VIWANGO AINA 4 VYA IMANI.



 
BWANA YESU asifiwe.

Somo hili litakusaidia kujua kiwango chako cha imani.


Karibu.


Yamkini  utajifahamu uko kiwango gani cha imani.

Imani ni kuwa na uhakika wa mambo unayotarajia.

Imani ni hakika.

Imani yako itaonekana kwenye maombi yako, sadaka  na chochote ukifanyacho kwa utukufu wa MUNGU.

Imani ni coordinator wa kuyapeleka maombi yako kwa MUNGU.

Imani ina macho na inaona.

   1.  Kiwango cha kwanza cha Imani ni IMANI HABA.
 
Unaweza ukaiita kwamba ni IMANI YA KUSAIDIWA NA WENGINE

Hii ni imani lakini ni haba.

Isingekuwa imani YESU asingeizungumzia kwamba ipo imani haba. Mfano Petro alipotaka kuzama kwenye maji  baada ya kuanza kutembea  na baada ya kuona shaka alianza kuzama, hii ni imani haba . Ndugu mashaka yako yanaweza kuwa msiba kwako, mashaka yamezaa imani haba. YESU alimshika mkono Petro na kumsaidia.

Imani haba ni imani ya kusaidiwa na wengine.

-Wengi wana imani haba yaani wana imani ya kushikwa mikono ndipo waweze.

-Imani haba yenyewe haiwezi kwenda mpaka isaidiwe  Mathayo 14:30-31 (Lakini alipouona upepo, akaogopa; akaanza kuzama, akapiga yowe, akisema, BWANA, niokoe. Mara YESU akanyosha mkono wake, akamshika, akamwambia, Ewe mwenye IMANI HABA, mbona uliona shaka? ).

Wakati huu Petro alikuwa na imani haba.

Tuangalie pia maandiko  ambapo BWANA YESU anazungumzia imani hapa.

Mathayo 8: 23-26 (Akapanda chomboni, wanafunzi wake wakamfuata. Kukawa msukosuko mkuu baharini, hata chombo kikafunikizwa na mawimbi; naye alikuwa amelala usingizi. Wanafunzi wake wakamwendea, wakamwamsha, wakisema, BWANA, tuokoe, tunaangamia. Akawaambia, Mbona mmekuwa waoga, enyi wa IMANI HABA? Mara akaondoka, akazikemea pepo na bahari; kukawa shwari kuu. )

Kipindi hiki wanafunzi wa YESU walikua na imani hapa yaani walikuwa na imani ya kusaidiwa.



       2.  Kiwango cha pili cha imani ni IMANI INAYOJITEGEMEA.


Tunaweza tukaiita IMANI INAYOJITOSHELEZA.

Mathayo 9:22( YESU akageuka, akamwona, akamwambia, Jipe moyo mkuu, binti yangu; imani yako imekuponya. Yule mwanamke akapona tangu saa ile. )

Imani inayojitegemea ni imani ambayo haiwasumbui wachungaji.

Imani inayojitosheleza ni imani ambayo inaleta matokeo bila kumsumbua BWANA YESU ona hapa Marko 2:1-12 ( Akaingia Kapernaumu tena, baada ya siku kadha wa kadha, ikasikiwa ya kwamba yumo nyumbani.  Wakakusanyika watu wengi, isibaki nafasi hata mlangoni; akawa akisema nao neno lake.  Wakaja watu wakimletea mtu mwenye kupooza, anachukuliwa na watu wanne.  Na walipokuwa hawawezi kumkaribia kwa sababu ya makutano, waliitoboa dari pale alipokuwapo; na wakiisha kuivunja wakalitelemsha godoro alilolilalia yule mwenye kupooza.  Naye YESU, alipoiona imani yao, akamwambia yule mwenye kupooza, Mwanangu, umesamehewa dhambi zako.  Na baadhi ya waandishi walikuwako huko, wameketi, wakifikiri mioyoni mwao,  Mbona huyu anasema hivi? Anakufuru. Ni nani awezaye kusamehe dhambi isipokuwa mmoja, ndiye MUNGU?  Mara YESU akafahamu rohoni mwake kwamba wanafikiri hivyo nafsini mwao, akawaambia, Mbona mnafikiri hivi mioyoni mwenu? Vyepesi ni vipi, kumwambia mwenye kupooza, Umesamehewa dhambi zako, au kusema, Ondoka, ujitwike godoro lako, uende? Lakini mpate kujua ya kwamba Mwana wa Adamu anayo amri duniani ya kusamehe dhambi, (hapo amwambia yule mwenye kupooza),
  Nakuambia, Ondoka, ujitwike godoro lako uende nyumbani kwako. Mara akaondoka, akajitwika godoro lake, akatoka mbele yao wote; hata wakastaajabu wote, wakamtukuza MUNGU, wakisema, Namna hii hatujapata kuiona kamwe. ).

Imani hii inaleta matokeo makubwa.

Huyu ndugu alikuwa hajaokoka ndio maana BWANA YESU alimwambia ‘’ Umesamehewa dhambi zako’’ lakini waliomleta pamoja nay eye mwenyewe walikua na imani inayojitegemea , walikua na imani kwa YESU ndio maana uzima uliingia kwake.

-Imani inaongea ndio maana imani iliwaongoza  njia, imani iliwaambia toboeni dari, imani hapo inaongea. Imani inaposema toboa dari haikosei ila inauhakika kwamba YESU yupo . Dari ndio ilikua kizuizi cha mwisho  na hata kwako ipo dari ambayo ndio kizuizi chako cha mwisho  ili upokee muujiza wako  ni lazima utoboe  dari ndio upone. Dari yako hakikisha inatoboka na wewe unakutana na YESU  na kupokea muujiza wako. Yawezekana dari yako  hujatoboa ili kukutana na YESU . Dari yako yawezekana ni wewe kufika tu kwenye mkutano wa injili, yawezekana dari yako ni wewe  kufika kanisani ili kuombewe. Toboa dari leo ili upone.



     3.  Kiwango cha 3 cha imani ni IMANI PUNGUFU.


Imani pungufu  ni tofauti na imani haba yaani hii ni imani ya furaha ya muda lakini yakitokea magumu kidogo tu inakimbia. Ni kama chupa ya soda ila haijajaa.

Imani hii ni ya rahu ila kukitokea ugumu kidogo au kuzidiwa na jambo Fulani  kwa muda inaweza ikatimua mbio. Mathayo 17:19-20 ( Kisha wale wanafunzi wakamwendea YESU kwa faragha wakasema Mbona sisi hatukuweza kumtoa? YESU akawaambia, Kwa sababu ya UPUNGUFU WA IMANI yenu. Kwa maana, amin, nawaambia, Mkiwa na imani kiasi cha punje ya haradali mtauambia mlima huu, Ondoka hapa uende kule; nao utaondoka; wala halitakuwako neno lisilowezekana kwenu. ).

Imani hii ni furaha ya muda tu  magumu yakitokea inaweza kuzimika au kuhama kanisa kabisa na kukimbia.


Luka 8:13 ( Na wale penye mwamba ndio wale ambao wasikiapo hulipokea lile neno kwa furaha; nao hawana mizizi, huamini kitambo kidogo, na wakati wa kujaribiwa hujitenga. )

Mtu mwenye imani hii anaweza kuwa ni muumini mzuri tu kanisani , anaweza kuwa mwimbaji,shemasi au kiongozi kanisani lakini kanisa likipita kwenye ugumu kidogo anahama.

Wengine asipotembelewa tu wakati anaumwa anahama kanisa hiyo ni imani pungufu.

Wengine kwa sababu wana imani pungufu wanakimbia makanisa yenye idadi ndogo ya waumini na kwenda kwenye makanisa makubwa ambako wanajua hawataambiwa mchango wa ujenzi wa kanisa hii ni imani pungufu. Hili ni kundi kubwa sana la watu.  Wenye imani hii hawataki shida , ikitokea tu wanakimbia.

Ndugu ningependa  utambue kwamba Kadiri unavyokua kiroho  ndivyo na jaribu lako linakuwa kubwa.  Usikimbie bali mtumikie MUNGU kwa uaminifu.



      4.  Kiwango cha 4 cha imani ni IMANI KUBWA.


Mathayo 15:21-28 ( YESU akaondoka huko, akaenda kando pande za Tiro na Sidoni. Na tazama, mwanamke Mkananayo wa mipaka ile akatokea, akampazia sauti akisema, Unirehemu, BWANA, Mwana wa Daudi; binti yangu amepagawa sana na pepo. Wala yeye hakumjibu neno. Nao wanafunzi wake wakamwendea, wakamwomba, wakisema, Mwache aende zake; kwa maana anapiga kelele nyuma yetu. Akajibu, akasema, Sikutumwa ila kwa kondoo waliopotea wa nyumba ya Israeli. Naye akaja akamsujudia, akisema BWANA, unisaidie. Akajibu, akasema, Si vema kukitwaa chakula cha watoto na kuwatupia mbwa. Akasema, Ndiyo, BWANA, lakini hata mbwa hula makombo yaangukayo mezani pa bwana zao. Ndipo YESU akajibu, akamwambia, Mama, IMANI YAKO NI KUBWA; na iwe kwako kama utakavyo. Akapona binti yake tangu saa ile. )

Hiyo ndio imani kubwa na BWANA mwenyewe anathibitishwa kwamba hii ni imani kubwa.

BWANA YESU alimwambia Yule ndugu mwenye imani kubwa kwamba ‘’ Iwe kama ulivyotaka’’ kwa sababu alikua na imani kubwa.

Mama huyu kwanza alikutana na wanafunzi, wakamwambia unatupigia kelele lakini imani kubwa ikavuka kikwazo hicho.

Kikwazo cha pili YESU alimwambia kwa kumjaribu kwamba yeye hakuja kwa ajili ya watu wasio Waisraeli lakini imani kubwa ikavuka na kikwazo hiki. Kikwazo cha 3 YESU alimwambia kwa kumjaribu kwamba  haiwezekani mbwa kula chakula cha watoto, yaani aliitwa mbwa lakini imani kubwa ilikivuka kikwazo hiki.

 Hebu tusome pia Mathayo 8:10-13 ( YESU aliposikia hayo, alistaajabu, akawaambia wale waliomfuata, Amin, nawaambieni, Sijaona IMANI KUBWA namna hii, kwa ye yote katika Israeli. Nami nawaambieni, ya kwamba wengi watakuja kutoka mashariki na magharibi, nao wataketi pamoja na Ibrahimu, na Isaka, na Yakobo katika ufalme wa mbinguni; bali wana wa ufalme watatupwa katika giza la nje, ndiko kutakuwako kilio na kusaga meno. Naye YESU akamwambia yule akida, Nenda zako; na iwe kwako kama ulivyoamini. Mtumishi wake akapona saa ile ile. )

YESU anasema kwamba hajawahi kuona imani kubwa katika Israel kama ya Yule akida.



Ndugu yangu najua umefahamu kiwango chako cha imani baada ya kujifunza ujumbe huu. Tunatakiwa viwango vyetu  vikue. Mitume walimwambia BWANA YESU awaongezee imani Luka 17:5 (Mitume wakamwambia Bwana, Tuongezee imani. ).

Je wewe uko kundi gani la imani?


 Kwa sasa naishia hapo, MUNGU akitupa nafasi tutajifunza tena siku nyingine.na kama hujampokea BWANA YESU muda wa kumpokea ni leo wala sio kesho, amua leo na atakuandika jina lako katika kitabu cha uzima na utaanza kuukulia wokovu kwa mafundisho kanisani. ROHO MTAKATIFU aliyenipa ujumbe huu ana makusudi kabisa na wewe, hataki upotelee motoni anataka uende uzimani aliko KRISTO BWANA.
                     MUNGU akubariki sana .
                      Ni mimi ndugu yako
                       Peter M Mabula
                 Maisha ya Ushindi Ministry.
                           0714252292
                 MUNGU akubariki sana uliyesoma somo hili.
 MUNGU Akubariki.

Comments