JINA LA YESU

Na Frank Philip


“Kwa sababu, ukimkiri Yesu kwa kinywa chako ya kuwa ni Bwana, na kuamini moyoni mwako ya kuwa Mungu alimfufua katika wafu, utaokoka. Kwa maana kwa moyo mtu huamini hata kupata haki, na kwa kinywa hukiri hata kupata wokovu. Kwa maana andiko lanena, Kila amwaminiye hatatahayarika. Kwa maana hakuna tofauti ya Myahudi na Myunani; maana yeye yule ni Bwana wa wote, mwenye utajiri kwa wote wamwitao; kwa kuwa, Kila atakayeliitia Jina la Bwana ataokoka” (Warumi 10:9-13).

Jina la Yesu ni jina lipitalo majina Yote. Hii ni kauli iliyozoeleka sana lakini sio kila mtu anajua UMUHIMU wa “kuliitia” Jina la Yesu. Hapa sizungumzii KUOMBA, nazungumzia kuliitia JINA la Yesu peke yake.

Mara nyingi sana watu wanatazama huu mstari ila hawajagundua kwamba unasema “KILA ATAKAYELIITIA Jina la Yesu” na sio “kila mtumishi wa Mungu atakayeliitia Jina la Yesu”. Kwa sababu baadhi ya watu wamedhani “wao hawastahili” kuliitia Jina la Yesu, basi wanakosa imani ndani yao, na kupata matokeo hafifu au bila matokeo kabisa wanapoliitia Jina la Yesu. Hila Jina halina mwenyewe, ni la KILA mtu kulitumia hata kama DINI yako sio ya kwenda kanisani, we ita tu Jina la Yesu utaona matokeao yako.

Nina shuhuda za watu ambao sio wakristo kabisa, wala hawajawahi kwenda kanisani ila wamewahi kusikia kwamba mtu akikemea kwa Jina la Yesu mambo yanatokea. Katika hali fulani ngumu wameliitia Jina la Yesu na wamepata msaada. Sasa kama unafikiri Jina la Yesu lina mwenyewe, bado hujamjua huyu Yesu. Yesu anasema “Njooni kwangu NINYI NYOTE wenye kusumbuka na kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha”. Yesu anawaita watu WOTE waje kwake, na kuwahudumia bila mipaka ya dini.

Hebu wafundishe watoto wako wadogo kuliitia Jina la Yesu hata kama hawajui kuomba. Hilo Jina ni ngao ya mambo yote na limeokoa wengi. Nimesikia shuhuda mbalimbali ambazo watoto wadogo wamekutana na hali za hatari wakiwa peke yao, na hawajui kuomba ila wanajua Jina la Yesu tu; wametamka tu “Jina la Yesu” na wamekuwa salama kwa maana tunaambiwa “KILA ATAKAYELIITIA JINA LA YESU ATAOKOKA”.

Sasa najua wengi wanadhani KUOKOKA ni kuwa MLOKOLE tu! Hapana. Yapo mambo mengi ambayo unahitaji kuokolewa nayo. Kumbuka, hata kama wewe ni mlokole, na uko karibia na kupata ajali, unahitaji kuokolewa na hiyo ajali, liitie Jina la Yesu mara moja na utaona wokovu mkuu.

Chukua ushauri huu na uanze kutumia Jina la Yesu hata kama wewe sio Mkristo au Mlokole. Yesu atakuja kukusaidia katika shida yako. Ndipo utakapogundua kwamba kama Jina la Yesu ni BIDHAA, basi hiyo sio bidhaa ya kununua kwa sababu KILA mtu anayo BURE. Ukisikia mahali pesa inahitajika kwa ajili ya KAZI iliyofanyika kwa Jina la Yesu, jua sio huyu Yesu aliyesulubiwa, akafa na kufufuka, kisha akapaa Mbinguni.

Sasa jua kuna wakati utahitaji kusaidiwa BAADHI ya mambo ya kiroho na watumishi wa Mungu. Ikifika mahali pa kuhitaji msaada ZAIDI, chukua hatua, nenda kwa watumishi wa Mungu, ila kwa kuanzia, hilo Jina unalo tayari, liitie tu, utaona matokeo mazuri hapo ulipo.

Frank Philip.

Comments