UKIWA NG’AMBO

Na Frank Philip


“Na hii ndiyo sheria, na amri, na hukumu, alizoziamuru BWANA, Mungu wenu, mfundishwe, mpate kuzitenda katika nchi ile mnayoivukia kuimiliki; upate kumcha BWANA, Mungu wako, kushika amri zake zote, na sheria zake, ninazokuamuru, wewe na mwanao, na mwana wa mwanao, siku zote za maisha yako; tena siku zako ziongezwe. Sikiza basi, Ee Israeli, ukaangalie kuzitenda; upate kufanikiwa, mpate kuongezeka sana, kama BWANA, Mungu wa baba zako, alivyokuahidi, katika nchi ijaayo maziwa na asali. Sikiza, Ee Israeli; BWANA, Mungu wetu, BWANA ndiye mmoja. Nawe mpende BWANA, Mungu wako, kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa nguvu zako zote. Na maneno haya ninayokuamuru leo, yatakuwa katika moyo wako; nawe uwafundishe watoto wako kwa bidii, na kuyanena uketipo katika nyumba yako, na utembeapo njiani, na ulalapo, na uondokapo. Yafunge yawe dalili juu ya mkono wako, nayo yatakuwa kama utepe katikati ya macho yako. Tena yaandike juu ya miimo ya nyumba yako, na juu ya malango yako” (Kumbukumbu la Torati 6:1-9).

Kuna mambo ya muhimu kuyajua ukiwa ng’ambo ya Yordani (ukitokea Misri). Mara nyingi watu wameongea kwa mifano kwamba kabla ya KUKATA SHAURI kumfuata Yesu (kuokoka), huwa ni maisha ya Misri, na kukata shauri ni kama kuamua kwa DHATI kumfuata Yesu, ili awe BWANA na MWOKOZI wa maisha yako. Angalia tena, awe Bwana (boss) ambaye utamtii na kufuata maagizo yake; kisha awe Mwokozi, atakayekuokoa katika dhambi, makucha ya adui, kutoka katika shida zako na kukuokoa na hukumu ya milele.

Sasa nisikilize vizuri. Kuna mtego mtu anapobadili maisha kutoka UTUMWANI (Misri) kuingia kwenye UHURU (ndani ya Kristo). Ghafla, umevuka mto Yordani, umefika mahali ambapo kuna MAZIWA na ASALI, PESA zako zimeongezeka, umejenga NYUMBA na MIFUGO yako imeongezeka. Chunga moyo wako USIMSAHAU Bwana Mungu wako aliyekuvusha katika mengi. Musa aliona hii shida na kuwaonya wana wa Israel. Nami nakuja na neno hili huku mwisho wa nyakati, nakupa onyo tena.

Watu wengi wakiisha kupigana vita vikali vya shule, kutafuta kazi, kutafuta mume/mke, kupata mali, nk. wanamsahau Mungu wao. Kimsingi hawasemi “Mungu nimekuacha”, au “Mungu sikupendi tena”, au “Sasa nimerudi nyuma”, nk. ila utaona kwenye matendo yao. Ule moto na nguvu ya KUMTAFUTA Mungu hakuna tena! Ile HOFU ya dhambi na kuogopa KUMKOSEA Mungu imetoweka kabisa. Sasa, ile BARAKA ambayo Mungu ameleta maishani mwao IMEGEUKA na kuwa CHUKIZO mbele za Mungu wao, japo wapo NG’AMBO ya Yordani. Mungu akiangalia anasema “sasa nimejua” kwamba hukunipenda Mimi ila dunia!

Utasikia mtu anasema “niko busy”, hana muda wa kusoma NENO ila ana muda wa kwenda lunch na bosi wake. Hana muda wa MAOMBI ila ana muda wa kwenda kufanya machukizo na wale watu “waliompatia” nafasi, eti, anashindwa kuwakatalia kwa sababu walimsaidia! Ona jambo hili, mtu anamkosea Mungu kwa kuogopa kumkasirisha mwanadamu! Huku amesahau vipindi vya kupita JANGWANI kusiko na maji wala chakula. Wenzake wengi wamekufa jangwani kwa KUNG’ATWA na nyoka za moto, yeye amevushwa na Mungu salama, sasa ameingia KAANANI anaanza kufanya MACHUKIZO kwa mfano wa kule Misri! Amesahau kwamba sio silaha wala jitihada zake, wala mwanadamu amemwinua ila ni Mungu, sasa anasema “hawa watu walinisaidia hata nikafikia nafasi hii”! na wala hamtaji tena Mungu hapo! Kweli wamekusaidia, ila hutaona utukufu ukienda kwa Musa, ila kwa Mungu japo kweli ni Musa ndio alienda kwa Farao kuomba kibali hawa jamaa watoke Misri. Ona jambo hili Mungu anaona katikati ya watu aliowanunua kwa Damu ya Mwanawe wa pekee. Baraka Mungu aliyowaapia imegeuka. Je! Utamsahau Bwana Mungu wako kwa upesi namna hii?

Angalia mambo machache hapo Kumb. 6: 1-9. Kwanza, ukimtii Mungu unapata bonus ya maisha marefu, siku zako zinaongezwa; pili, mpende BWANA, Mungu wako, kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa nguvu zako zote; tatu, “maneno haya ninayokuamuru leo” (Ushuhuda wa Kristo), yatakuwa katika moyo wako (imani); nawe uwafundishe watoto wako kwa bidii, na kuyanena uketipo katika nyumba yako, na utembeapo njiani, na ulalapo, na uondokapo. Kazi ya kushuhudia habari za Kristo kila mahali ni LAZIMA sio uchaguzi (option); nne, hakikisha kuna matunda ya kazi yako katika Kristo, mtu akikutazama mkononi mwako aone UTEPE, akija nyumbani mwako aone kwenye MIIMO ya mlango wako jambo.

Chunga moyo wako kuliko vitu vyote, ili usije ukaishi huku NG'AMBO kwa mfano wa yale matendo ya MISRI. Mungu tusaidie kukaa ng’ambo ya Yordani kwa kukupendeza.

Frank Philip.

Comments