MTU AMBAYE ANA MAONO YA MUNGU.


BWANA YESU asifiwe.

Baada kifo cha Baba na Mama kutukimbia, tulichukuliwa na Bibi nikiwa na miaka 3 na nusu  tu, nikiwa pamoja na kaka yangu Samwel na mdogo wangu Kepha. Maisha awamu hii yalikuwa tofauti na mwanzo, tulihama kutoka Mwanza mjini na kwenda kuishi kijiji cha Kibehe wilaya ya Biharamulo mkoa wa kagera. Hali ilikuwa ni mbaya sana, kuna wakati nilidhani sikuzaliwa na watu bali nilirushwa tu na malaika wa MUNGU kutoka mbinguni ndio maana ninaishi.ilikuwa ni kipindi cha njaa. Babu kazi yake ilikuwa ni ulevi na akija nyumbani usiku ni kumpiga tu bibi na kupelekea kila mtu ndani ya nyumba kulia, kwangu mimi ilikuwa ni zaidi maana nilianza kuona aina ya maisha ambayo sitakiwi kuyaishi na nilijua natakiwa kuishi maisha Fulani. Kuna siku nikiwa peke yangu nilimwomba MUNGU kwamba naweka nadhiri na nadhiri hiyo ambayo nilimweleza MUNGU ilikuwa kwamba Kama MUNGU akinipa Kazi nzuri serikalini harafu akanipa Mke mzuri na akanipa Nyumba ya kumiliki mwenyewe basi mimi nitamtumikia MUNGU kama kichaa ili watu wote waokolewe. Nadhiri hiyo ilikuwa ni maono yangu na maono hayo kwa miaka zaidi ya 10 sauti yake ilikuwa inajirudia rudia ndani yangu hivyo nilijua lazima nitimize nadhiri yangu hiyo kwa MUNGU wangu.

Leo tunazungumzia maono.

Unapoacha maisha maovu na kumpa BWANA YESU maisha yako unapokea maisha mapya, maisha yaliyovuviwa na baada ya hapo utakuwa unatembea  na ROHO wa MUNGU ndani yako. Baada ya hapo utakuwa unapokea maono na maelekezo  kutoka kwa MUNGU.

Jua linapochomoza  huanza kuonekana kwanza mwanga mdogo kasha nuru kubwa huja baadae.

Mwanzo 12:1-3 (BWANA akamwambia Abramu, Toka wewe katika nchi yako, na jamaa zako, na nyumba ya baba yako, uende mpaka nchi nitakayokuonyesha; nami nitakufanya wewe kuwa taifa kubwa, na kukubariki, na kulikuza jina lako; nawe uwe baraka; nami nitawabariki wakubarikio, naye akulaaniye nitamlaani; na katika wewe jamaa zote za dunia watabarikiwa. ).

MUNGU anampa maono Ibrahimu na anamwonyesha kusudi lake.

MUNGU anamwonyesha Ibrahimu mambo yajayo ya Ibrahimu.

Kabla na hapo Ibrahimu hakujua anataka kupelekwa wapi lakini MUNGU alimwambia Ibrahimu kwamba atamfanya kuwa Baraka na katika yeye watu wote watabarikiwa.

Na ni kweli kabisa kupitia Ibrahimu watu wote hubarikiwa maana kupitia Ibrahimu BWANA YESU alikuja (Mathayo 1:1-Kitabu cha ukoo wa Yesu Kristo, mwana wa Daudi, mwana wa Ibrahimu. )  na kwa njia ya BWANA YESU watu wote watakaomwendea wataokolewa, Uzima wa milele ambayo ndio Baraka kuu kuliko zote itapatikana kupitia KRISTO pekee aliye Mwamba wa kabila la Yuda na yuda alitoka kwa Daudi na Daudi alitoka kwa Ibrahimu aliyepewa maono na MUNGU.

Mwanzo 15:1-6( Baada ya mambo hayo neno la BWANA likamjia Abramu katika njozi, likinena, Usiogope, Abramu, Mimi ni ngao yako, na thawabu yako kubwa sana. Abramu akasema, Ee BWANA MUNGU, utanipa nini, nami naenda zangu hali sina mtoto, na atakayeimiliki nyumba yangu ni huyu Eliezeri, Mdameski? Abramu akasema, Tazama, hukunipa uzao, na mtu aliyezaliwa nyumbani mwangu ndiye mrithi wangu.  Nalo neno la BWANA likamjia likinena, Huyu hatakurithi, bali atakayetoka katika viuno vyako ndiye atakayekurithi.  Akamleta nje, akasema, Tazama sasa mbinguni, kazihesabu nyota, kama ukiweza kuzihesabu. Akamwambia, Ndivyo utakavyokuwa uzao wako.  Akamwamini BWANA, naye akamhesabia jambo hili kuwa haki. ).

MUNGU anapompa mtu kitu humpa na uwezo na kuona kitu hicho halisi.

Tabia moja wapo ya  ni kwamba MUNGU anafanya kazi na mtu ambaye hazuiliwi na vitu vinavyoonekana.

2 Kor 4:18 ( tusiviangalie vinavyoonekana, bali visivyoonekana. Kwa maana vinavyoonekana ni vya muda tu; bali visivyoonekana ni vya milele. ).

Kitaalamu Sarah alikuwa ni tasa lakini MUNGU neno aliloliona husimama siku zote.

Kwetu usukumani zamani ilikuwa hivi. Watu waliogopa kupanda miti ya miembe maana tamaduni na mila zao zilisema kwamba kila apandaye mwembe hatakula matunda ya mwembe huo hadi kifo chake. Maana mwembe ukiupanda wewe  utachelewa sana kuzaa mbele zako hadi kifo chako, na ukitaka ule matunda ya mwembe ulioupanda wewe mwenyewe basi itokee uwe unaukata mwembe uliupanda mwenyewe  na mtu akukute ndio unaanza kuukata harafu akukataze kukata mwembe huo basi utakula matunda ya mwembe huo.

Hiyo ilikuwa ni desturi tu lakini vitu hivi vinavyoonekana viliwakwamisha wengi sana.

Na hii ni mfano wa vitu ambavyo vinavyoonekana ambavyo vinawakosesha wengi haki zao.

Hata wewe ndugu yawezekana kuna jambo ambalo hukukwamisha kuyatimiza maono yako ya utumishi wako kwa MUNGU.

MUNGU hapendi ukwamishwe na vitu unavyoviona ili kuyafikia maono au malengo aliyokupangia yeye.

Ona hapa hata baada ya Ibrahimu kuondoka, MUNGU aliendeleza kusudi lake kupitia Isaka mwanawe Mwanzo 25:11 (Ikawa, baada ya kufa kwake Ibrahimu, MUNGU akambariki Isaka mwanawe. Naye Isaka akakaa karibu ya Beer-lahai-roi. ).



Ili kufikia maono au malengo yake Ibrahimu. MUNGU alimwambia Ibarahimu ampe kwanza sadaka. Hapa kwenye sadaka kuna nzuri ambayo hata wewe unaweza kutumia ili kutimiza maono yako.

Usiiache ahadi ya MUNGU kwako.

MUNGU anamwambia Musa  ‘’Nenda kawachukue waisraeli uwapeleke katika nchi yao.’’

MUNGU atakuletea mchumba wako baada yaw ewe kukaa vizuri mbele zake na tena kama vitu vinanyoonekana havitakutisha.

Ukimpenda YESU utamtumikia na kwa kumtumikia utakuwa umejiepusha na hatari nyingi sana. 

Kwa leo naishia hapo, MUNGU akitupa nafasi tutajifunza tena siku nyingine.na kama hujampokea BWANA YESU muda wa kumpokea ni leo wala sio kesho, amua leo na atakuandika jina lako katika kitabu cha uzima na utaanza kuukulia wokovu kwa mafundisho kanisani. ROHO MTAKATIFU aliyenipa ujumbe huu ana makusudi kabisa na wewe, hataki upotelee motoni anataka uende uzimani aliko KRISTO BWANA.
                     MUNGU akubariki sana .
                      Ni mimi ndugu yako
                       Peter M Mabula
                 Maisha ya Ushindi Ministry.
                           0714252292

                 MUNGU akubariki sana uliyesoma somo hili.

Comments