia amewaomba wazazi kuendeleza ushirikiano wao ambao umepelekea Shirika hilo kufikia hatua hiyo ya kuanzisha chuo kikuu.

Comments