SABUNI

Na Frank Philip


Kazi ya Sabuni ni kusafisha uchafu, ambao kwa maji pekee hauwezi kuondoka. Huwezi kula bila kunawa vyema kwa sabuni. Cha kushangaza sana, sabuni yenyewe hailiwi, ila husafisha mikono ili iwe safi!

Watu wengi kwenye maisha yetu, wana madhara kama ilivyo sabuni, lakini ni wa muhimu kutusafisha na kuimarisha imani zetu. Usishindane na sabuni, itakudhuru. Wala usijaribu kuifanya chakula chako, itakutakasa tu, na ukiwa safi, utakula chakula chako (baraka) kwa amani.

Watu wengi sana sehemu za kazi, ofisini, nyumbani, kwenye ndoa, mahusiano nk., wako kama sabuni. Ladha yao ni mbaya, kila saa hawafai kwa chakula, lakini wakiwepo kati yetu, thamani yao ni kama SABUNI. Jua neno hili leo, hao watu na vurugu zao, ni wa muhimu sana kuthibitisha na kudhibitisha imani zetu. Usilipize KISASI kwa maana hutamwona Mungu akikuinua hatua nyingine, mwache mwovu aangamizwe na uovu wake mwenyewe. Japo kwa uovu huo huo, autendaye huangamia na astahimiliye huoshwa kama kwa sabuni.

Basi, wanaheri wale wastahimilio mateso na mashaka waletewayo na wengine katikati yao, kwa maana wakisha kushinda, watakuwa safi zaidi kuliko ambao kati yao hakuna sabuni; wale ambao maisha yao ni mepesi kama maji matupu, wamesafishwa, ila sio kwa sabuni, wafaa sana, japo hawana cha kujivunia kwani hawakushindana.

Usisahau kumshukuru Mungu kwa kila jambo, jua hao yote ni mapenzi yake. Japo unapita katika moto, hutaangamia; japo unapita katika maji mengi, hutafurikishwa. Mungu atakulinda na mabaya yote. Simama katika nafasi yako, usigeuke kushoto wala kulia; usirudi nyuma wala usizimie moyo. Jua hao wakuleteao vurugu na mateso, wapo kwa kusudi la Mungu pia, naam, hata wamekuwa sabuni nzuri ya kukusafisha na kukufanya bora kila siku. Jua ikupasavyo kuingia na kutoka mbele zao; omba siku zote ili usiwachukie kwa uovu na maumivu wakuleteayo, ukiweza hapo, thawabu yako ni kubwa na amani yako itadumu.

Frank Philip.

Comments