ZAKA YA FUNGU LA KUMI

Na Frank Philip


“Usiache kutoa zaka ya fungu la kumi katika maongeo yote ya mbegu zako, yatokayo shamba mwaka baada ya mwaka. Nawe utakula mbele za BWANA, Mungu wako, mahali atakapochagua apakalishe jina lake, zaka ya nafaka zako, na divai yako, na mafuta yako, na wazaliwa wa kwanza wa makundi yako ya ng’ombe na ya kondoo; ili upate kujifunza kumcha BWANA, Mungu wako, daima” (Kumbukumbu 14:22,23).

“Kila mwaka wa tatu, mwisho wake, toa fungu la kumi lote la maongeo yako ya mwaka huo, uliweke ndani ya malango yako; na Mlawi kwa kuwa hana fungu wala urithi pamoja nawe, na mgeni, na yatima, na mjane aliyefiliwa na mumewe, walio ndani ya malango yako, na waje wale na kushiba; ili kwamba BWANA, Mungu wako, akubarikie katika kazi yote ya mkono wako uifanyayo” (Kumbukumbu 14:28,29).

Mafundisho mengi kuhusu UTOAJI wa SADAKA yamekuwa na shida ya kuelemea upande fulani, hivyo kupelekea watu kushindwa kufanya yawapasayo na kuishi kwa hofu, bila kupata baraka zinazostahili katika utoaji wao.

Kuna mambo machache ya kujifunza katika sadaka. Sadaka ZOTE zina mambo 5 ya kuangalia: 1. Aina ya sadaka, 2. Kiasi cha sadaka, 3. Muda wa kutoa, 4. Mahali pa kutoa, na 5. Nani apewe hiyo sadaka.

Haya mambo 5 nayaweka katika makundi mawili: Kwanza, sababu au lengo la kutoa; na pili, matokeo ya kutoa.

Jifunze jambo hili. Kila utoaji una kusudi/lengo fulani. Lengo la msingi kabisa ni KUMCHA Mungu. Mambo mengine yatafuata hapo, kwenye kusidi/lengo la utaji wako, ila anza na Mungu. Kama lengo sio kumpendeza Mungu, au kutoa kwa kumcha Mungu, fikiri tena kwa habari ya utaoji wako. KANUNI ya msingi ya utoaji wowote ni kutoa kwa MOYO wa kupenda. Ukitoa kwa sababu ya KULAZIMISHWA, angalia tena kusudi la huo utoaji. Jifunze kutoa kwa UKARIMU kwa maana utavuna kwa ukarimu pia.

KUMCHA MUNGU

Sasa nisikilize vizuri. Kwanza usiache kutoa ZAKA, na usitoe mahali POPOTE, ila pale Mungu alipopachagua. Ona lengo la kufanya hivi, “ili upate kujifunza kumcha BWANA, Mungu wako, daima” (Kumb. 14:23). Unaposikiliza maelekezo ya kutoa, ukakubali kutoa na ukatoa MAHALI Mungu alikokuagiza (alipopachagua) kutoa, hiyo ni KUMCHA Mungu wako, unaambiwa “ili upate kujifunza kumcha Mungu wako daima”. Ni jambo la kujifunza daima. Muulize Mungu MAHALI pa kupeleka sadaka zako, ili Mungu ajue unamcha.

Ukiangalia Kumbukumbu 14:24 na 25, utaona kuna wakati utapata maagizo ya kupeleka sadaka zako, ila ni mbali na hapo ulipo. Na kwa sababu ni LAZIMA kumtii Mungu kwa habari ya mahali pa kutoa, ndipo unaagizwa ubadili hiyo sadaka kuwa pesa (uuze), kisha upeleke hiyo fedha huko ulikoagizwa na Mungu.

Sasa najua msitari mashuhuri unaosema “LETENI”, [“Leteni zaka kamili ghalani, ili kiwemo chakula katika nyumba yangu”, (Malaki 3:10a)] na mara nyingi hutawasikia watumishi wa Mungu wakisema “PELEKA”. Nakubali kimsingi kabisa kuna wakati utatakiwa KULETA, ila kuna wakati utatakiwa KUPELEKA pia. Ukitaka kuona msisitizo wa wahubiri wa namna hii, angalia VITISHO nyumba ya mahubiri ya “LETENI”. Je! Kusudi ni kumcha Mungu?

BARAKA

Zingatia mambo haya; kuna aina ya sadaka, kiasi, muda, na walaji wa zaka. Ukiangalia Kumbukumbu 14: 28 na 29, utaona orodha ya watu wanaostahili kula hilo fungu lako la kumi. Utaona WALAWI, tena ni kwa sababu hawana urithi (biashara, mshara, miradi, nk.), kazi yao ni moja tu, huduma mbele za Bwana. Je! Kila mtumishi wa Mungu ataitwa MLAWI? Pima mwenyewe na kujua jibu ukiongozwa na Roho Mtakatifu. Mbona mgeni, yatima na wajane wamesahulika katikati yetu? Je! Hatukuagizwa kwamba nao wapeewe wale washibe? Mbona wajane, yatima na masikini katikati yetu wanalala njaa? Je! Umesahau hadithi ya Msamaria mwema, ambapo watu wa Mungu waliona mhitaji njiani, wakapita hapo kando wakiwahi mahekaluni mwao?

Ana jambo hili, unapopeleka zaka, ili iwe CHAKULA kwa haya makundi ambayo Mungu ameagiza, kuanzia watumishi wake, wageni (mgeni ni mtu asiye na urithi katikati yako, unaweza kutumia neno “masikini” badala ya “mgeni”), yatima, wajane, tena kuanzia MALANGONI mwako, ndipo upeleke mahali utakapoagizwa MOJAWAPO ya jamaa zako (mahali Bwana alipoamua kuweka jina lake), ndipo “BWANA, Mungu wako, akubarikie katika kazi yote ya mkono wako uifanyayo”.

Sasa najua watu wamefundishwa kutazama baraka, kama ndio kichocheo cha kutoa zaka na sadaka zao. Kumbuka baraka ni matokeo, kichocheo cha kutoa na lengo la MSINGI ni kumcha Bwana Mungu wako. Ukitoa kwa sababu unamwogopa au unamwonea aibu mchungaji wako, hiyo ni shauri yako, ila leo nakupa shauri, toa zaka na sadaka zako kwa sababu unataka KUMCHA Mungu na kumpendeza. Fuata maagizo yake, na ujue kiasi, mahali na muda wa kutoa zaka na sadaka zako. Bila kusahau kwamba Bwana alisema sadaka ni SIRI; “mkono wako wa kushoto usijue nini mkono wa kulia unafanya”.

Frank Philip.

Comments