NGUVU ILIYOMO NDANI YA FEDHA KIUONGOZI(3)

Na Mwl. Christopher Mwakasege
BWANA YESU asifiwe.
Karibu katika sehemu ya mwisho ya somo hili liitwalo NGUVU ILIYOMO NDANI YA FEDHA KIUONGOZI.
Najua umebarikiwa sana kwa sehemu ya kwanza na sehemu ya pili na hata hivyo wewe ambaye hukuisoma sehemu ya kwanza hii hapa FUNGUA HAPA Na sehemu ya pili ni hii hapa  FUNGUAHAPA

Kwa sehemu ya 3 na ambayo ni sehemu ya mwisho 

karibu.

Tusome pamoja 1Timotheo 6: 10; “Maana shina moja la mabaya ya kila namna ni kupenda fedha; ambayo wengine hali wakiitamani hiyo wamefarakana na Imani na kujichoma kwa maumivu mengi”
Ikiwa mtu anaweza kuipenda fedha, ina maana anaweza kujikuta anasema anampenda mtu huyo mwenye fedha, wakati kiuhakika kilichovuta huo upendo ni fedha aliyonayo, na wala si upendo kwake.


Hii ina maana fedha inaweza ikakuletea na kukukutanisha na watu ambao wanajifanya marafiki zako, lakini kwa kweli wamefuata kufanya urafiki na fedha uliyonayo!
Na marafiki wa jinsi hii unatakiwa uwe mwangalifu sana nao, maana urafiki wao baada ya muda, mara nyingi unakuwa “shina la mabaya ya kila namna”, na hata wakakufanya ufarakane na Imani, na kukuchoma na maumivu mengi!


 “Shina moja la mabaya ya kila namna ni kupenda fedha; ambayo wengine hali wakiitamani hiyo wamefarakana na Imani na kujichoma kwa maumivu mengi”. (1Timotheo 6: 10).

Mithali 14:20 inasema: “Maskini huchukiwa hata na jirani yake; bali tajiri ana rafiki wengi”.


Mithali 18:24 inasema: “Ajifanyiaye rafiki wengi ni kwa uangamivu wake mwenyewe…”
Mithali 19:4, 7 inasema: “Utajiri huongeza rafiki wengi; bali maskini hutengwa na rafiki yake. Ndugu wote wa maskini humchukia; jinsi gani rafiki zake huzidi kujitenga naye”.

 
Ikiwa wewe ni kiongozi au unataka uwe kiongozi, tafakari hii ya leo, ikupe kuwa mwangalifu juu ya uwezo wa fedha wa kukuchagulia marafiki…maana si wote wana nia nzuri!...au wewe huna nia hasa ya kujenga urafiki nao!


Je, wewe unavutwa na nini ukawa rafiki yao? Au wao wamevutwa na nini kwako wakawa rafiki zako?
Ukaribu wao kwako unazaa nini kwako? Je, unazaa “mabaya”? Je unakufanya upoe kiroho? Je, unazaa “mazuri”? Je unakuimarisha kiroho?
Hii ina maana hali yako ya utajiri au umaskini ina uwezo wa kukuchagulia marafiki!


 Ikiwa ‘kupenda fedha’ kunaweza kukamfanya mpenda fedha, afarakane na Imani yake, ina maana kupenda fedha kunaweza kupoozesha au kuua kabisa nguvu zake za maombi.

Tunasoma katika 1Timotheo 6:10 ya kuwa: “Shina moja la mabaya ya kila namna ni kupenda fedha, ambayo wengine hali wakiitamani hiyo wamefarakana na Imani na kujichoma kwa maumivu mengi”.
Jihadhari sana k
atika hili! Hasa unapokuwa kiongozi, na hata kama siyo kiongozi; na labda una mpango wa kuwa kiongozi baadaye! Ni rahisi sana unapokuwa na moyo wa kupenda fedha, moyo wa kumpenda Mungu unapoa, na hali yako ya kumtegemea Mungu kwa njia ya maombi inapungua, na hata wakati mwingine kupotea kabisa.


Unajikuta Imani na tegemeo lako la kupata majibu ya mahitaji yako, unaweka kwenye fedha na kwa wenye fedha badala ya Mungu!
Imeandikwa katika Mhubiri 10:19 kuwa: “…na fedha huleta jawabu la mambo yote”


Hata kama fedha inakuweza kujibu mahitaji yako, usiache ikaharibu uhusiano wako na Mungu katika maombi.

MUNGU akubariki.
Mwl. Christopher  Mwakasege. 

Comments