ONGEA NA MUNGU WAKO (1)




Ndugu,
baada ya kuona tunavyopaswa kuishi
kwa kusadiki, kuadhimisha na kupenda,
ni wakati wa kuzama katika fumbo la Mungu kwa njia ya sala.
Roho Mtakatifu, anayetuwezesha kusadiki, kuadhimisha na kupenda,
ndiye pia anayetuongoza katika sala hasa,
kama alivyowafanyia Yesu, Maria na umati wa wenzetu,
hata wasiofahamu kweli zote tulizofunuliwa na Mungu.
Nyuma yao hata wewe funga safari ya Kiroho
ya kuongea na Mungu aliye hai,
Baba, Mwana na Roho Mtakatifu,
kwa imani, tumaini na upendo mkubwa zaidi na zaidi.
Hakuna mwingine ambaye ni muhimu uongee naye
kuliko Mwenyezi Mungu, Muumba na Mwokozi wako.
Maisha yako yote, ya sasa na ya milele, yamo mikononi mwake:
unamtegemea kabisa upande wa mwili, tena zaidi upande wa roho.
La ajabu ni kwamba ana hamu ya kuongea nawe
kuliko wewe mwenyewe,
kwa kuwa anakupenda zaidi:
daima ndiye wa kwanza katika upendo.
Kwa nini usinyamaze mbele yake ili kusikiliza sauti yake ya fumbo?
Kwa nini usimuitikie kama Yesu alivyofanya?
Kwa nini usiache Roho Mtakatifu ndani mwako
amlilie na kusema naye kwa dhati,
akimuita Baba kwa niaba yako na ya viumbe vyote?
Hapa mbele utakuta baadhi ya maneno ya sala
yaliyobubujika mioyoni mwa watu wa Mungu,
wanaume kwa wanawake, karne hata karne.
1

Kwa hakika utamu wake utakusaidia kutambua
jinsi mafumbo ya imani yalivyo hai na ya kuvutia;
siyo nadharia ya dini iliyo mbali na maisha,
bali ndiyo kiini chake.
Zama ndani ya Mungu kwa kuongea naye:
hapo utazidi kuishi kwa utulivu na furaha ya dhati!
SALA KUTOKA BIBLIA
ABRAHAMU (Mwa 18:27)
Nimeshika kusema na Bwana, nami ni mavumbi na majivu tu.
YAKOBO (Mwa 32:26)
Sikuachi, usiponibariki!
MUSA (Kut 33:18)
Nakusihi unionyeshe utukufu wako.
GIDEONI (Amu 6:15)
       Ee Bwana, nitawaokoa Israeli kwa jinsi gani?
Tazama, jamaa zangu ndio walio maskini sana katika Manase,
 na mimi ndimi niliye mdogo katika nyumba ya baba yangu.
SAMWELI (1Sam 3:10)
Nena, Bwana, kwa kuwa mtumishi wako anasikia.
DAUDI (2Sam 7:18)
Mimi ni nani, Bwana Mungu, na nyumba yangu ni nini,
              hata umenileta hata hapa?
DAUDI (2Sam 24:17)
       Tazama, ni mimi niliyekosa, ni mimi niliyepotoka;
            lakini kondoo hawa, wamefanya nini?
Mkono wako na uwe juu yangu, na juu ya nyumba ya baba yangu!
DAUDI (1Nya 29:10-13)
2

   Uhimidiwe, Ee Bwana, Mungu wa Israeli baba yetu, milele na milele.
 Ee Bwana, ukuu ni wako, na uweza, na utukufu, na kushinda, na enzi;
          maana vitu vyote vilivyo mbinguni na duniani ni vyako.
Ufalme ni wako, Ee Bwana, nawe umetukuzwa, u mkuu juu ya vitu vyote.
  Utajiri na heshima hutoka kwako wewe, nawe watawala juu ya vyote;
                na mkononi mwako mna uweza na nguvu;
     tena mkononi mwako mna kuwatukuza na kuwawezesha wote.
    Basi sasa, Mungu wetu, twakushukuru na kulisifu jina lako tukufu.
SULEMANI (1Fal 3:9)
 Nipe mimi mtumwa wako moyo wa adili niwahukumu watu wako,
               na kupambanua mema na mabaya;
maana ni nani awezaye kuwahukumu hawa watu wako walio wengi?
SULEMANI (1Fal 8:23)
Ee Bwana, Mungu wa Israeli, hakuna Mungu kama wewe,
           mbinguni juu wala duniani chini!
  Ushikaye maagano na rehema kwa watumishi wako,
       waendao mbele zako kwa mioyo yao yote.
ELIYA (1Fal 18:36-37)
Ee Bwana, Mungu wa Ibrahimu, na wa Isaka, na wa Israeli,
na ijulikane leo ya kuwa wewe ndiwe Mungu katika Israeli,
            na ya kuwa mimi ni mtumishi wako,
 na ya kuwa nimefanya mambo haya yote kwa neno lako.
     Unisikie, Ee Bwana, unisikie, ili watu hawa wajue
           ya kuwa wewe, Bwana, ndiwe Mungu,
     na ya kuwa wewe umewageuza moyo wakurudie.
ELIYA (1Fal 19:4)
Yatosha! Sasa, Ee Bwana, uiondoe roho yangu;
 kwa kuwa mimi si mwema kuliko baba zangu.
YEREMIA (Yer 15:16)
        Maneno yako yalionekana, nami nikayala;
       na maneno yako yalikuwa ni furaha kwangu,
              na shangwe ya moyo wangu,
maana nimeitwa kwa jina lako, Ee Bwana, Mungu wa majeshi.
AZARIA (Dan 3:37-40)
3

      Sisi, Ee Bwana, tumekuwa duni kuliko maìtaifa mengine yote,
na kudhulumiwa leo katika ulimwengu wote kwa sababu ya dhambi zetu.
              Sasa hakuna mfalme wala nabii wala kiongozi;
         hakuna dhabihu wala kafara wala sadaka wala uvumba,
           wala mahali pa kukutolea dhabihu na kuona rehema.
Lakini kwa moyo uliovunjika na kwa roho nyenyekevu tukubaliwe nawe,
                  na sadaka yetu iwe machoni pako leo
               kama dhabihu za kondoo waume na ng’ombe,
                   na kama kondoo wanono elfu kumi.
Nasi tukufuate kwa unyofu, maana wanaokutumaini Wewe hawataaibika.
VIJANA WATATU (Dan 3:52-56)
    Umehimidiwa, Ee Bwana, Mungu wa baba zetu,
      wastahili kusifiwa na kuadhimishwa milele.
       Limehimidiwa jina lako takatifu, tukufu.
      lastahili kusifiwa na kuadhimishwa milele.
  Umehimidiwa katika hekalu la fahari yako takatifu,
        wastahili kusifiwa na kutukuzwa milele.
      Umehimidiwa juu ya kiti cha ufalme wako.
      wastahili kusifiwa na kuadhimishwa milele.
Umehimidiwa utazamaye vilindi, uketiye juu ya makerubi,
      wastahili kusifiwa na kuadhimishwa milele.
        Umehimidiwa katika anga la mbinguni,
        wastahili kusifiwa na kutukuzwa milele.
BIBI ARUSI (Wim 8:6-7)
              Nitie kama muhuri moyoni mwako,
               kama muhuri juu ya mkono wako;
          kwa maana upendo una nguvu kama mauti,
                 na wivu ni mkali kama ahera.
                Mwako wake ni mwako wa moto,
                na miali yake ni miali ya Bwana.
           Maji mengi hayawezi kuuzimisha upendo,
                 wala mito haiwezi kuuzamisha.
Kama mtu angetoa badala ya upendo mali yote ya nyumbani mwake,
                    angedharauliwa kabisa.
KUJIOMBEA HEKIMA (Hek 9:1-6)
Ee Mungu wa baba zetu, Bwana, mwenye kuihifadhi rehema yako,
             umevifanya vitu vyote kwa neno lako;
       na kwa Hekima yako ukamwumba mwanadamu,
           ili avitawale viumbe vilivyoumbwa nawe,
4

       na kumiliki ulimwengu katika utakatifu na kwa haki,
             na kutoa hukumu kwa unyofu wa moyo.
                      Nakusihi unipe Hekima,
      ambayo huketi karibu nawe katika kiti chako cha enzi,
      wala usinikatae mimi miongoni mwa watumishi wako;
     mimi niliye mtumwa wako, na mwana wa mjakazi wako,
                 mtu dhaifu asiye na siku nyingi,
        wala sina nguvu ya kufahamu hukumu na sheria.
Kwa maana mtu ajapokuwa ni mkamilifu miongoni mwa wanadamu,
     pasipo Hekima itokayo kwako atahesabiwa kuwa si kitu.
ZABURI YA 8
             Wewe, Mungu, Bwana wetu,
   jinsi lilivyo tukufu jina lako duniani mwote!
    Wewe umeuweka utukufu wako mbinguni.
Vinywani mwa watoto wachanga na wanyonyao
             umeiweka misingi ya nguvu;
      kwa sababu yao wanaoshindana nawe;
       uwakomeshe adui na mijilipiza kisasi.
Nikiziangalia mbingu zako, kazi ya vidole vyako,
          mwezi na nyota ulizoziratibisha;
        mtu ni kitu gain hata umkumbuke,
          na binadamu hata umwangalie?
    Umemfanya mdogo punde kuliko Mungu;
      umemvika taji ya utukufu na heshima;
    umemtawaza juu ya kazi za mikono yako;
     umevitia vitu vyote chini ya miguu yake.
           Kondoo, na ng’ombe wote pia;
          naam, na wanyama wa kondeni;
    ndege wa angani, na samaki wa baharini;
         na kila kipitiacho njia za baharini.
             Wewe, Mungu, Bwana wetu,
  Jinsi lilivyo tukufu jina lako duniani mwote!
ZABURI YA 123
  Nimekuinulia macho yangu, wewe uketiye mbinguni.
Kama vile macho ya watumishi kwa mkono wa bwana zao;
   kama macho ya mjakazi kwa mkono wa bibi yake;
   hivyo macho yetu humlekea Bwana, Mungu wetu,
                 hata atakapoturehemu.
         Uturehemu, Ee Bwana, uturehemu sisi,
             kwa maana tumeshiba dharau.
      Nafsi zenu zimeshiba mzaha wa wenye raha,
               na dharau ya wenye kiburi.
5

ZABURI YA 130
       Ee Bwana, toka vilindini nimekulilia;
            Bwana, uisikie sauti yangu.
 Masikio yako na yaisikilize sauti ya dua zangu.
    Bwana, kama Wewe ungehesabu maovu,
          Ee Bwana, nani angesimama?
Lakini kwako kuna msamaha, ili Wewe uogopwe.
  Nimemngoja Bwana, roho yangu imemngoja,
           na neno lake nimelitumainia.
         Nafsi yangu inamngoja Bwana,
       kuliko walinzi waingojavyo asubuhi,
       naam, walinzi waingojavyo asubuhi.
           Ee Israeli, umtarajie Bwana;
         maana kwa Bwana kuna fadhili,
        na kwake kuna ukombozi mwingi.
Yeye atawakomboa Israeli na maovu yake yote.
BIKIRA MARIA (Lk 1:38)
Tazama, mimi ni mjakazi wa Bwana;
 na iwe kwangu kama ulivyosema.
SIMEONI (Lk 2:29-32)
   Sasa, Bwana, wamruhusu mtumishi wako,
         kwa amani, kama ulivyosema;
kwa kuwa macho yangu yameuona wokovu wako,
    uliouweka tayari machoni pa watu wote;
      nuru ya kuwa mwangaza wa Mataifa,
     na kuwa utukufu wa watu wako Israeli.
YOHANE MBATIZAJI (Math 3:14)
Mimi nahitaji kubatizwa na wewe, nawe waja kwangu?
MKOMA (Mk 1:40)
Ukitaka, waweza kunitakasa.
MWANAMKE MSAMARIA (Yoh 4:15)
Bwana, unipe maji hayo, nisione kiu, wala nisije hapa kuteka.
WAGALILAYA (Yoh 6:34)
6

Bwana, sikuzote utupe chakula hiki.
MWANDISHI (Math 8:19)
Mwalimu, nitakufuata kokote uendako.
WANAFUNZI WA YESU (Math 8:25)
Bwana, tuokoe, tunaangamia.
    PEPO (Mk 5:7,12)
Nina nini nawe, Yesu, Mwana wa Mungu aliye juu?
       Nakuapisha kwa Mungu usinitese...
Tupeleke katika nguruwe, tupate kuwaingia wao.
MWANAMKE MKANANAYO (Math 15:22,25,27)
          Unirehemu, Bwana, Mwana wa Daudi.
          Binti yangu amepagawa sana na pepo.
                    Bwana, unisaidie.
Hata mbwa hula makombo yaangukayo mezani pa bwana zao.
PETRO (Mk 9:5)
Rabi, ni vizuri sisi kuwapo hapa; na tufanye vibanda vitatu,
kimoja chako wewe, kimoja cha Musa, na kimoja cha Eliya.
BABA WA MTOTO ALIYEPAGAWA (Mk 9:24)
Naamini, nisaidie kutokuamini kwangu.
MWANAFUNZI WA YESU (Lk 11:1)
           Bwana, tufundishe sisi kusali,
kama vile Yohane alivyowafundisha wanafunzi wake.
MTOZAUSHURU (Lk 18:13)
Ee Mungu, uniwie radhi mimi mwenye dhambi.
KIJANA TAJIRI (Mk 10:17)
Mwalimu mwema, nifanye nini nipate kuurithi uzima wa milele?
BARTIMAYO (Mk 10:47,48,51)
7

 Mwana wa Daudi, Yesu, unirehemu!
   Mwana wa Daudi, unirehemu!
Mwalimu wangu, nataka nipate kuona.
MARTHA (Yoh 11:21-22,27)
  Bwana, kama ungalikuwapo hapa, ndugu yangu hangalikufa.
Lakini hata sasa najua ya kuwa yoyote utakayomwomba Mungu,
                       Mungu atakupa...
Naam, Bwana, mimi nimesadiki ya kwamba wewe ndiwe Kristo,
           Mwana wa Mungu, yule ajaye ulimwenguni.
MHALIFU (Lk 23:42)
Ee Yesu, nikumbuke utakapoingia katika ufalme wako.
YESU (Math 11:25-26)
    Nakushukuru, Baba, Bwana wa mbingu na nchi,
kwa kuwa mambo haya uliwaficha wenye hekima na akili,
           ukawafunulia watoto wachanga.
Naam, Baba, kwa kuwa ndivyo ilivyopendeza mbele zako
YESU (Yoh 11:41-42)
            Baba, nakushukuru kwa kuwa umenisikia.
        Nami nalijua ya kuwa wewe wanisikia sikuzote;
lakini kwa ajili ya mkutano huu wanaohudhuria nalisema haya,
        ili wapate kusadiki kwamba ndiwe uliyenituma.
YESU (Yoh 17:1-26)
                       Baba, saa imekwisha kufika.
        Mtukuze Mwanao, ili Mwana wako naye akutukuze wewe;
        kama vile ulivyompa mamlaka juu ya wote wenye mwili,
            ili kwamba wote uliompa awape uzima wa milele.
                      Na uzima wa milele ndio huu:
 wakujue wewe, Mungu wa pekee wa kweli, na Yesu Kristo uliyemtuma.
 Mimi nimekutukuza duniani, hali nimeimaliza kazi ile uliyonipa niifanye.
               Na sasa, Baba, unitukuze mimi pamoja nawe,
kwa utukufu ule niliokuwa nao pamoja nawe kabla ya ulimwengu kuwako.
   Jina lako nimewadhihirishia watu wale ulionipa katika ulimwengu;
       walikuwa wako, ukanipa mimi, na neno lako wamelishika.
          Sasa wamejua ya kuwa yote uliyonipa yatoka kwako.
                Kwa kuwa maneno uliyonipa nimewapa wao;
8

         nao wakayapokea, wakajua hakika ya kuwa nalitoka kwako,
                wakasadiki ya kwamba wewe ndiwe uliyenituma.
                   Mimi nawaombea hao; siuombei ulimwengu;
                       bali hao ulionipa, kwa kuwa hao ni wako;
            na wote walio wangu ni wako, na walio wako ni wangu;
                                nami nimetukuzwa ndani yao.
                           Wala mimi simo tena ulimwenguni,
               lakini hawa wamo ulimwenguni, nami naja kwako.
            Baba mtakatifu, kwa jina lako ulilonipa uwalinde hawa,
                          ili wawe na umoja kama sisi tulivyo.
                                 Nilipokuwapo pamoja nao,
             mimi naliwalinda kwa jina lako ulilonipa, nikawatunza;
                      wala hapana mmojawapo wao aliyepotea,
                   ila yule mwana wa upotevu, ili andiko litimie.
                                     Na sasa naja kwako;
                       na maneno haya nayasema ulimwenguni,
                ili wawe na furaha yangu imetimizwa ndani yao.
           Mimi nimewapa neno lako, na ulimwengu umewachukia,
  kwa kuwa wao si wa ulimwengu, kama mimi nisivyo wa ulimwengu.
                Mimi siombi kwamba uwatoe katika ulimwengu;
                                bali uwalinde na yule mwovu.
          Wao si wa ulimwengu, kama mimi nisivyo wa ulimwengu.
                Uwatakase kwa ile kweli; neno lako ndiyo kweli.
                     Kama vile ulivyonituma mimi ulimwenguni,
                 nami vivyo hivyo naliwatuma hao ulimwenguni.
                    Na kwa ajili yao najiweka wakfu mwenyewe,
                            ili na hao watakaswe katika kweli.
                               Wala si hao tu ninaowaombea;
            lakini na wale watakaoniamini kwa sababu ya neno lao.
                                    Wote wawe na umoja;
           kama wewe, Baba, ulivyo ndani yangu, nami ndani yako,
                                  hao nao wawe ndani yetu,
    ili ulimwengu upate kusadiki ya kwamba wewe ndiwe uliyenituma.
                      Nami utukufu ule ulionipa nimewapa wao,
                     ili wawe na umoja kama sisi tulivyo umoja.
Mimi ndani yao, nawe ndani yangu, ili wawe wamekamilika katika umoja;
                 ili ulimwengu ujue ya kuwa ndiwe uliyenituma,
                    ukawapenda wao kama ulivyonipenda mimi.
        Baba, hao ulionipa nataka wawe pamoja nami popote nilipo,
                 wapate na kuutazama utukufu wangu ulionipa;
        kwa maana ulinipenda kabla ya kuwekwa msingi ulimwengu.
                    Baba mwenye haki, ulimwengu haukukujua;
   lakini mimi nalikujua, na hao wamejua ya kuwa ndiwe uliyenituma.
              Nami naliwajulisha jina lako, tena nitawajulisha hilo,
  ili pendo lile ulilonipenda mimi liwe ndani yao, nami niwe ndani yao.
9

YESU (Mk 14:36)
Aba, Baba, yote yawezekana kwako; uniondolee kikombe hiki;
   walakini, si kama nitakavyo mimi, bali utakavyo wewe.
YESU (Mk 15:34)
                Eloi, Eloi, lama sabakthani?
(maana yake, Mungu wangu, Mungu wangu, mbona umeniacha?)
YESU (Lk 23:46)
Ee Baba, mikononi mwako naiweka roho yangu.
MARIA MAGDALENA (Yoh 20:16)
          Raboni!
(maana yake, Mwalimu wangu!)
TOMA (Yoh 20:28)
Bwana wangu na Mungu wangu!
PETRO (Yoh 21:17)
     Bwana, wewe wajua yote;
wewe umetambua ya kuwa nakupenda.
KANISA LA YERUSALEMU (Mdo 4:24-30)
                       Bwana, wewe ndiwe Mungu,
   ndiwe uliyefanya mbingu na nchi na bahari na vitu vyote vilivyomo;
                    nawe ulinena kwa Roho Mtakatifu
             kwa kinywa cha babaetu Daudi, mtumishi wako:
                    Mbona mataifa wamefanya ghasia,
                    na makabila wametafakari ubatili?
                     Wafalme wa dunia wamejipanga,
na wakuu wamefanya shauri pamoja juu ya Bwana na juu ya Kristo wake.
                 Maana ni kweli, Herode na Pontio Pilato
                  pamoja na Mataifa na watu wa Israeli,
                       walikusanyika katika mji huu
        juu ya Mtumishi wako mtakatifu Yesu, uliyemtia mafuta,
        ili wafanye yote ambayo mkono wako na mashauri yako
                   yamekusudia tangu zamani yatokee.
                Basi sasa, Bwana, yaangalie matisho yao;
     ukawajalie watumwa wako kunena neno lako kwa ujasiri wote,
10

                  ukinyosha mkono wako kuponya;
ishara na maajabu vifanyike kwa jina la Mtumishi wako mtakatifu Yesu.
STEFANO (Mdo 7:59-60)
Bwana Yesu, pokea roho yangu…
Bwana, usiwahesabie dhambi hii.
PAULO (Mdo 22:10)
Nifanye nini, Bwana?
WAZEE 24 MBINGUNI (Ufu 4:11)
        Umestahili wewe, Bwana wetu na Mungu wetu,
          kuupokea utukufu na heshima na uweza,
        kwa kuwa wewe ndiwe uliyeviumba vitu vyote,
na kwa sababu ya mapenzi yako vilikuwako, navyo vikaumbwa.
WENYE UHAI 4 NA WAZEE 24 MBINGUNI (Ufu 5:9-10)
Wastahili wewe kukitwaa hicho kitabu na kuzifungua muhuri zake;
   kwa kuwa ulichinjwa, ukamnunulia Mungu kwa damu yako
          watu wa kila kabila na lugha na jamaa na taifa,
   ukawafanya kuwa ufalme na makuhani kwa Mungu wetu;
                   nao wanamiliki juu ya nchi.
WAFIADINI MBINGUNI (Ufu 6:10)
        Ee Mwenyezi, Mtakatifu, Mwenye kweli,
hata lini kutokuhukumu, wala kuipatia haki damu yetu
              kwa hao wakaao juu ya nchi?
WAZEE 24 MBINGUNI (Ufu 11:17-18)
Tunakushukuru wewe, Bwana Mungu Mwenyezi, uliyeko na uliyekuwako,
      kwa sababu umeutwaa uweza wako ulio mkuu, na kumiliki.
           Na mataifa walikasirika, hasira yako nayo ikaja,
             na wakati ukaja wa kuhukumiwa waliokufa,
  na wa kuwapa thawabu yao watumwa wako manabii na watakatifu,
          na hao walichao jina lako, wadogo kwa wakubwa,
               na wa kuwaharibu hao waiharibuo nchi.
WASHINDI MBINGUNI (Ufu 15:3-4)
Ni makuu, na ya ajabu, matendo yako, Ee Bwana Mungu Mwenyezi;
11

 Ni za haki, na za kweli, njia zako, Ee Mfalme wa mataifa.
  Ni nani asiyekucha, Ee Bwana, na kulitukuza jina lako?
          Kwa kuwa wewe peke yako u Mtakatifu;
kwa maana mataifa yote watakuja na kusujudu mbele zako;
 kwa kuwa matendo yako ya haki yamekwisha kufunuliwa.
ROHO MTAKATIFU NA BIBIARUSI (Ufu 22:20)
Na uje, Bwana Yesu!
ITAENDELEAAAAA............
MUNGU akubariki sana.
By Dickson Haji.

Comments