VITU 7 AVICHUKIAVYO MUNGU.



 
BWANA YESU asifiwe ndugu yangu.


Karibu tujifunze kuhusu mambo 7 anayoyachukia MUNGU. Mambo haya hutendwa na mwanadamu aliyeumbwa na MUNGU. MUNGU anachukia sana juu ya tabia hii ya mwanadamu.  MUNGU kupitia neno lake anasema tuache uovu. MUNGU alituumbia macho, ulimi, masikio, midomo, miguu na mikono ili tuitumie kwa wema na kwa utukufu wake lakini wanadamu walio wengi hutumia viungo vyao vya mwili kwa mambo mabaya.

Mithali 6:16-19 ( Kuna vitu sita anavyovichukia BWANA; Naam, viko saba vilivyo chukizo kwake. Macho ya kiburi, ulimi wa uongo, Na mikono imwagayo damu isiyo na hatia; Moyo uwazao mawazo mabaya; Miguu iliyo myepesi kukimbilia maovu; Shahidi wa uongo asemaye uongo; Naye apandaye mbegu za fitina kati ya ndugu. ).


1.    MACHO.


Macho ndio ya kwanza kabisa kumfanya mwanadamu atende dhambi.

Kuona kunasababisha mtu kufanya uovu.

Matamanio, wizi au kuiga husababishwa na macho.

MUNGU hakutupa macho ili tuyatumie kwa ubaya bali kwa matendo mema. Kuna watu wataenda jehanamu kwa sababu macho yao yaliwadanganya. Ndugu yangu tumia macho yako kwa utukufu wa MUNGU na sio kutumia macho yako kwa ajili ya kazi ya shetani.

2.    ULIMI.


Ulimi husababisha kutenda dhambi kwa kupotosha ukweli, kusema uongo, kushauri vibaya, uchochezi na mengine mengi. Ndugu zangu tusiutumie ulimi wetu kumtukuza MUNGU na wakati huo huo tuutimie kuwakandamiza wanadamu wengine walioumbwa na MUNGU. Usitumie ulimi wako kuwalaani watu wa MUNGU. Tumia ulimi wako kumtukuza MUNGU aliye kuumba na kumtukuza kwa sababu ya uumbaji wake wanyama, mawingu, bahari na nchi ni vitu ambayo MUNGU aliviumba na hakika anastahili heshima na sifa zote. Tumia ulimi wako vizuri. 
Ndoa nyingi zimekufa kwa sababu ya ulimi wa uongo.

Watu wengi wamekufa kwa sababu tu ulimi ulitumika kuleta uongo.

Watu wamefukuzwa shule kwa sababu ya ulimi.

Uzima na mauti huwa katika uwezo wa ulimi(Mithali 18:21), ukiutumia ulimi wako kwa mabaya utakula matunda yake na matunda yake ni jehanamu.

MUNGU atusaidie.

MUNGU anapoyaangalia matendo ya ulimi wa mwanadamu anashangaa sana maana walio wengi wanatumia ndimi zao vibaya.

Ndugu ombea ulimi wako, utiishe ulimi wako kwa jina la YESU KRISTO.

           

3.  MIKONO.


Mikono husababisha kumwaga damu.

Mikono ya madaktari imesababisha kutoa mimba.

Mikono ya askari imetumika kuua.

Mikono ya magaidi imetumika kuangamiza maelfu.

Mikono ya wamama wengi imetumika kuroga na kuua.

Mikono ya wababa wengi imetumika kufanya ujambazi na kuua. MUNGU anashangaa sana maana hakuiumba mikono kwa ajili ya mabaya bali kwa ajili ya mema. Wazinzi wengi wangekua hawana mikono nakuhakikishia uzinzi usingekuwepo. MUNGU akiitazama mikono yako leo ataona nini? Kwa walio wengi MUNGU ataona dhambi tu imejaa na kuzidi sana.

Ni wakati wa kutubu na kurejea kwa BWANA maana uovu wa mwanadamu umezidi, uovu wa sasa umezidi hata sodoma na gomora lakini MUNGU ametupa neema yake tu kupitia mwanawe wa pekee YESU KRISTO lakini wanadamu hao hao kupitia akili zao ndogo hawataki wokovu mkuu namna hii. Wakiambiwa kuokoka,  mikono yao inawaaambia subiri ukizeeka ndipo utaokoka maana kipindi hicho mikono haitakua na uwezo wa kupapasa wadada. Ndugu zangu MUNGU anachukia sana uovu wa wanadamu. Ameandaa adhabu kali na ndio maana neema yake pia ni kubwa sana leo. Ni wakati wa kumwambia MUNGU ''tuumbie mwili mpya unakutukuza na kukutumikia wewe tu BWANA.''


4.  MOYO.


Hapa sasa ndio makao ya uovu wa mwanadamu.

Moyo ndio chanzo cha vyote vibaya na vizuri na kwa kutumia moyo mtu hutenda dhambi ya aina yeyote.

BWANA MUNGU anachukia sana moyo unaowaza mabaya.



ROHO MTAKATIFU anatamani tumpe nafasi ili yeye atawale mioyo yetu lakini wanadamu hawamhitaji wala hawahitaji kuacha uovu. MUNGU ninayemtumikia akusaidie wewe unayesoma ujumbe huu akutengeneze ili utimie kwa ajili ya mema tu,  akufinyange roho yako ili kuondoa makunyanzi yote ya shetani. BWANA YESU akukumbuke na kukuandika jina lako katika kitabu chake cha uzima , akutiishe ili umpendeze MUNGU tu. Uovu yatosha, tulifanya mabaya mengi sana kupitia viungo vyetu lakini BWANA YESU akatuhurumia. Ndugu neema hii usiipoteze, mpe YESU maisha yako na ROHO MTAKATIFU ataingia moyoni mwako na kukutawala  na kama akikutawala yeye atakupa nguvu za kushinda kila aina ya dhambi na uovu kama tu ukimsikiliza yeye. Ndugu yangu hii ni muhimu tena muhimu sana .

BWANA YESU anasema ''moyo wa mwanadamu ndio unaoongoza kwa kumtia unajisi mwanadamu, maana moyoni hutoka mawazo mabaya,''  dhambi zote zinapikwa mioyoni ndipo zinaenda kutendeka. Moyo wa mwanadamu una mambo mabaya sana ni nani awezaye kuyajua? Dhambi za mwanadamu ambazo zinatengenezwa katika moyo wake ndizo zinamfarakanisha mwanadamu na MUUMBA wake. Ndugu je MUNGU anataka nini kwako?. Ukimpa nafasi BWANA YESU utapona lakini uking’ang’ania dini tu nakuhakikishia huwezi kuuona uzima wa milele. Linda moyo wako kuliko yote uyalindayo maana ndiko zitokako chemchemi za uzima.

Moyo wangu u wazi, niko hapa BWANA YESU, Niguse BWANA, Moyo wangu u wazi.

Moyoni mwangu nimempata YESU wewe je?


5.       MIGUU.


Miguu mingi ni myepesi  kukimbilia maovu badala ya kukimbilia uzima. Maovu ni machukizo kwa MUNGU.

Miguu ni myepesi sana kukimbilia disko kuliko kukimbilia kwenye mkutano wa injili, miguu ni myepesi sana kukimbilia tamasha la bongo fleva kuliko kukimbilia maombi kanisani.


6.     SHAHIDI WA UONGO.


Uongo wowote kwa ujumla ni chukizo kwa MUNGU.

Watu wengi ni mashahidi wa uongo, wengi ni manabii wa uongo kwa maana wako kinyume na KRISTO.

Ushahidi wa uongo umesababisha vifo vingi sana. MUNGU anachukia sana uongo.



7.   FITINA.


Fitina pia ni chanzo cha dhambi nyingi.

Fitina husababisha vita, ugomvi , uchochezi na matengano.

 MUNGU anachukia fitina. Kwanini kufitini ndugu yako.



Ndugu yangu mambo haya 7, dhambi zote azitendazo mwanadamu ziko ndani yake.

Hakuna dhambi ambayo iko nje na vitu hivi 7.

MUNGU anachotaka tu tuache dhambi na tuishi kwa kumcha yeye, ukimcha MUNGU hutatenda machukizo haya.

MUNGU anachukia dhambi na dhambi ni mbaya dhambi huzaa mauti, kuzimu ipo kwa ajili watenda dhambi tu. Dhambi ni mbaya sana.

Isaya 55:6-7(Mtafuteni BWANA, maadamu anapatikana, Mwiteni, maadamu yu karibu;  Mtu mbaya na aache njia yake, Na mtu asiye haki aache mawazo yake; Na amrudie BWANA, Naye atamrehemu; Na arejee kwa MUNGU wetu, Naye atamsamehe kabisa. ).

Kwa sasa naishia hapo, MUNGU akitupa nafasi tutajifunza tena siku nyingine.na kama hujampokea BWANA YESU muda wa kumpokea ni leo wala sio kesho, amua leo na atakuandika jina lako katika kitabu cha uzima na utaanza kuukulia wokovu kwa mafundisho kanisani. ROHO MTAKATIFU aliyenipa ujumbe huu ana makusudi kabisa na wewe, hataki upotelee motoni anataka uende uzimani aliko KRISTO BWANA.
                     MUNGU akubariki sana .
                      Ni mimi ndugu yako
                       Peter M Mabula
                 Maisha ya Ushindi Ministry.
                           0714252292
                 MUNGU akubariki sana uliyesoma somo hili.
 MUNGU Akubariki.


Comments