JE UNAJUA JINA LAKO LIMEBEBA NINI?



 
BWANA YESU asifiwe.


Kabla sijaokoka kuna mama mmoja ambaye alikuwa jirani yetu kule Mwanza, mama huyu alikuwa mimba  ya miezi 8, alikua na tatizo la kuchagua jina la kumpa mtoto wake kifungua mimba wake ambaye angejifungua wiki 2 baadae, akaamua kuniuliza jina gani ampe mtoto wake, kwa haraka sana nikasema ukizaa mtoto wa kiume mpe jina la Frank Yule mama akalipenda jina hilo na kweli alipozaa akamwita mtoto jina hilo yaani frank, huyo Frank yupo hata leo anasoma shule ya msingi. Lakini mama huyu hakujua kwanini mimi nilichagua jina la Frank, hakujua kabisa  ila siri nilikuwa nayo mimi moyoni. Nilipendekeza jina la Frank kwa sababu tu kuna mcheza filamu wa marekani ambaye nilikua nampenda sana anaitwa Frank Zagarino, Hivyo Frank huyu wa Tanzania ametokana na Frank Zagarino wa Marekani. 


Karibu tujifunze kitu muhimu sana yaani JINA.


Mithali 22:1 ‘’Heri kuchagua jina jema kuliko mali nyingi; Na neema kuliko fedha na dhahabu. ‘’


Kila mtu ana jina lake na jina hilo linabeba kitu kikubwa sana.



Chimbuko ya neno ‘’jina’’ linatokana na neno la kigiriki liitwalo ‘’Sum’’


‘’Sum’’ maana yake ni ukumbusho au kumbukumbu.

Kutoka 17:14 inasema ‘’  BWANA akamwambia Musa, Andika habari hii katika kitabu iwe ukumbusho, kisha ihubiri masikioni mwa Yoshua; ya kuwa nitaufuta ukumbusho wa Amaleki kabisa, usiwe tena chini ya mbingu. ‘’

Ukumbusho au Sum kama ilivyoandikwa katika Biblia ya kigiriki maana yake ni jina Hivyo kwenye hilo andiko unaweza kusema kwamba ‘’MUNGU atalifuta jina la Amaleki’’



-Kwa hiyo maana ya kwanza ya jina/sum ni ukumbusho ambao mtu anapewa.


-Jina/sum maana yake ni alama ya pekee ambayo anapewa mtu ili kumtofautisha na wengine.


-Jina/sum ni zawadi ya pekee ambayo mtu anapewa.


Vigezo vya kumpatia mtu jina hutofautiana.

Majina mengine huwakilisha heshima  ya kipekee.

Wafilipi 2:9-11( Kwa hiyo tena MUNGU alimwadhimisha mno, akamkirimia Jina lile lipitalo kila jina; ili kwa jina la YESU kila goti lipigwe, la vitu vya mbinguni, na vya duniani, na vya chini ya nchi; na kila ulimi ukiri ya kuwa YESU KRISTO NI BWANA, kwa utukufu wa MUNGU Baba. )


Majina mengine huwakilisha sifa ya huyo anayepewa jina .

Mfano rais wanchi ni jina la sifa ambalo anapewa mhusika.

Majina mengine ni kuonyesha mamlaka mfano Askari ni jina ambalo linaonyesha mamlaka.


Kwa sababu ya tabia Fulani Fulani baadhi ya majina hutokea.


Mfano mwingine JEHOVAH SHALOM maana yake MUNGU ni mani yetu hili ni jina jema ambalo linatokana na sifa ya MUNGU katika kuleta amani kwa watu wake.


Mfano Paka amepewa jina la Nyau kwa sababu tu ya kulia nyauuuuu.


Kuna mtu anaitwa Chausiku na jina hilo alilipata baada tu ya kuzaliwa usiku.


Mimi sijui wewe unaitwa nani na jina lako linatokana na nini. Maana majina yanabeba jambo kubwa sana kwa mhusika.


Mfano mtu mchafu anaweza kupewa jina kutokana na uchafu wake ni jina hilo likamshika na kushika maisha ya mtu husika huyo.

Hata mpole anaweza kupewa jina kwa sababu tu ya upole wake, je jina lako ni nani? Na linatokana na nini, je jina lako linatokana na kitu chema au kibaya?


Je jina lako limebeba Baraka? Au laana?


Mfano hai ni hivi Mimi naitwa PETER MICHAEL MABULA.

Maana ya majina yangu ni hii; 


-Peter  maana yake mwamba au jiwe Yohana 1:42.

Kumbuka pia BWANA YESU alimwambia mtume Petro kwamba  ‘’ Juu ya Mwamba huu nitalijenga kanisa langu na wala milango ya kuzimu haitaliweza.’’ Mwamba ni maana  ya Peter lakini hapa BWANA YESU alikuwa anazungumzia mitume wote yaani juu ya mitume injili ya KRISTO itasonga mbele na ndio maana Imani yetu imejengwa juu ya mitume na manabii’.


-Michael maana yake ‘’Ni nani aliye kama MUNGU?’’


-Mabula ni jina la kisukuma ambalo maana yake ni ‘’mtoto wa kiume aliyezaliwa wakati wa mvua.’’

Mabula inatokana na mbula kwa kisukuma ambapo mbula maana yake mvua, hivyo mtoto wa kiume akizaliwa wakati wa mvua anaweza akaitwa Mabula na majina haya ni mengi sana usukumani yaani Mwanza kwetu, na kama mtoto akizaliwa wa kike wakati wa mvua huitwa Kabula ikiwa na maana sawa na Mabula ila tu Mabula ni wa kiume na Kabula ni wa kike.


Je jina lako ni nani? 


Je jina lako limebeba nini? 


Limebeba uzima au mikosi, limebeba Baraka au lina maagano na mashetani?


 Kwa msaada tu kama utapenda kujua maana ya jina lako fungua Blog yangu  ya Maisha ya ushindi  na kwenye Research/ Tafuta andika maneno haya ‘’MAJINA NA MAANA ZAKE’’ Utaona majina zaidi ya 200 na maana zake. Ubarikiwe na tunaendelea na somo.


Kwa hiyo mtu anaweza kupewa jina kulingana na cheo au sifa.

AINA KUU 2 ZA MAJINA.



1.  Jina ambalo mtu anapewa na wazazi wake au jina la Asili.

2.  Jina kutoka nje ya familia kutokana na sifa za mtu huyo.

Mfano kuna watu wanaitwa ‘’Kahaba’’ au ‘’Mwizi’’ hayo ni majina ila yanatokana na tabia.



Je jina lako ni nani?

Tafakari jina lako je umelipataje?

 Je jina lako linatokana na nini?


Ni muhimu sana kujua maana ya jina lako na chanzo chake maana jina linaweza kubeba laana au Baraka.

Kuna majina hutokana na ukoo au kabila, haya ni ya kuchunga sana maana koo zetu nyingi hawajaokoka hivyo ni rahisi sana kupewa jina ambalo lina maagano na mizimu na kukupelekea kupata majanga maishani.


Luka 1:59-61” Ikawa siku ya nane wakaja kumtahiri mtoto; wakataka kumpa jina la babaye, Zakaria. Mamaye akajibu akasema La, sivyo; bali, ataitwa Yohana. Wakamwambia, Hapana mtu katika jamaa zako aitwaye jina hilo. “

Kwenye hayo maandiko juu Unaweza kujiuliza kwanini MUNGU aliamua kutoa jina kwa Yohana mbatizaji? Huku ndugu  wakitaka jina la ukoo?

MUNGU alijua kabisa kwamba jina hilo la ukoo lisingeweza kulitimiza kusudi lake.


Kumbe kuna majina hayawezi kutimiza makusudi ya MUNGU. Ndio maana kuna kuokoka, pia ndio maana kuna ubatizo ili tu kuzika utu wa kale na maagano ya ukoo na mizimu na kabila ambao mengine hutokana  na maagano ya kishetani.


Wazazi na wale ambao mtakuwa wazazi baadaye nawaombeni mliangalie sana jambo hili yaani jina ambalo mtampa mtoto wenu.

Sio vizuri kuiga jina.


Nampenda sana BWANA YESU maana jina YESU maana yake ni ‘’Mtu mwenye kuokoa’’


Wapo watu wengi kutokana na majina yao wameshindwa kutimiza kusudi la MUNGU.


Ibrahimu kabla hajaitwa hivyo aliitwa Abram, MUNGU aliona Abram haiwezi kulitimiza kusudi lake ndio maana akambadili jina la kumwita Ibrahimu. Mwanzo 17:5 (wala jina lako hutaitwa tena Abramu, lakini jina lako litakuwa Ibrahimu, kwani nimekuweka uwe baba wa mataifa mengi. )

Hata Sara mwanzo aliitwa Sarai, MUNGU akambadilishia jina na kumwita Sara ambalo maana yake ni ‘’Binti mfalme’’ Mwanzo 17:15 (MUNGU akamwambia Ibrahimu, Sarai mkeo, hutamwita jina lake Sarai, kwa kuwa jina lake litakuwa Sara ).

Je unauona umuhimu wa jina?


Yakobo haikuwepo kwenye mikakati ya MUNGU ndio maana akaitwa Israeli.


Ndugu yangu nakuomba usipokee tu jina mradi ni jina.

Mwanzo 41:45 ( Farao akamwita Yusufu, Safenath-panea; akamwoza Asenathi, binti Potifera, kuhani wa Oni, kuwa mkewe Yusufu akaenda huko na huko katika nchi yote ya Misri. )
Hapa Farao alimpa jina jipya Yusufu lakini jina hilo halikufanya kazi na likafutika maana Yusufu ilikuwa jina linalotimiza kusudi la MUNGU.

Hesabu 13:16 ( Hayo ndiyo majina ya hao watu waliotumwa na Musa waende kuipeleleza nchi. Na huyo Hoshea mwana wa Nuni, Musa akamwita jina lake Yoshua. ) 
Hapa jina Hoshea halikuwa linatimiza kusudi ndio maana akaitwa Yoshua maana yake mkombozi.


Kuna watu wamerithi majina  na majina hayo yanawatesa sasa.

 Wapo waliorithi majina ya bibi zao walikuwa wanasumbuliwa na magonjwa Fulani, lakini licha ya kupita miaka mingi kwa sasa wajukuu zao waliorithi majina hayo, wanasumbuliwa na magonjwa yale yale yaliyowatesa hadi kuwaua bibi zao.


Wewe Mzazi nakusihi; Mpe mwanao jina linalomtukuza MUNGU.

Mithali 18:21 ( Mauti na uzima huwa katika uwezo wa ulimi; Na wao waupendao watakula matunda yake. )

Hata MUNGU aliumba kwa kutamka hivyo kuna nguvu katika kutamka. Hivyo wewe unayeitwa sura mbaya, hao watu wanaokuita hivyo wanakuumbia sura mbaya , hakika utakuwa sura mbaya na hakuna atakayetaka kukuoa sura mbaya.

Tafuta maana ya jina lako.



Inawezekana jina lako linatengeneza Baraka au laana.

Na kama jina lako lina maagano ya kiukoo au kikabila, au jina lako limekusababishia mabaya kila siku  dawa yake ni kuokoka tu maana Biblia inasema katika 2 Kor 5 :17 kwamba ‘’ Hata imekuwa, mtu akiwa ndani ya KRISTO amekuwa kiumbe kipya; ya kale yamepita tazama! Yamekuwa mapya. ‘’


Wengine wanafilisika kwa sababu tu majina yao yanawafilisi.

Mithali 22:1 ‘’Heri kuchagua jina jema kuliko mali nyingi; Na neema kuliko fedha na dhahabu. ‘’

Usikubali jina lililo na maagano ya mababu, wala usikubali jina leye ushetani ndani yake.

1 Samweli 25:25 (Nakusihi, bwana wangu, wewe usimwangalie huyu mtu asiyefaa, yaani, Nabali; kwa maana kama lilivyo jina lake ndivyo alivyo yeye; jina lake ndilo Nabali, na upumbavu anao; lakini mimi, mjakazi wako, sikuwaona hao vijana wa bwana wangu aliowatuma. )

Nabali maana yake ni mpumbavu.

Sasa kama jina lako wewe ni mpumbavu je upumbavu utakaa mbali na wewe?


Wewe mzazi ni vizuri ukaangalia jina Zuri kwenye Biblia ili kumpa mtoto wako.

Mwite mtoto wako jina linaloleta utukufu kwa MUNGU.

Yawezekana hujaokoka na ndio maana unaitwa ‘’Mwenye dhambi’’ Hivyo ni vyema kufuta jina hilo kwa kuokoka.

Yohana 1:12-13  ‘’ Bali wote waliompokea aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa MUNGU, ndio wale waliaminio jina lake;
13 waliozaliwa, si kwa damu, wala si kwa mapenzi ya mwili, wala si kwa mapenzi ya mtu, bali kwa MUNGU. ‘’ 



Kwa sasa naishia hapo, MUNGU akitupa nafasi tutajifunza tena siku nyingine.na kama hujampokea BWANA YESU muda wa kumpokea ni leo wala sio kesho, amua leo na atakuandika jina lako katika kitabu cha uzima na utaanza kuukulia wokovu kwa mafundisho kanisani. ROHO MTAKATIFU aliyenipa ujumbe huu ana makusudi kabisa na wewe, hataki upotelee motoni anataka uende uzimani aliko KRISTO BWANA.
                     MUNGU akubariki sana .
                      Ni mimi ndugu yako
                       Peter M Mabula
                 Maisha ya Ushindi Ministry.
                           0714252292
                 MUNGU akubariki sana uliyesoma somo hili.
 MUNGU Akubariki.

Comments

Unknown said…
ubarikiwe