FAHAMU KUHUSU IBADA YA SANAMU.

Na Frank Philip


“Basi, vifisheni viungo vyenu vilivyo katika nchi, uasherati, uchafu, tamaa mbaya, mawazo mabaya, na kutamani, ndiyo ibada ya sanamu; kwa ajili ya mambo hayo huja ghadhabu ya Mungu” (Wakolosai 3:5,6).

Mara nyingi watu wamedhani kwamba ibada ya sanamu ni kuweka kinyago hapo mbele yako na kuanza kukiabudu. Kwa upande mwingine, watu wameshangaa wenzao ambao wana vinyago majumbani, mahekaluni, kazini, nk., na wakiviabudu na kuviita miungu yao. Kweli unaweza ukaona hao wamepotea sana, je! Unajua Mungu anavyoingalia ibada ya sanamu? Umewahi kujiuliza ni watu wangapi wanaabudu sanamu na hawajijui huku wananyooshea wenzao vidole? Basi nisikilize vizuri, ibada ya sanamu ni ibada kamili na nitakupa maana ya mungu ili ujue ni nani mungu katikati yako.

Mungu ni kitu chochote ambacho unakipa kipaumbele na nafasi ya kwanza maishani mwako. Kwa ajili ya “mungu”, utafanya mambo uyapendayo na usioyapenda ili kumpendeza huyo “mungu” wako. Ukiweza kufanya vyema mambo upendayo na usiyoyapenda kwa ajili ya huyo “mungu”, utaitwa “mcha mungu”. Sasa ona nimeandika neno “mungu” kwa herufi ndogo nikimaanisha hapo ni “kitu chochote” na sio Mungu wetu katika Yesu Kristo.

Ukijikuta wewe unazama katika “uasherati, uchafu, tamaa mbaya, mawazo mabaya, na kutamani,” huku ukijua ufanyavyo sio sahihi mbele za Mungu, ila unafanya tu, jua hiyo ni “ibada ya sanamu”. Kwa lugha nyingine, UMESHINDWA kumcha Mungu wako kwa kuacha kufanya MATAMANIO ya moyo wako ili umpendeze Mungu.

Sasa, ni rahisi sana kuwashangaa wana wa Israel walipotengeneza “ndama wa dhahabu” na kuanza kuiabudu na “wakasema, Hiyo ndiyo miungu yako, Ee Israeli, iliyokutoa katika nchi ya Misri” (Kutoka 32:1-8). Hawa jamaa wanakumbuka mkono wa Mungu ulionyooshwa ambao uliwavusha bahari ya Shamu; wanakumbuka yale mapigo makuu juu ya Farao na Misri; wanakumbuka walivyoenda chini ya nguzo ya wingu na moto; wanakumbuka kusikia sauti ya Mungu wao. Ghafla! Wako peke yao, hakuna “kiongozi” wa kuwatazama wanachofanya, Musa “amekawia kurudi”, wamegeukia miungu mingine na kuiabudu! Hata sasa, tazama UNAPOKUWA MWENYEWE NA HAKUNA MTU ANAKUONA, unafanya nini? Je! UNAJICHAFUA na mawazo na maneno (chatting) mabaya? Je! Unazini mawazoni mwako? Kumbuka hii ni ibada ya sanamu HALISI na “kwa ajili ya mambo hayo huja ghadhabu ya Mungu” (Wakolosai 3:6).

Kumbuka siku zote, ibada ni mfumo wa maisha ya kila siku na sio kwenda kanisani tu na kutoa sadaka. Unavyoenenda mbele za Mungu wako ndio Mungu atajua kama unamwabudu Yeye au sanamu. Ukisubiri kuambudu kwenye “mlima huu au ule” jua bado hujaanza kuwa “mwabudu Mungu halisi”. Imekupasa kumwabudu Mungu katika ROHO na KWELI, na huu ni mfumo wa maisha ya KILA SIKU sio jumapili tu.

Frank Philip.

Comments