NGUVU ILIYOMO NDANI YA FEDHA KIUONGOZI ( 1)

Na Mwl. Christopher Mwakasege
"Nguvu iliyomo ndani ya fedha,inaweza kukusaidia au kukuharibia msimamo wako wa kiuongozi."
 Maswali ya Msingi ya kujiuliza: Kwanini kiongozi yeyote, asipokuwa na matumizi mazuri ya fedha anajikuta anapoteza nafasi yake ya kiuongozi?

Kwa nini kiongozi asipokuwa na matumizi mazuri ya fedha, huwa anajikuta anapoteza ile hali ya kuaminiwa na wale anaowaongoza?

Kumbuka, Imo nguvu ndani ya fedha inayoweza kuimarisha au kuharibu msimamo wa kiuongozi wa mtu.

Swali jingine la kujiuliza: Kwa nini mtu anapokuwa kiongozi, halafu hana matumizi mazuri ya fedha, pia anajikuta amepoteza sauti ya kimamlaka juu ya wale anaowaongoza?  Yes....na heshima yake kiuongozi inashuka au inaondoka mbele ya hao anaowaongoza....why??

Kumbuka; Ndani ya fedha kuna nguvu inayoweza kukusaidia uongozi wako ukaimarika au inaweza ikasababisha uongozi wako ukaharibika.

 Uongozi wa mtu kwenye maeneo mengine ya uongozi ukiwa mzuri lakini akaharibu kwenye eneo la fedha kwenye nafasi hiyo aliyopewa ya uongozi,ni vyepesi sana kwake kujikuta amepoteza kazi yake hiyo.

Eneo la fedha katika uongozi wa mtu likiwa dhaifu, linatosha kuwa sababu ya kumwondoa katika uongozi. Msimamo kama huu utaukuta katika jamii,katika biashara, katika serikali, katika ngazi za kimataifa na hata katika familia na katika vikundi mbalimbali
Kumbuka: Nguvu iliyomo katika fedha inaweza kuvuruga au kuimarisha uongozi wa mtu.


 Kutoka 18:21,22 inasema hivi: "Zaidi ya hayo utajipatia katika watu hawa watu walio na uwezo, wenye kumcha Mungu, watu wa kweli, wenye kuchukia mapato ya udhalimu,ukawaweka juu yao, wawe wakuu wa maelfu, na wakuu wa mia, na wakuu wa hamsini na wakuu wa kumi, nao wawaamue watu hawa siku zote kisha kila neno lililo kubwa watakuletea wewe,lakini kila neno dogo wataliamua wenyewe,basi kwako wewe mwenyewe utapata nafasi zaidi, nao watauchukua huo mzigo pamoja nawe."

Tunaona jinsi katika biblia uhusiano wa mtu na fedha ni kigezo kimoja wapo muhimu cha kumweka mtu katika nafasi ya uongozi.

 Swali lingine la kujiuliza tena, Kwa nini suala la uhusiano wa fedha na mtu, huwa halitumiki sana kama kigezo cha kumweka mtu katika uongozi?  ingawa kinatumika mara nyingi kama kigezo cha kumwondoa mtu kutoka kwenye nafasi yake ya kiuongozi?

Kumbuka: Ndani ya fedha imo nguvu inayoweza ikamfanya mtu apate nafasi ya uongozi au aipoteze nafasi ya uongozi aliyokuwa nayo!


 Hagai 2:8 inatuambia hivi; “Fedha ni mali yangu, na dhahabu ni mali yangu, asema Bwana wa majeshi”
Kwa kuwa fedha ni mali ya Mungu, kwa hiyo ni dhahiri anajua kusudi lililofanya ‘aiumbe’ fedha na itumike. Na kwa kuwa hivi ndivyo, anao uweza wa kukufundisha na kukusaidia uwe na uhusiano na fedha, ambao hautaharibu misimamo bora ya kiuongozi ndani yako.


Ndiyo maana tunakuhimiza usisahau kuongeza katika ajenda zako za maombi, kwamba Mungu akusaidie kujiandaa, na akusaidie uandaliwe ipasavyo katika eneo la fedha, kwa namna ambayo uongozi wako utakuwa na mafanikio makubwa.


 Hagai 2:8 inatueleza ya kwamba: “Fedha ni mali yangu, na dhahabu ni mali yangu, asema Bwana wa majeshi”.
Ikiwa Fedha ni mali ya Mungu na Mungu ni Roho, kwa hiyo fedha ni jambo la kiroho kabla halijawa la Kimwili. Tena kwa ajili hiyo, suala la uhusiano wa fedha na mtu, ni la kiroho kwanza, kabla halijawa la kitaalamu.


Je, unajua ya kuwa fedha ina nguvu kuliko moyo wa mtu? Yesu alisema katika Mathayo 6:21 hivi: “Kwa kuwa hazina yako ilipo, ndipo utakapokuwapo na moyo wako”.

Neno hili “hazina” limetumika hapa likiwa na maana mojawapo ya “fedha”. Kwa hiyo, fedha yako ilipo, ndipo utakapokuwapo na moyo wako! Kwa hiyo, moyo wako unafuata mahali fedha yako ilipo. Ikiwa moyo unafuata fedha, ina maana fedha ina nguvu kuliko moyo! Ndiyo maana fedha inaweza ikavuta moyo – na moyo ukaenda fedha ilipo!
Kufuatana na Mathayo 6:21 fedha ina nguvu kuliko moyo, maana Yesu alisema “hazina yako ilipo, ndipo utakapokuwapo na moyo wako”.
Kiuongozi ina maana ya kwamba, kuna uwezekano mtu akijikuta anaongoza kwa msukumo wa nguvu ya fedha, baada ya fedha kuubana moyo wake! Unaliona hili? Fedha ikitawala moyo wa kiongozi, uongozi wake utakaaje? Kwa hiyo, ni muhimu kwa kiongozi kuwa mwangalifu na fedha anayoipokea akiwa kiongozi, au anapotafuta nafasi ya uongozi – maana inaweza kuvuruga uongozi wake, au inaweza ikajenga uongozi wake.

MUNGU akubariki sana
By Mwl. Christopher Mwakasege.

SOMO LITAENDELEAAAAA.....   USIKOSE.

By Mwl. Christopher Mwakasege.

Comments