BALOZI WA PAPA: HATA KAMA KANISA LITATESWA LAKINI HALITATETEREKA


DSC_0854
BALOZI wa Papa nchini Askofu Mkuu Fransisko Padilla
  • Akemea utengano ndani ya Kanisa
BALOZI wa Papa nchini Askofu Mkuu Fransisko Padilla amesema kuwa ijapo Kanisa  linaendelea kuteswa na kupata manyanyaso, halitatetereka bali litaendelea kutoa sauti ya kinabii inayosimamia ukweli ambao chimbuko lake ni Kristo. 

“Ni milenia ya pili sasa Kanisa  linaendelea kushuhudia mateso na manyanyaso. Mateso hayo hayataliweka Kanisa katika hatari ya kutetereka bali linatakiwa kuwa na nguvu zaidi kwa kuwa na ushirikiano baina ya viongozi wanaokuwa na sauti moja ya kuwaongoza watu wake.

” Ameyasema hayo wakati wa ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa 67 wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) uliofanyika katika Makao Makuu ya Baraza hilo Kurasini Jijini Dar es Salaam. Mkutano huo ulihudhuriwa na Maaskofu wa Kanisa Katoliki kutoka majimbo mbalimbali nchini, Makatibu Watendaji wa Idara na Tume za Baraza hilo , Wakuu wa seminari Kuu, shule za sekondari, vyuo vikuu, hospitali, mashirika ya kitawa na viongozi wa kitaifa wa vyama vya kitume. Askofu Mkuu Padilla amesisitiza juu ya umoja ndani ya Kanisa hususani viongozi wake ambao wanadhama ya kichungaji kuwa na lengo moja la kuunganisha watu ili kanisa liendelee kusimama na kumtangaza Kristo aliye asili ya uhai wa kila mmoja.

 “Ninasisitiza umoja na mshikamano ndani ya Kanisa Tanzania kwani sisi sote kama Kanisa ni mwili mmoja uliounganika na Kristo anaye lielekeza Kanisa na kulitegemeza. Mwili ukijitenga na kichwa hauna uhai bali mfu. Hivyo ni jukumu la Kanisa kuunganika na Kristo kwa upendo na imani thabiti,”ameeleza. Ameendelea, “Lazima Kanisa liwe na viongozi wenye maadili wanalolisimamia Kanisa na kuongoza watu katika utimilifu wake. Viongozi waruhusu Kristo kuchunga Kondoo zake, wawaoneshe njia ya kupita na kuwarutubisha kiroho. Wote tuishi katika umoja na muunganiko ndani ya Kristo na Kanisa. Kukabiliana na matakwa binafsi, na kutambua umuhimu wa kila mmoja ndani ya familia, parokia, majimboni na katika kazi mbalimbali. Msiruhusu mafarakano kwani yatatutenganisha na Kristo. Mafarakano yanaweza kutusababisha tukue lakini yanaweza kutugawanya. Tuungane hata kama tunatofauti zetu kwani jukumu la Kanisa ni kuunganisha watu wenye vipaji tofauti. Ni milenia yapili sasa ambapo kanisa limeshuhudia manyanyaso lakini hatutetereki. Tunatakiwa tubaki katika umoja na kutoa sauti ya kinabii ya kulinda imani ya Kristo duniani na kushinda nguvu za giza zinazolishambulia Kanisa. Kinachotakiwa ni kubaki katika umoja na kuwa na viongozi imara. Uongozi imara ndiyo utakaolitegemeza Kanisa. Waamini wanamategemeo makubwa kutoka kwetu sisi viongozi Ujumbe wa Papa Fransisko kwa Maaskofu wa Tanzania wakati walipomtembelea (Ad limina apostolorum), alisisitiza juu ya maadili ya mapadri. Mapadri wanatakiwa kuwa na maadili ambayo yanafaa kuongoza taifa la Mungu na kujengeka kiroho, kimwili na kitaaluma katika maisha yao yote. 

Tuhakikishe tunakuwa na mapadri bora . Tutafakari juu ya maisha yao na kuona jinsi gani maisha yao yanaungana na imani ya Kristo. Kuwasaidia kujitambua wao ni akina nani. Kuwaza, kuishi na kutenda kutokana na wito wao. Wawe mfano kwa waamini na kuwa waaminifu katika mafanikio na changamoto. Wawe mababa na ndugu wenye huruma kwa watu, na kukumbatia umasikini wa roho. Katika kuwatayarisha vijana kuwa mapadri, lazima kuangalia malezi ya kijana tangu seminari Kuu. Anatakiwa kuangaliwa hasa uhusiano wake na watu anaoishi nao katika mda ambao ni wakushirikishana mambo mbalimbali ili aweze kujenga mahusiano chanya na wenzake pamoja na watu wengine. Tusipolea mapadri wenye maadili Kanisa halitapata vingozi thabiti watakaoiliongoza Kanisa.” Kuwaandaa mapadri wadogo kushika nyadhifa mbalimbali katika Kanisa kama uparoko, makatibu, viongozi wa kiroho katika sekta mbalimbali za kanisa. Huku ni kuwaandaa kuwa viongozi bora wa Kanisa. 

Ameeleza pia chanagamoto za ushirikina ambazo kwa namna moja zinalikumba Kanisa na kusisitiza kwamba, iwapo viongozi hawatakuwa makini kuangalia changamoto hizo wataleta madhara ndani ya Kanisa. “Uongozi usipokuwa imara kunauwezekano wa kuwa na kutoelewana na hata kujenga mafarakano kati yetu. Aidha amewakumbusha washiriki wa Mkutano huo kushirikishana karama miongoni mwa viongozi wakuu wa taasisi zilizopo chini ya TEC na watumishi wa kada mbalimbali, ili kuleta ufanisi. Amesema “Ni lazima kuwepo na ushirikiano wa karibu baina ya uongozi yaani utawala na watumishi wengine na kufanya hivyo licha ya kuleta mafanikio, pia kutasaidia kuonyesha kwa vitendo kwamba huduma inayotolewa kwa jamii ina sura ya Kanisa,” amesisitiza.

 Ameongeza adui mkubwa kuliko wote ndani ya taasisi ni kutoelewana miongoni mwa watumishi na viongozi wao, mambo ambayo kwa kiasi kikubwa yanachangiwa na kutokuwa na maadili na ukosefu wa utiifu. Amesema,“ Umoja tu ndiyo ngao ya kujenga amani iwe ni katika ngazi ya kiuchumi ama kisiasa na hata kijamii,” katika hili nasisitiza sana hasa kwa shule za seminari kuzingatia miongozo iliyowekwa na Kanisa,”

Comments