MTUMISHI AU MWANAFUNZI WA KWELI WA YESU KRISTO NI HUYU.





BWANA YESU asifiwe ndugu.
Inawezekana unataka kumjua mtumishi au mwanafunzi wa kweli wa YESU KRISTO au yawezekana kabisa ni wewe mwenyewe unataka kujipima ili ujue kama kweli wewe ni mwanafunzi wa kweli wa BWANA YESU.
Biblia ina majibu ya shwari hili. Na jibu la swali hili ni muhimu kwa kila mtu duniani.
Kipindi cha mwanzo cha kuokoka kwangu nilikua na mitihani mingi maana haikua jambo rahisi kuacha kwa mara moja tabia ambazo nilizizoea kuzifanya tangu utotoni. Na mara nyingi niliamini MUNGU alikua anamueleza mchungaji wangu kila jambo baya ambalo nimefanya, kama nimesema uongo siku hiyo nikienda kanisani mahubiri yalilenga sana juu ya madhara ya uongo na hali hiyo ilinitisha na kuniogopesha sana lakini MUNGU alikua ananiwazia mema sana, kwa kufundishwa kanisani nilijigundua kabisa kwa wakati huo sikuwa mwanafunzi wa kweli wa YESU KRISTO bali nilikua najaribu tu kuwa mwanafunzi.  Neno la MUNGU lina majibu ya kujua kama wewe au mimi ni wanafunzi wa kweli wa BWANA YESU.
Ngoja nikupe sifa za mtu kuwa mwanafunzi au mtumishi wa kweli wa BWANA YESU.

MTUMISHI WA KWELI WA YESU NI HUYU.

     1.   Ni mtu ambaye anajifunza sana kuendelea katika maombi. Yakobo 5:13-16 (Mtu wa kwenu amepatikana na mabaya? Na aombe. Ana moyo wa kuchangamka? Na aimbe zaburi. Mtu wa kwenu amekuwa hawezi? Na awaite wazee wa kanisa; nao wamwombee, na kumpaka mafuta kwa jina la BWANA. Na kule kuomba kwa imani kutamwokoa mgonjwa yule, na BWANA atamwinua; hata ikiwa amefanya dhambi, atasamehewa. Ungameni dhambi zenu ninyi kwa ninyi, na kuombeana, mpate kuponywa. Kuomba kwake mwenye haki kwafaa sana, akiomba kwa bidii. )

    2.  Amejitoa kabisa kwa MUNGU ili MUNGU amtumie . Warumi 12:1-2 ( Basi, ndugu zangu, nawasihi, kwa huruma zake MUNGU, itoeni miili yenu iwe dhabihu iliyo hai, takatifu, ya kumpendeza MUNGU, ndiyo ibada yenu yenye maana. Wala msiifuatishe namna ya dunia hii; bali mgeuzwe kwa kufanywa upya nia zenu, mpate kujua hakika mapenzi ya MUNGU )

      3.  Mwanafunzi au mtumishi yeyote lazima awe ana kusudi katika maisha yake. Wafilipi 3:7-11 ( Lakini mambo yale yaliyokuwa faida kwangu, naliyahesabu kuwa hasara kwa ajili ya KRISTO. Naam, zaidi ya hayo, nayahesabu mambo yote kuwa hasara kwa ajili ya uzuri usio na kiasi wa kumjua KRISTO YESU, BWANA wangu; ambaye kwa ajili yake nimepata hasara ya mambo yote nikiyahesabu kuwa kama mavi ili nipate KRISTO; tena nionekane katika yeye, nisiwe na haki yangu mwenyewe ipatikanayo kwa sheria, bali ile ipatikanayo kwa imani iliyo katika KRISTO, haki ile itokayo kwa MUNGU, kwa imani; ili nimjue yeye, na uweza wa kufufuka kwake, na ushirika wa mateso yake, nikifananishwa na kufa kwake; ili nipate kwa njia yo yote kuifikia kiyama ya wafu. ).

      4.  Kwa neema ya MUNGU, BWANA ameondoa kila kikwazo ndani yake. Waebrania 12:1-2 (Basi na sisi pia, kwa kuwa tunazungukwa na wingu kubwa la mashahidi namna hii, na tuweke kando kila mzigo mzito, na dhambi ile ituzingayo kwa upesi; na tupige mbio kwa saburi katika yale mashindano yaliyowekwa mbele yetu,  tukimtazama YESU, mwenye kuanzisha na mwenye kutimiza imani yetu; ambaye kwa ajili ya furaha iliyowekwa mbele yake aliustahimili msalaba na kuidharau aibu, naye ameketi mkono wa kuume wa kiti cha enzi cha MUNGU. )

Taji ya miiba kichwani mwa BWANA YESU ilikuwa na maana ya kuweka akili ya ufalme wa MUNGU kwa wakristo ili wakilisikia neno la MUNGU lichome mioyo yao ili wapate akili za uzima ulio katika KRISTO ambaye ni neno juu ya neno.

BWANA YESU asifiwe.
Shahidi wa kwanza wa maisha ya mtu ni mtu mwenyewe, ndugu yangu liweke neno la MUNGU moyoni mwako na umpokee BWANA YESU ndipo utakuwa shahidi  mwaminifu  na ambaye ushahidi wake ni wa uzima.

Ewe mteule wa KRISTO
Ndani yako kuna mwenyeji mmoja tu yaani YESU KRISTO , lakini wageni ni wengi ambao ni vikwazo, dhambi na ukatishwaji tamaa lakini naomba utambue kwamba lengo la hao wageni ni kuhakikisha hauendi mbinguni, Ndugu yangu mwenyeji uliyempokea ana nguvu kuliko wageni wote na ukidumu na huyo mwenyeji ndani ya moyo wako una uzima wa milele ambao pekee unatoka kwake. Songa mbele na BWANA YESU na maadui watakimbia tu Warumi 3:23-26 ( kwa sababu wote wamefanya dhambi, na kupungukiwa na utukufu wa MUNGU; wanahesabiwa haki bure kwa neema yake, kwa njia ya ukombozi ulio katika KRISTO YESU; ambaye MUNGU amekwisha kumweka awe upatanisho kwa njia ya imani katika damu yake,ili aonyeshe haki yake ,kwa sababu ya kuziachilia katika ustahimili wa MUNGU dhambi zote zilzotangulia kufanywa. apate kuonyesha haki yake wakati huu, ili awe mwenye haki na mwenye kumhesabu haki yeye amwaminiye YESU. ).

  Kwa leo naishia hapo, MUNGU akitupa nafasi tutajifunza tena siku nyingine.na kama hujampokea BWANA YESU muda wa kumpokea ni leo wala sio kesho, amua leo na atakuandika jina lako katika kitabu cha uzima na utaanza kuukulia wokovu kwa mafundisha kanisani. ROHO MTAKATIFU aliyenipa ujumbe huu ana makusudi kabisa na wewe, hataki upotelee motoni anataka uende uzimani aliko KRISTO BWANA.
                     MUNGU akubariki sana .
                      Ni mimi ndugu yako
                       Peter M Mabula
                 Maisha ya Ushindi Ministry.
                           0714252292

                 MUNGU akubariki sana uliyesoma somo hili.

 MUNGU Akubariki.

Comments