ONGEA NA MUNGU WAKO (2)





SALA ZA WANAKANISA KARNE KWA KARNE
MWANDISHI WA DIDAKEE (80 hivi)
                    Tunakushukuru, Baba yetu,
      kwa mzabibu mtakatifu wa Daudi mtumishi wako,
            uliotujulisha kwa njia ya Kristo Mwanao.
                  Utukufu ni wako hata milele…
   Kama vile mkate huu uliomegeka ulitawanyika vilimani,
         nao kisha kukusanywa umekuwa kitu kimoja,
 vivyo hivyo Kanisa lako likusanywe toka mipaka ya dunia
                        katika ufalme wako:
              kwa kuwa utukufu na nguvu ni vyako
              kwa njia ya Yesu Kristo hata milele…
                Tunakushukuru, Baba mtakatifu,
                  kwa ajili ya jina lako takatifu,
                ulilolifanya likae mioyoni mwetu,
  na pia kwa ajili ya ujuzi, imani na uzima usio na mwisho
           ulivyotufunulia kwa njia ya Yesu Mwanao.
                  Utukufu ni wako hata milele.
Wewe, Baba mwenyezi, uliviumba vyote kwa ajili ya jina lako,
   ukawajalia wanadamu chakula na kinywaji ili wakusifu;
  lakini sisi umetuneemesha chakula na kinywaji cha kiroh
     na cha uzima wa milele kwa njia ya Yesu Mwanao.
       Kwanza tunakushukuru kwa kuwa u Mwenyezi.
                  Utukufu ni wako hata milele.
                Ulikumbuke, Bwana, Kanisa lako,
 uliokoe na kila uovu na kulikamilisha katika upendo wako,
            Ulitakase na kulikusanya toka pepo nne
                katika ufalme wako uliloliandalia;
         kwa kuwa nguvu na utukufu ni vyako milele.
     Neema ya Mungu itufikie na ulimwengu huu upite.
                    Hosana, Mwana wa Daudi!
         Aliye mtakatifu aje, na asiye hivyo aongoke.
12

Maranatha! Amina!
MT. KLEMENTI I (30-96)
Wewe umefunua macho ya mioyo yetu, ili tukujue wewe Mungu pekee,
                 uliye juu sana katika mbingu za juu,
                mtakatifu unayekaa kati ya watakatifu,
          ambaye unanyenyekeza ufidhuli wao wenye kiburi,
                  unabatilisha mashauri ya mataifa,
      unawainua juu wanyonge na kuwashusha wanaojikweza,
    wewe ambaye unatajirisha na kufukarisha, unaua na kuhuisha,
                  ambaye peke yako unafadhili roho
              na ni Mungu pekee wa kila mwenye mwili,
      unatazama vilindi, unachunguza matendo ya wanadamu,
  unawasaidia waliopo hatarini na ni mkombozi wa waliokata tamaa,
               ni muumbaji na mtunzaji wa roho zote,
                      unazidisha mataifa duniani,
         ambaye kati ya wote umewachagua wanaokupenda,
              kwa njia ya Yesu Kristo Mwanao mpendwa,
 ambaye kwa njia yake umetulea, umetutakasa na kutuvika heshima.
        Tunakusihi, Bwana, uwe kwetu msaidizi na tegemeo.
     Uwakomboe walio taabuni kati yetu, uwahurumie wanyonge,
           uwainue walioanguka, ujidhihirishe kwa wahitaji,
     uwaponye wagonjwa, uwarudishe waliojitenga na taifa lako,
        uwashibishe wenye njaa, uwafungue wafungwa wetu,
            uwaimarishe walio dhaifu, uwatulize walio duni.
 Mataifa yote wapate kujua ya kuwa ndiwe Mungu, wewe peke yako,
                  na ya kuwa Yesu Kristo ni Mwanao
           nasi tu wako wako na kondoo wa malisho yako.
MT. POLIKARPO (70-155)
                    Ee Bwana, Mwenyezi Mungu,
        Baba wa Mwanao mpenzi na mbarikiwa Yesu Kristo,
                ambaye kwa njia yake tumekufahamu;
      Mungu wa malaika na wa wenye uwezo, wa kila kiumbe
      na wa kizazi chote cha waadilifu wanaoishi mbele yako:
      mimi nakubariki kwa kuwa siku hii na saa hii umenijalia
   nishiriki kikombe cha Kristo wako pamoja na wafiadini wote,
     kwa ufufuo wa roho na wa mwili katika uzima wa milele,
      katika hali ya kutoharibika kwa njia ya Roho Mtakatifu.
           Niweze leo kupokewa pamoja nao mbele yako
                 kama sadaka nono na ya kupendeza,
kama vile wewe, Mungu usiye na hila na msemakweli, ulivyoiandaa
             ukanionyesha mapema na sasa umeitimiza.
 Kwa sababu hiyo na kwa mambo yote mimi nakusifu, nakuhimidi,
13

nakutukuza pamoja na kuhani wa milele na wa kimbingu Yesu Kristo,
Mwanao mpenzi, ambaye kwa njia yake kwako na kwa Roho Mtakatifu
            uwe utukufu sasa na nyakati zijazo. Amina.
ORIGEN (185-253)
                  Yesu, miguu yangu ni michafu.
 Njoo kama mtumwa kwangu, mimina maji katika beseni yako,
                     njoo unitawadhe miguu.
         Ninapoomba hivyo najua kuwa nathubutu mno,
          lakini naogopa tishio lililotolewa uliponiambia,
         “Nisipokutawadha miguu, huna ushirika nami”.
Basi, osha miguu yangu, kwa kuwa naonea shauku urafiki wako.
MT. HILARI (315-367)
                   Mungu, Baba Mwenyezi, najua vema kuwa
      huduma kuu inayonipasa kwako katika maisha yangu ni kwamba
                   kila neno na wazo langu liseme juu yako.
       Kipawa cha kusema ulichonijalia hakiwezi kunipa furaha kubwa
                     kuliko ile ya kukutumikia kwa kuhubiri
na kuonyesha kwa ulimwengu usiokujua, au kwa mzushi anayekukanusha,
      jinsi ulivyo, yaani Baba, Baba ambaye Mwanae pekee ni Mungu.
         Lakini kwa kusema haya, nasema tu ninachotaka kufanya.
Ili niweze kukifanya kweli nahitaji kuomba msaada wako na huruma yako,
          kuomba ujaze upepo tanga nilizozipandisha kwa ajili yako
                 na uzisukume mbele katika mwendo wangu,
    yaani umvuvie Roho wako katika imani yangu na katika kuiungama,
               na uniwezeshe kuendelea mahubiri niliyoyaanza…
  Acha niseme nawe, Mwenyezi Mungu, ingawa ni mavumbi na majivu tu,
          acha niseme kwa uhuru kwa kuwa nimefungamana nawe
                            kwa vifungo vya upendo.
                      Kabla sijakufahamu nilikuwa si kitu.
           Nilikuwa na bahati mbaya ya kutojua maana ya maisha,
           nilikuwa sijielewi, nilikuwa tofauti kabisa na jinsi nilivyo.
                       Huruma yako ndiyo iliyonipa uhai…
        Muda wote ambao nitaishi na kupumua kwa pumzi uliyonipa,
    Baba Mtakatifu, Mwenyezi Mungu, nitakiri kwamba tangu milele yote
                        wewe si Mungu tu, bali Baba pia.
          Sitakuwa kamwe na kichaa na uovu wa kujifanya hakimu
          wa uwezo wako usio na mipaka, wala wa mafumbo yako,
           hata nipendelee wazo langu maskini kuliko yale ambayo
                 dini inakiri juu ya ukuu wako usio na mipaka
                  au imani inafundisha kuhusu umilele wake…
               Nakuomba, utunze salama imani hiyo uliyonijalia,
       na kunifadhilia kwamba muda wote wa maisha yangu niweze tu
14

  kuzingatia yale ambayo dhamiri yangu inasema juu yake.
Niweze daima kushika imani niliyoiungama nilipozaliwa upya,
       Nishike ungamo lake nililolitamka nilipobatizwa
    kwa jina la Baba, na la Mwana na la Roho Mtakatifu.
            Niweze kukuabudu wewe, Baba yetu,
           na kumuabudu Mwanao pamoja nawe;
  niweze kuwa jinsi Roho wako Mtakatifu anavyotaka niwe,
      yeye atokaye kwako kwa njia ya Mwanao pekee.
MT. EFREM (306-373)
Mwokozi wetu, msalaba wako ulikomesha uhai wa mwili.
         Utujalie tusulubishe kiroho nafsi yetu.
Ufufuko wako, Yesu, ukuze utu wa kiroho ndani mwetu…
     Umbile duni la mwili wetu linatuelekeza kufa.
      Mimina juu yetu upendo wako wa Kimungu,
  ufute moyoni mwetu matokeo ya sisi kuelekea kifo.
MT. GREGORI WA NAZIENZI (329-390)
  Ee Bwana, umpokee mikononi mwako kaka yangu aliyetuacha.
                 Kwa wakati wake utupokee sisi pia,
 kisha kutuongoza katika hija ya duniani hadi lengo ulilotupangia.
        Utujalie tuje kwako tukiwa tayari na watulivu kweli,
      si tumevurugwa na hofu, si katika hali ya uadui nawe,
           walau siku ya mwisho, siku ya kufariki kwetu.
    Utujalie tusijisikie tunaondolewa na kung’olewa kwa nguvu
                     katika ulimwengu na maisha,
           wala kwa hiyo tusifunge safari shingo upande.
           Bali utujalie tuje kwa utulivu na utayari mzuri,
kama watu wanaoondoka kuendea uzima wa heri usio na mwisho,
         uzima ule ulioma katika Kristo Yesu, Bwana wetu,
          ambaye apate utukufu milele na milele. Amina.
MT. MAKRINA (330-380)
            Ee Bwana, wewe umetuondolea hofu ya kifo.
Mwisho wa maisha yetu hapa umeufanya mwanzo wa uzima wa kweli.
          Kwa kitambo tu utaacha miili yetu ilale usingizi,
   halafu kwa tarumbeta ya mwisho utaiamsha kutoka usingizini.
      Wewe unaukabidhi udongo ukutunzie udongo wako huu
                  ulioufinyanga kwa mikono yako;
 nawe utauchukua tena na kutoka fungu la kufa, lisilo na muundo,
                utaugeuza kuwa na uzuri usiokufa.
MT. GREGORI WA NISA (335-394)
15

            Ee Mchungaji mwema, unakwenda wapi kuchunga,
                wewe unayebeba mabegani kundi lako lote?
                         Kwa kuwa kondoo yule pekee
         anawakilisha ubinadamu wote uliobeba mabegani mwako.
                        Unionyeshe mahali pa pumziko,
               unifikishe kwenye majani mema ya kunilisha,
   uniite kwa jina, ili mimi pia, niliye kondoo, niweze kusikia sauti yako
               na kwa hiyo niweze kupata uzima wa milele:
                    “Unionyeshe mpenzi wa roho yangu”.
 Ndivyo ninavyokuita, kwa kuwa jina lako liko juu ya kila jina na uelewa,
wala ulimwengu wote wa viumbe wenye akili hauwezi kulitaja nakulielewa.
             Basi, jina lako, ambamo wema wako unajitokeza,
                unawakilisha upendo wa roho yangu kwako.
 Kwa kuwa ningewezaje kutokupenda, baada ya wewe kunipenda mno?
    Ulinipenda hivi hata ukatoa uhai wako kwa kundi la malisho yako.
              Haiwezekani kufikiria upendo mkuu kuliko huo.
                  Umelipa wokovu wangu kwa uhai wako.
MARTIN WA TOURS (316-397)
Ee Bwana, nikihitajiwa bado na watu wako, sikatai uchovu wa kazi:
                         utakalo lifanyike!
MT. AMBROSI (340-397)
 Ee Bwana, mwenye huruma kwa wote, uniondolee dhambi zangu,
na kwa huruma washa ndani mwangu moto wa Roho wako Mtakatifu.
       Uniondolee moyo wa jiwe na kunipa moyo wa nyama,
            moyo wa kukupenda na kukuabudu wewe,
    moyo wa kupata raha ndani yako, kukufuata na kukufurahia
                       kwa ajili ya Kristo.
MT. JEROMU (347-420)
Ee Bwana, umetupatia Neno lako kama nuru ambayo iangazie njia yetu;
      utujalie tulitafakari Neno lako na kufuata mafundisho yake
     hivi kwamba tuone hiyo nuru inazidi kuangaza hadi adhuhuri,
                     kwa njia ya Kristo Bwana wetu.

Comments