NGUVU ILIYOMO NDANI YA FEDHA KIUONGOZI(2)

Na Mwl. Christopher Mwakasege
BWANA YESU asifiwe 
somo linaendelea na kama hukusoma sehemu ya kwanza FUNGUA HAPA 
Sehemu ya pili ya ujumbe huu kutoka kwa mtumishi wa MUNGU Mwl. Christopher Mwakasege inaanzia hapa.
karibu.

Mathayo 6: 21 Kwa tafsiri iliyo nyepesi kuielewa inasema: “fedha yako ilipo, ndipo utakapokuwapo na moyo wako”.
Hii inatupa kuona angalizo muhimu ndani ya mstari huu ya kwamba: Mtu mwenye pesa anaweza kutumia fedha yake kutawala mioyo ya watu. Au, tunaweza tukasema hivi: mtu mwenye fedha akitaka kutawala mahali, hahitaji yeye kuwapo pale, anapotaka kupatawala; bali anaweza kutuma pesa yake, na kwa fedha hiyo akatawala eneo hilo pamoja na viongozi wa pale.


 Je, unajua ya kwamba, kuna uwezekano kwa kiongozi kutumiwa na wenye fedha kutawala mioyo ya watu wake? Yesu alisema: “Hazina ya mtu ilipo, ndipo utakapokuwepo na moyo wake” (Mathayo 6: 21).
Neno hili ‘hazina’ limetumika hapa likiwa na maana ya ‘fedha’. Hii inatupa kujua ya kuwa, mfumo wa utawala wa kiuongozi anaoutumia kutawala na kuongoza watu wake, siyo wake, bali ni wa mtu mwenye fedha zinazolipia mfumo huo wa utawala wa kiongozi husika!
Kwa hiyo unaweza ukawa katika nafasi ya kiuongozi, na usiwe kiongozi, bali ukabaki kuwa chombo kilichowekwa na wenye fedha ili wakutumie kuongoza!


 Fedha ina uwezo wa kubeba kilichomo ndani ya mtoa fedha hizo. Hii ni kwa sababu, kufuatana na Mathayo 6: 21, moyo unafuata fedha ya mwenye moyo huo ilipo!
Yesu alisema: “Hazina (Fedha) yako ilipo, ndipo utakapokuwapo na moyo wako” (Mathayo 6: 21). Kwa hiyo nguvu ya fedha, inaweza kutumika kushawishi mpokea fedha, atumie misimamo ya mtoa fedha ili kufanya maamuzi yake!
Haitoshi tu kuwa mwangalifu na nguvu ya fedha katika kuleta maendeleo, bila ya pia kuangalia hiyo fedha imebeba moyo wa namna gani huko ilikotoka! Hii ni muhimu kwa sababu watumia fedha hizo, si tu watapokea msaada wa kimaendeleo, bali watapokea pia na misimamo ya kimaisha ya wale waliowapa fedha hizo.

 Kila kiongozi ni muhimu awe mwangalifu juu ya nguvu iliyomo ndani ya fedha zinazokuja kwake. Jambo hili ni muhimu kwake, kwa kuwa nguvu ya fedha akiitumia vizuri inaweza ikawa msaada katika maamuzi yake; lakini akiitumia vibaya inaweza ikaleta uharibifu mkubwa katika maamuzi yake, na kwa wale anaowaongoza.
Yesu alisema katika Mathayo 6: 21 kwa namna ambayo, a
litaka tujue ya kuwa, fedha ya mtu ina nguvu ya kuvuta na kubeba moyo wa mtu. Neno ‘moyo’ katika sentensi hiyo ya Yesu, lilikuwa na maana ya ‘nafsi’.


Kumbuka ndani ya nafsi mna maeneo mbalimbali kama: Nia, hisia, maamuzi, dhamiri na akili. Na vyote hivyo ni muhimu katika uongozi wa kiongozi. Lakini kwa kuwa vyote vimo ndani ya moyo, ina maana vinaweza kutawaliwa na fedha. Na fedha ikiwa imebeba moyo mbaya wa mtoaji fedha hizo, ina maana itaharibu utendaji kazi wa moyo wa mpokeaji na vyote vilivyomo ndani yake.


 Je, unajua ya kuwa kuna nguvu ndani ya fedha, inayoweza kuvuta upendo wa mtu? Biblia inasema katika 1Timotheo 6:10 ya kuwa: “Maana shina moja la mabaya ya kila namna ni kupenda fedha; ambayo wengine hali wakiitamani hiyo wamefarakana na Imani na kujichoma kwa maumivu mengi”
Kwa hiyo, mtu anaweza kupenda fedha! Au – kwa kuwa mtu anatumia moyo wake kupenda, ina maana ya kuwa moyo wa mtu unaweza ukaipenda fedha. Hii inatupa onyo ya kuwa katika kuitumia fedha, tusije tukajikuta tunaipenda fedha.
Fikiria kama kiongozi, au mtu anayetaka kuwa kiongozi, awe na moyo wa kuipenda fedha, uongozi wake utakuwaje! Kufuatana na 1Timotheo 6:10, utakuwa uongozi ulio “Shina la mabaya ya kila namna”. Ni nani anayetaka uongozi wake uwe na sifa mojawapo ya kuwa shina la mabaya ya kila namna? Nakuombea usiwe mpenda fedha!

 Fedha ina uwezo wa kuvuta upendo toka ndani ya moyo wa mtu! Huu ni upendo ambao ndani yake umejaa tamaa!
Hii ni kwa sababu: “Shina moja la mabaya ya kila namna ni kupenda fedha; ambayo wengine hali wakiitamani hiyo wamefarakana na Imani na kujichoma kwa maumivu mengi” (1Timotheo 6:10)
Ninalotaka ulione leo, ni kwamba upendo huu juu ya fedha, una tamaa ndani yake! Na tamaa hii inaweza ikamfanya mtu afarakane na Imani yake! Hii ina maana ukisukumwa na upendo huu wa kitamaa juu ya fedha, ni rahisi sana kujikuta Imani yako ya wokovu, au ya Ukristo – umekaa nayo mbali.


Imani yako katika Kristo ni mtaji mkubwa sana katika kufanikiwa kiuongozi – ikiwa utajua kuitumia ipasavyo! Kwa hiyo, Mungu awe msaada kwako katika kukuondolea kiu ya kuipenda fedha, ili usije ukafarakana na Imani yako!
Usiyumbishwe msimamo wako kiimani kwa sababu ya upendo ulionao juu ya fedha!

MUNGU akubariki sana.
Mwl. Christopher  Mwakasege. 

Somo hili litaendelea usikose sehemu ya mwisho.

Comments