Lilongwe. Malawi. Ilikuwa ni nderemo na vifijo
katika mji wa Blantyre nchini Malawi baada ya Rais Peter Mutharika wa
nchi hiyo kufunga ndoa na Gertrude Maseko.
Harusi hiyo ilifungwa katika Kanisa la Mtakatifu Michael jana mchana .
Muda mwingi Gertrude, alionekana akitabasamu huku akiwa amevaa gauni refu jeupe lililokuwa likiburuza chini.
Harusi hiyo ilishuhudiwa na viongozi mbalimbali wa
Serikali ya Malawi, akiwamo Jaji Mkuu, Anastasia Msosa, Spika wa Bunge
la Malawi, Richard Msowoya na kiongozi wa upinzani, Lazarus Chakwera.
Watoto wa kiume na wa kike wa rais wa zamani wa
Malawi, Bingu wa Mutharika walishuhudia ndoa hiyo ikifungwa na
kuhudhuria sherehe iliyofanyika katika mji huo.
Rais Mutharika alianza maisha mapya na mke wake baada ya kutamka: “Nimempokea Gertrude kuwa mke wangu kwa raha na shida.”
Wakati wakila kiapo cha ndoa kanisani, Rais
Mutharika alitamka : “Gertrude Maseko ni mke wangu.” Naye Gertrude
alitamka maneno hayo, hayo.
Padri Rapson Chikwenzule alitangaza kuwa wawili hao sasa ni mume na mke baada ya kufungisha ndoa hiyo saa 11:45 jana.
“Kuanzia sasa, natangaza Peter na Gertrude
wamekuwa mume na mke kwa jina la Baba, Mwana na Roho Mtakatifu.
Alichokiunganisha Mungu, mwanadamu hawezi kukitenganisha,” alisema Padri
Chikwenzule.
Baada ya kauli ya padri iliyoibua vifijo na
vigelegele, wawili hao walisaini hati ya ndoa baada ya Padri Roy Zingani
kuibariki tena ndoa hiyo.
Mashahidi wa ndoa hiyo walikuwa ni Arthur Msamba na Rorbert Salama ambao walitia saini hati ya ndoa ya wawili hao.
Baada ya ndoa hiyo kanisani, sherehe za harusi, zitafanyika
katika Kijiji cha Ndata, wilayani Thyolo ambako familia ya Rais
Mutharika inaishi.
Mume wa Gertrude ambaye amekuwa mbunge tangu mwaka
2009, alifariki dunia mwaka jana na katika uchaguzi wa mwaka huu,
alipoteza nafasi ya ubunge, baada Lucius Banda kushinda kiti hicho.
Peter Mutharika ni rais wa tatu kuoa baada ya kushika wadhifa wa urais nchini Malawi.
Rais wa zamani wa nchi hiyo, Bakili Muluzi alifunga ndoa akiwa madarakani baada ya kuachana na mke wake, Anne.
Vilevile rais mwingine wa zamani wa nchi hiyo Bingu wa Mutharika naye alioa kutokana na mke wake wa kwanza, Ethel kufariki dunia.
Comments